UCHAMBUZI: Elimu ya kilimo na ufundi iwe lazima sekondari

Hivi karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alidokeza kwamba Serikali imejipanga kuziimarisha shule zote zilizokuwa za mchepuo wa kilimo na ufundi ili zianze kutekeleza malengo yake kwa faida ya Taifa.

Alitoa kauli hiyo akiwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), alipohudhuria siku ya kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Edward Sokoine aliyefariki kwa ajali ya gari miaka 35 iliyopita.

Alisema tayari Sh7 bilioni zimetumika kukarabati na kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuzifufua shule husika, huku akiitaka ofisi ya kamishna wa elimu kuhakikisha mpango wa kuanza masomo hayo unatekelezwa kuanzia Januari mwakani.

Profesa Ndalichako hakuzitaja shule husika, lakini baadhi ya shule zilizojulikana tangu miaka ya 1970 hadi 2000 kuwa ni za michepuo ya ufundi na kilimo ni pamoja na Ifunda, Tanga, Moshi, Mtwara na Iyunga.

Nyingine ni Musoma (Mara), Kibiti na Ruvu ( Pwani), Ifakara ( Morogoro) na Sekondari ya Malangali (Iringa) iliyokuwa na bustani za matunda, mbogamboga na mashamba makubwa ya mahindi.

Katika shule za ufundi, wanafunzi walijifunza masomo mbalimbali yakiwamo yaliyohusu ufundi wa umeme, umakenika, uashi na upakaji rangi, wakati kwa shule za kilimo walijifunza kilimo cha mazao mbalimbali kwa njia ya kisasa, kilimo cha bustani, ufugaji wa kisasa na hata jinsi ya kuboresha mimea na mifugo.

Shule hizo zilitengewa vifaa vingi vya kufundishia masuala ya ufundi na kilimo yakiwamo majengo huku zikiwa na walimu maalumu waliobobea katika fani hizo.

Wapo wahitimu wengi wa shule hizo ambao baadaye walijiunga na vyuo vikuu mbalimbali kwa kuendeleza vipaji vyao vya uhandisi katika ujenzi, umeme, teknolojia ya mawasiliano huku wengine wakimalizia masomo ya juu huko Sua.

Hata hivyo, kutokana na changamoto za nchi nzima kiuchumi, malengo ya shule hizo yalianza kufifia na kupoteza mwelekeo kwa kukosa vifaa na hata walimu.

Hivyo mkakati wa Serikali ya awamu ya tano kuanza kuziboresha zaidi shule zote za michepuo ya kilimo na ufundi, unastahili kupongezwa.

Pamoja na kupongeza, nadhani wakati umefika kwa Serikali kubadili mitalaa ya elimu kuanzia shule za msingi hadi sekondari, ili kwenda sambamba na mipango ya kuibadili Tanzania kuwa nchi ya viwanda na teknolojia.

Bila shaka mikakati ya Rais John Magufuli ni kuifanya nchi kuwa ya viwanda, hivyo ipo haja ya kuangalia upya mfumo wa elimu ya sasa ili iwe ya kuliandaa taifa lijalo kwa mambo ya viwanda na teknolojia.

Ni wakati mwafaka wa kuhakikisha vijana wa sasa wanajikita zaidi katika masomo ya kilimo, ufundi, sayansi na teknolojia ya viwanda ambayo yanawawezesha vijana kujiamini na kujiajiri baada ya kumaliza masomo.

Kwa mfano, mfumo mpya wa elimu unaweza kuwa na shule nyingi za michepuo ya kilimo cha mazao, shule za ufugaji, ufundi wa mambo ya samani, shule za ujenzi wa nyumba, ufundi magari, ufundi mawasiliano, na pia ziwepo shule za michezo ya aina mbalimbali kuanzia za msingi hadi kidato cha nne.

Mpango huo pia uziandae shule nyingi zaidi za kidato cha tano hadi cha sita kwa ajili ya masomo ya aina hiyo kwa wanafunzi wanaobahatika kusonga mbele.

Kwa vyovyote vile mpango huo utasababisha pia kuwapo kwa umuhimu wa kuongeza vyuo vikuu vingi vya kilimo, ufundi na teknolojia ambavyo vitapata wanafunzi sahihi kwa masomo sahihi ambao wataweza kuanzisha miradi ya maendeleo kwa taifa.

Kwa kuwa Serikali imeanza kuzifufua shule za kilimo na ufundi nchini, naamini inaweza pia kuimarisha zaidi mpango huo kwa kubadili mitalaa na kuzitenga shule nyingi zaidi kwa ajili ya masomo hayo.

Pia, Serikali inaweza sasa kuanzisha shule maalum za kuwasaidia watoto wenye vipaji mbalimbali vikiwamo vya sanaa za uchoraji, uimbaji, uchongaji na hata maigizo.

Ni kipindi hiki cha kuachana na masomo yanayolenga kuendelea kuitukuza historia ya kikoloni ambayo inawafanya vijana wengi washindwe maisha baada ya kumaliza masomo.

Lauden Mwambona ni mdau wa maendeleo anayeishi mkoani Mbeya: 0767 338897