MAONI: Kifo cha Glory kitukumbushe kupima afya zetu

Juzi meneja mawasiliano na uhusiano wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Glory Mziray alimaliza safari yake ya mwisho duniani kwa kifo cha ghafla.

Glory alifikwa na mauti akiwa ofisini kwake Jengo la Mpingo (zamani Wizara ya Maliasili na Utalii) wakati akizungumza na waandishi wa habari ambako ghafla aliishiwa nguvu na baada ya kufikishwa hospitalini madaktari walidhibitisha kwamba alishafariki dunia.

Kabla ya kufikwa na umauti, meneja huyo alioneka akiwa amejiandaa vilivyo kutekeleza jukumu lake lakini alishindwa kumalizia kazi hiyo. Hivyo ndivyo, mama huyo alivyomaliza muda wake hapa duniani. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.

Taarifa za kitabibu zinasema kuwa Glory alikuwa na tatizo la shinikizo la damu au shambulio la moyo na hata historia ya ugonjwa kutoka kwa familia yake zilieleza hivyo.

Shinikizo la damu ni miongoni mwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaua watu wengi.

Ugonjwa huu unasababishwa na nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa kuwa kubwa kuliko kawaida na hivyo kusababisha moyo kufanya kazi kupita kiasi ili uzungushe damu katika mishipa.

Unafahamika pia kama ugonjwa unaoua taratibu kwani si mara zote unakuwa na dalili za wazi na hivyo kufanya wengi wasijitambue.

Utafiti uliofanyika nchini Uingereza, umeonyesha kuwa asilimia 30 ya wakazi wake wana presha ya kupanda bila ya kujitambua.

Inaelezwa kuwa tatizo hili likiendelea kuachiwa bila ya kutibiwa, linasababisha kuongeza hatari ya kupata mshtuko wa moyo au kiharusi.

Si athari hizo pekee, ugonjwa huo pia unasababisha mshtuko wa moyo ambao hushindwa kufanya kazi na pia unaweza kusababisha ugonjwa sugu wa figo.

Kifo kama cha Glory si kigeni katika jamii zetu, mara kadhaa tumeshuhudia watu wa rika tofauti wa kawaida, maarufu na wenye madaraka wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huu.

Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kwamba wengi wanaopata ugonjwa huu na kupoteza maisha hugundulika katika dakika za mwisho kabisa.

Hali hii inaelezwa kuwa inatokana na watu kutokuwa na tabia ya kupima afya zako na badala yake wanasubiri mpaka waugue au kupata dalili za wazi.

Ni wazi kwamba ugonjwa huu ni changamoto kubwa katika jamii yetu. Si tu mamlaka husika zinapaswa kuwajibika, lakini kwanza jitihada za makusudi zinapaswa kuwekwa kwa watu wenyewe kubadilisha mfumo wa maisha.

Tukio la Glory litukumbushe tabia ya kuangalia afya kwa kupima mara kwa mara badala ya kusubiri mpaka uugue.

Kwa kuchunguza afya zetu, mgonjwa atagundua mapema na kupatiwa matibabu kabla hali haijawa mbaya.

Jambo lingine ni kubadili mfumo wetu wa maisha. Tunapaswa kuepuka vyakula vyenye chumvi nyingi, mafuta mengi, punguza kiasi cha nyama nyekundu, kuepuka matumizi ya pombe na kula matunda na mbogamboga kiasi cha kutosha katika kila mlo.

Ushauri mwingine ni kutopuuza mabadiliko ya mwili kwani wapo wanaoona mabadiliko hayo na kuendelea na kazi kama kawaida badala ya kwenda kupima na kugundua tatizo.

Lakini pia wale waliogundulika kuugua ugonjwa huu hawana budi kufuata ushauri wa madaktari ikiwa ni pamoja na kutumia dawa kikamilifu kama walivyoelekezwa na wataalamu.