UCHAMBUZI: Ramaphosa ameunda Baraza la kukusanya kodi

Friday June 7 2019

 

By Julius Mnganga

Rais John Magufuli anakutana na wafanyabiashara maarufu watano wa kila wilaya kesho, ukiwa ni mwendelezo wake wa kuzungumza na wadau wa sekta binafsi.

Alishakutana na wachimbaji wadogo wa madini, akapokea maoni na ushauri wao ambao Serikali iliahidi kuufanyia kazi. Zaidi ya mara moja amekutana na wafanyabiashara wakubwa na kubadilishana nao uzoefu.

Bado ninaukumbuka mkutano wa Dk Magufuli na watendaji wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alipoitaka kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kuongeza idadi ya walipakodi.

Kwenye mkutano huo, alisema Tanzania yenye zaidi ya watu milioni 55, ina walipakodi milioni 2.27 tofauti na nchi nyingine ambazo zina watu wachache lakini zinatuzidi kwa idadi ya walipakodi. Katika mifano mingi aliyoitoa kujenga hoja hiyo, alisema Msumbiji yenye watu milioni 27 ina walipakodi milioni 5.3. Ingawa tumeizidi idadi ya watu, lakini inatushinda kwa walipakodi. Na Afrika Kusini iliyo na watu milioni 56.52 ina walipakodi milioni 19.98.

Maneno haya yanadhihirisha mapungufu yaliyopo katika kutengeneza na kuwaandaa walipakodi nchini. Hata kama TRA inaimarisha ukusanyaji kila mwaka, wachache ndio wanaoumia kwani wanalazimika kukamuliwa.

Siku chache zilizopita Afrika Kusini walimwapisha rais mpya waliyemchagua, Cyril Ramaphosa kwenye hafla ambayo Rais Magufuli alihudhuria pia. Muda mfupi baadaye, Ramaphosa alitangaza baraza lake la mawaziri 28.

Ni baraza hili ndilo lililonipa tafakuri. Achana na sekta ya elimu ambako amewateua mawaziri wawili; atakayesimamia elimu ya msingi na atakayeangalia elimu ya juu, sayansi na teknolojia, viwanda na biashara imepewa kipaumbele cha aina yake.

Kuna wizara tano katika eneo hilo ambazo, endapo watendaji wake watachapa kazi, lazima watutangulie kiuchumi kwa kuwa na idadi kubwa ya walipakodi wanaochangia pato la Taifa kwa usawa bila kuumiza kundi dogo kama ilivyo hapa kwetu.

Ramaphosa ameunda wizara ya biashara na viwanda kama ilivyo hapa kwetu lakini kuongeza ushiriki wa wananchi, kuna wizara ya ushirika na mambo ya kijamii, na wizara ya mashirika ya umma.

Ushirika unaowajumuisha wakulima wa mazao tofauti ya biashara huku ukiwa na uwezekano wa kuwajumuisha vijana hasa wahitimu wa ngazi tofauti ambao wanaweza kuanzisha biashara ya bidhaa au huduma tofauti kwa kutumia maarifa waliyonayo.

Kuna fursa kubwa ya kuongeza mapato ya kodi kutoka kwa wanachama wa vyama vya ushirika vilivyopo au vitakavyoanzishwa. Vilevile, Tanzania ina mashirika 253 lakini kwa mwaka 2017/18 ni 24 tu ambayo ni sawa na asilimia tisa yametoa gawio serikalini. Nadhani Ramaphosa hatamuelewa waziri wake utendaji ukiwa hivi.

Ufanisi wa mashirika haya yanaongeza uwezekano wa kujitanua, kuajiri zaidi hivyo kukuza mapato ya kodi na mengineyo kwa Taifa. Hii ni sehemu ya kwanza ambayo Tanzania inapoteza chanzo cha uhakika cha mapato tofauti na Afrika Kusini.

Lakini, Ramaphosa ameunda wizara ya maendeleo ya biashara ndogo ndogo pamoja na wizara ya huduma za jamii na utawala. Kuna tofauti, ingawa inaweza isionekane kwa urahisi.

Nchini, waziri wa viwanda na biashara anazungumza na mabilionea wa ndani au kimataifa halafu anahitaji kuzungumza na wamachinga. Yaani akimalizana na Said Bakhresa anayekerwa na maziwa yake kuzuiwa kuingizwa Bara akakutane na wamachinga wa Mbinga mjini.

Ramaphosa kaweka mawaziri wawili hapa. Mmoja anataka aachane na suti na aingie mtaani akazungumze na wamachinga na kutoa miongozo kwa wakati kuepusha mkanganyiko wowote unaoweza kutokea. Ufanisi wa waziri huyu bila shaka utakuwa kurasimisha wamachinga wengi zaidi.

Hii, kwa mtazamo wangu naona inatutofautisha sana na Afrika Kusini. Waziri wa wamachinga hatakiwi kuwafuata na gari kubwa tena akiwa amezungukwa na walinzi pamoja na wasaidizi. Anatakiwa kufanana nao kwa haiba.

Kama zilivyo wizara mbili za elimu ambazo zitaandaa wananchi wenye ujuzi unaotakiwa ukizingatia mahitaji ya soko na kila waziri kuhakikisha anaboresha eneo lake, wizara ya huduma za jamii na utawala ikipokea vipaumbele vya waziri wa wamachinga, vyama vya ushirika au biashara na viwanda, lazima Afrika Kusini iwe na idadi kubwa ya walipakodi kuliko Tanzania.

Julius ni mwandishi wa Mwananchi. Anapatikana kwa 0759 354 122