MAONI: Kughushi vitambulisho ni uhujumu uchumi

Friday June 7 2019

 

Juzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alifanya ziara maeneo ya Kariakoo kukagua matumizi ya vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo maarufu vitambulisho vya wajasiriamali au wamachinga.

Vitambulisho hivyo vilianza kugaiwa kwa wafanyabiashara hao nchini Desemba 10 mwaka jana na Rais John Magufuli kwa kugawa vitambulisho 670,000 kwa mikoa yote nchini.

Lengo la vitambulisho hivyo ni kuwatambua wafanyabiashara ndogo nchini ili wafanye shughuli zao bila kusumbuliwa na ili kupata kitambulisho hicho kila mfanyabiashara au mjasiriliamali mdogo anatakiwa kulipa kiasi cha 20,000.

Wakati utaratibu wa kugawa vitambulisho hivyo ukiendelea nchini kote, jijini Dar es Salaam, mkuu wa mkoa kupitia ziara yake hiyo akabaini kuwapo tatizo la baadhi ya wafanyabiashara hao kughushi vitambulisho hivyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Makonda katika ziara yake akiwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa pia waligundua kwamba kuna wafanyabiashara wanaotumia kitambulisho kimoja huku wakiwa na meza zaidi ya moja ya biashara.

Zaidi ya hilo, Makonda pia alidai kugundua wafanyabiashara wanaoazimana vitambulisho hivyo na wengine kukodishana kwa malipo ya Sh1,000 ili ukaguzi unapofanyika aonekane yupo salama.

Matukio yote hayo ni kielelezo cha kuwapo hujuma katika vitambulisho hivyo ambavyo tunaamini pamoja na mambo mengine vina malengo makuu mawili, moja ni kuhakikisha wafanyabiashara hawabughudhiwi wawapo kazini na pili ni nia ya Serikali kukusanya mapato.

Mambo yote hayo yana umuhimu wake na ndio maana tunasema kwamba yeyote anayekiuka au kwenda kinyume na utaratibu huo anahujumu uchumi wa nchi na kwa mantiki hiyo vyombo vya sheria vina wajibu wa kumkamata na kumuadhibu.

Serikali inapoanzisha utaratibu wenye lengo la kukusanya kodi halafu akatoke mtu wa kuhujumu utaratibu huo ni wajibu wa Serikali na mamlaka zake kumshughulikia mtu huyo kwa mujibu wa sheria.

Japokuwa jambo hili limezungumzwa jijini Dar es Salaam, tunaamini ni vyema uchunguzi ukafanyika na kwingineko Tanzania kwani huenda nako hali ikawa hiyo hiyo ambayo imeanza kujitokeza jijini Dar es Salaam.

Kwa maana hiyo wakuu wa mikoa na wilaya nchini ni vyema wakaanza msako maalumu wa kuwakamata wale wote wanaohujumu matumizi ya vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo ndogo na kuhakikisha mkono wa sheria unawaangukia.

Wakuu wa mikoa na wilaya watakuwa wamefanya kosa kubwa kama wakijiaminisha kwamba tatizo liko Dar es Salaam pekee na kwamba wako salama.

Zaidi ya hilo kwa kuwa tayari ugawaji wa vitambulisho hivi upo nchini kote ni vyema Serikali ikaja na ufafanuzi zaidi wa ni nani hasa mhusika wa vitambulisho hivi ili kuondoa mkanganyiko uliojitokeza katika siku za karibuni.

Wakati tukifahamu kuwa vitambulisho hivyo ni kwa wafanyabiashara ndogondogo wasiozidi kipato cha Sh4 milioni kwa mwaka, hivi karibuni tumesikia habari za makundi mengine yakitajwa kutakiwa kuwa na vitambulisho na hivyo kuzua mkanganyiko.

Kuondoa utata huo ni vyema ufafanuzi ukatolewa na mamlaka husika ili waliochanganywa na ongezeko la makundi wakawa na uhakika kama wanahusika na vitambulisho hivyo au hawahusiki.