Serikali itamke ubakaji kwa watoto ni janga

Ni saa moja jioni katika Kijiji cha Mbegu, Wilaya ya Matombo. Kibena Mzeru, binti mwenye miaka sita, ametumwa dukani na mama yake kununua sukari. Anakwenda bila wasiwasi, tena akiimba ili asisahau alichotumwa. Lakini ghafla, anatokea kijana, mwenye misuli, anamshika na kumbaka.

Mama yake Kibena anapoona binti yake anachelewa, anamfuata, lakini akiwa njiani kabla ya kufika dukani, anamuona binti yake akiwa ametupwa kichakani, amepoteza fahamu. Baada ya kumchunguza zaidi, anabaini kuwa amebakwa.

Hizi ndizo kesi, zinazoripotiwa mara kwa mara katika vyombo vya habari, zikionyesha matukio ya ubakaji kwa watoto.

Wakati tukielekea kuadhimisha; ‘Siku ya mtoto wa Afrika’ Juni 16 mwezi huu, ni vizuri Taifa likakiri sasa kuwa ubakaji wa watoto ni janga. Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yanakwenda na kauli mbiu isemayo: ‘Mtoto ni msingi wa Taifa endelevu, tumtunze, tumlinde na kumuendeleza.’

Kwa kutambua kuwa hili ni janga, ndipo tutakapotafuta njia nyingine mbadala za kuzuia au kupambana na wabakaji.

Ripoti iliyochapishwa na Tume ya Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Juni mwaka jana, ilionyesha kuwa watoto wa kike 2,365 wenye umri wa miaka mitatu hadi 14 walibakwa katika kipindi cha Januari hadi Juni 2018.

Januari hadi Juni mwaka huo huo, watoto wa kiume 53 walibakwa.

Ukiangalia takwimu hizo kwa mwaka 2017 na 2018, inaonyesha dhahiri kuwa ubakaji unaongezeka. Kwa mfano, mwaka 2017, watoto wa kike waliobakwa walikuwa 759 na wa kiume walikuwa 12 tu.

Utafiti wa LHRC unaonyesha kuwa kuna ongezeko la matukio ya ubakaji kutoka 4,728 mwaka 2017 hadi 6,376 mwaka 2018.

Akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, mwaka 2016, Dk Harrison Mwakyembe alisema kwamba kesi 19 za ubakaji zinaripotiwa kila siku katika kipindi cha mwaka 2012-2015. Hii inatosha kusema ubakaji ni janga na ubakaji wa watoto ni janga zaidi.

Serikali imefanya mengi katika masuala ya sheria na sera kuhusu ubakaji, hasa ile ya kifungo cha miaka 30 au maisha kwa kosa la ubakaji, kwa hili tunaipongeza. Hata hivyo, bado kuna hatua zaidi zinazotakiwa kufanyika ili kuonyesha uzito wa tatizo hili la ubakaji.

Kama zilivyowahi kufanyika kampeni nyingine zenye mafanikio, kwa mfano ‘Afya yako, Mtaji wako’ au ile ya upimaji Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wajawazito, au ile ya fistula basi hali kadhalika suala la ubakaji kwa watoto nalo linahitaji mkakati kazi, mpango madhubuti na kelele nyingi.

Madhara ya ubakaji kwa watoto siyo tu yanaathiri watendaji kazi wa Taifa la kesho, bali pia maendeleo ya kielimu, kiafya na mchangamano wa kijamii.

Kwa nini nasema ubakaji kwa watoto utamkwe rasmi kuwa ni janga kwa Taifa, ni kwa sababu ifuatazo;

Kwanza ripoti ya 2016 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) inasema kwamba ubakaji kwa watoto unafanywa na watu walio karibu yao, yaani baba, mjomba, jirani, kaka au babu.

Hii ina maana kuwa, wanafamilia wa karibu ndiyo maadui wakubwa wa watoto wetu. Je, tutawaficha wapi watoto hawa? Ukiwaficha ndani, wabakaji wapo ndani, ukiwatoa nje, wabakaji pia wapo huko.

Lakini jingine linalofanana na hilo, ni kuwa kama wabakaji ni miongoni mwa wanafamilia, aghalabu kesi zake huwa hazifikishwi mahakamani.

Utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) umebaini kuwa mara kadhaa kesi za ubakaji haziripotiwi au hata kama zikiripotiwa hazifiki mahakamani kwa sababu wabakaji ni ndugu wa familia na hivyo hulindana na kumaliza tatizo kindugu.

Kingine kinachosababisha ubakaji wa watoto uitwe janga, ni maradhi, mimba. Ubakaji mara nyingi husababisha maradhi, kwa mfano Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa lakini wakati mwingine ni mimba.

Kama idadi hii ya watoto wanaobakwa itaongezeka, miaka ijayo tujue kabisa kizazi chetu kitakuwa na maradhi.

Sababu nyingine ni uwepo wa sheria na ongezeko la ubakaji. Licha ya sheria ya makosa ya jinai kuweka adhabu ya miaka 30 au kifungo cha maisha kwa mbakaji, lakini idadi ya watoto wanaobakwa inaongezeka. Kwa nini?

Wazazi kutokujua sheria, kuona uvivu kufuatilia kesi, kupewa rushwa na watuhumiwa ili wavunje kesi na kubwa zaidi ni kuona aibu kuripoti kuwa mtoto kabakwa. Hili nalo linaongeza makali ya janga hili.

Heko Serikali kwa kuanzisha kamati za ulinzi wa wanawake na watoto, kutunga sheria na kuanzisha vituo vya huduma zote kwa pamoja (one stop centre). Lakini bado ubakaji upo, unatisha na unaathiri taifa la kesho.

Mwandishi wa uchambuzi huu ni mfanyakazi wa Tamwa, anapatikana kwa namba 0764438084