UCHAMBUZI: Beki wa pembeni ni mchezaji muhimu timu kupata ushindi

Monday January 14 2019

 

Kuimarisha ulinzi

Wajibu wa kwanza wa walinzi wa pembeni ni kulinda goli la na kuhakikisha kwamba mipira ya krosi haichezwi na timu pinzani kuelekea kwao.

Ifahamike kwamba ulinzi mzuri ni ule ambao huyu wa pembeni anakuwa sehemu sahihi kutegemea mpira uko eneo na upande gani wa uwanja.

Mathalani, pale timu yake inaposhambulia na kupoteza mpira katika eneo la mwisho wa uwanja, matarajio ni kwamba walinzi hawa wa pembeni watakuwa maeneo sahihi ambayo yataifanya timu isiache maeneo wazi.

Kinachoonekana kwenye mechi nyingi ni kwamba walinzi hawa wanabaki pembeni mwa uwanja na hivyo kusababisha eneo la kati kuwa wazi hivyo huwapa kazi ya ziada walinzi wa kati na viungo wa asili.

Matokeo ya kutotimiza wajibu huo ni washambuliaji kufunga magoli kirahisi kwa kutoilinda miamba kivuli na kutocheza kama walinzi wa kati vivuli.

Tumeshuhudia mara nyingi mwamba wa pili ambako mpira hautokei ukiwa wazi na hivyo magoli kufungwa kirahisi.

Kinachotegemewa hali hiyo ya timu kushambuliwa inapotokea, ni kwamba mlinzi aliye upande wa kivuli, ahakikishe kwamba mwamba wa goli wa upande wake uko salama.

Aidha, tumeshuhudia pia pale ambako walinzi wa kati wameegemea upande mmoja kutokana na shambulizi la timu pinzani, walinzi wa pembeni hushindwa kuingia eneo la kati na kucheza kama walinzi wa kati wasaidizi, hivyo kuacha eneo wazi ambalo hutumiwa na washambuliaji kufunga kirahisi.

Kinachotegemewa ni walinzi wa pembeni kucheza kama walinzi wa kati kivuli ili kuilinda timu isifungwe.

Kutocheza kama washambuliaji wa pembeni.

Mtiririko wa mpira kwa sasa unategemea sana uwezo wa walinzi wa pembeni kushiriki katika ushambuliaji kwa kutumia mapana ya uwanja.

Wajibu huu kwa mpira wa sasa ni muhimu kwa sababu washambuliaji wa pembeni wamebadilishiwa majukumu na kucheza eneo la kiungo. Timu nyingi zimeshindwa kuwa na walinzi wa pembeni wenye kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Nikiangalia, jambo ambalo wengi linawashinda kutekeleza jukumu hilo, ni walinzi hawa kutokuwa kwenye eneo sahihi wakati timu yao inaposhambulia hivyo kuliona eneo la pembeni kulifikia kuwa mbali.

Kutotimiza majukumu hayo kunapunguza raha ya mpira kwa sababu mashambulizi ya kutokea pembeni yanakuwa machache na msisimko wa ushambuliaji unapungua.

Kucheza kama washambuliaji wa asili kivuli

Mchezaji wa nafasi hii ya ulinzi wa pembeni anatakiwa acheze pia kama mshambuliaji kivuli kila inapobidi.

Muda mzuri wa kufanya hivyo ni pale ambapo shambulizi la timu yake kwenda timu pinzani limefika robo ya nne na liko upande wa pili wa mlinzi wa pembeni.

Ambacho mara nyingi tunashuhudia, eneo ambalo huwa linakuwa wazi na zuri kwa mlinzi wa pembeni kuwapo na linaweza pia kutumika kufunga, ni lile kwenye nafasi kivuli ya namba nane au kumi kutegemea mpira umetokea wapi.

Walinzi wengi wa pembeni hawafiki maeneo hayo na matokeo yake wanashindwa kuongeza uwezo wa wao wa kufunga na kuzipa timu zao ushindi.

Wachache ambao wanatimiza majukumu haya ni kama vila alivyokuwa Shomari Kapombe (ambaye kwa sasa ni majeruhi).

Kwa wenzetu wa Ulaya, unawaona walinzi kama Marcelo wa Real Madrid. Walinzi hawa wakumbuke kwamba ukiwa unacheza nafasi hiyo na ukatimiza jukumu muhimu, hili la kufunga unajiongezea thamani.

Kushindwa kuifikisha mipira ya krosi sehemu sahihi

Limekuwa ni jambo la kawaida kuwaona walinzi wa pembeni wakiwa wamefanya kazi nzuri ya kushambulia vizuri kwa kutumia mapana ya uwanja, lakini namna ya kuifikisha krosi eneo sahihi limekuwa ni tatizo kubwa.

Ni vyema wachezaji hawa wakasaidiwa kuelezwa anapopiga krosi kutoka eneo tofauti na krosi ifike eneo gani kwa manufaa ya timu.

Wajibu wa makocha

Kwa kutambua ukweli wa majukumu ya kucheza nafasi hizi, ni dhahiri kwamba kuwa mlinzi wa pembeni kunahitaji mchezaji kupata utimamu zaidi wa mwili.