UCHAMBUZI: Elimu yetu itazalisha ‘wafaulu mitihani’ wasiofaa kwa jamii mpaka lini?

Tuesday January 21 2020Moustapha Puya

Moustapha Puya 

By Moustapha Puya

Taifa halihitaji wafaulu mitihani tu, linahitaji vijana wenye utu, wenye kuipenda nchi yao na wenye ujuzi. Kuipenda nchi, utu na ujuzi havitokani na kufaulu mitihani, havitokani na kuwapa presha na kuwalazimisha watoto kukariri muda wote ili wafaulu mitihani.

Vinatokana na kuwapa maarifa na ujuzi, kuwapenda, kuwajali, kuwasikiliza, kuwapa muda wa kutosha kucheza na kushirikiana na wenzao.

Pia, kuwajengea uwezo wa kung’amua mema na mabaya, kuwaruhusu kujifunza mengine yafanyikayo nje ya darasa. Ni vijana tunaotarajia wawe na mawazo na maono ya kuzikabili changamoto zilizopo katika jamii yetu.

Nchini kwetu hali imekuwa tofauti; mfumo wetu wa elimu ambao ulitegemewa kuzalisha vijana makini wenye kufahamu wajibu wao kwa taifa umegeuka na kuwa chombo cha kuzalisha ‘wafaulu mtihani’ wasio na manufaa kwa Taifa.

Ushabiki wa kufaulu na kupata cheti kizuri umesababisha misingi ya elimu ya kuzalisha watu wenye ujuzi na maarifa kusahauliwa, badala yake njia za mkato za kuzalisha wafaulu mitihani zimebuniwa.

Njia za mkato za kufaulisha mitihani nyingi zinanajisi taaluma ya elimu na nyingine zinabagua, kuwanyanyasa na kuwaangamiza wanafunzi kabisa.

Advertisement

Kwa mfano, kutokana na ushabiki wa kufaulu ili kupata wateja, shule binafsi zinapitisha mchujo mkali kuwapata wanafunzi wenye uwezo mkubwa wa masomo na kuwaacha wale wenye uwezo mdogo kimasomo.

Katika shule binafsi pia kuna makundi ya shule za watu wenye uwezo mkubwa kiuchumi, uwezo wa kati na za wanaojiweza kiasi.

Serikali nayo ina kundi lake la shule za vipaji maalum, shule kongwe na shule za kata. Makundi yote haya ya shule yanapokea wanafunzi wenye uwezo tofauti kimasomo.

Hii maana yake tayari mfumo wetu wa elimu unabagua watoto wetu kiuwezo wa masomo. Badala ya shule zetu kuwa na utaratibu wa darasa la kawaida (ordinary classroom) ambalo litakuwa na uwakilishi wa watoto wenye uwezo tofauti, madarasa yetu yanakuwa na utaratibu wa madarasa ya wenye mahitaji maalum (special needs). Wenye uwezo mkubwa peke yao, wenye uwezo wa wastani peke yao na wenye uwezo mdogo peke yao.

Weledi wa elimu unasemaje? Weledi wa elimu unataka kwa kiasi kikubwa wanafunzi washiriki katika madarasa ya kawaida, madarasa yenye uwakilishi wa watu wote waliopo duniani, isipokuwa wale tu wenye mahitaji ya kipekee ambayo mahitaji yao hawawezi kuyapata katika mfumo wa umoja.

Darasa kama sehemu ya elimu imsaidie mwanafunzi kupata maarifa ya kuishi na watu wenye ulemavu, watu wenye uelewa mdogo, watu wenye uelewa mkubwa na mahitaji mengine tofauti.

Mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa kimasomo aliyeishi na wenzake wenye uwezo mkubwa, atawezaje kuwaelewa watu wenye uwezo mdogo ikitokea mwanafunzi huyo akawa kiongozi?

Ushabiki huu wa kufaulu mitihani unaotuonyesha dhahiri ujengwaji wa kasi wa matabaka ya mafukara na wenye nacho; tena ukifanywa na taasisi zinazosimamia udhibiti wa ubora na tathmini ya elimu nchini.

Pamoja na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), kufahamu ubaguzi wa usaili na uchujaji wa wanafunzi kwa misingi ya uwezo wa kimasomo na uwezo wa kiuchumi, bado inawapambanisha ulingoni mabondia wenye uzito tofauti.

Shule yenye wanafunzi wanaosomea mpaka tabiti inashindanishwa na shule ya kata ambayo haina walimu, haina mabweni, haina umeme.

Tunajidanganya. Tunatarajia nini? Utaratibu wa shule bora na wanafunzi bora kigezo kikiwa mitihani umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu sasa. Taifa limekuwa likizalisha wafaulu mitihani wengi na wamekuwa wakiitwa wanafunzi bora

Hivi kama Taifa tunajua walipo wanafunzi hawa bora tangu utaratibu wa kuwatambua uanze? Tumewahi kujiuliza kufaulu kwao kumeliletea tija gani Taifa? Je, tunapowapongeza wafaulu mitihani, ni kwa namna gani wanarudisha heshima tuliyowapa kwa Taifa?

Tusikubali kuendelea kuzalisha wafaulu mitihani kama hatujui tuliokwisha wazalisha wana tija gani. Tusiendelee kushabikia shule bora wakati tunafahamu fika tunashindanisha shule dhaifu dhidi ya shule bora halafu eti tunatoa matokeo ya kuwa tumepata shule bora. Tunajidanganya!

Pia, tusiendelee kuunga mkono unajisi wa elimu kwa mtoto wa darasa la nne kusoma kwa saa 12 siku saba za wiki kwa ajili ya kufaulu mitihani ya kitaifa

Muda uliowekwa kwenye mitalaa unatosha na anapaswa mtoto kutahiniwa uwezo wake kwa muda ulioainishwa. Tusikubali watoto wa darasa la saba kusoma darasani kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa tatu usiku.

Tukiwekeza nguvu katika kuwaaminisha watoto wetu na vijana wetu kuwa maisha ni kufaulu mitihani ya darasani, watafaulu lakini elimu hiyo isiwe na msaada kwao.

Moustapha Puya ni mdau wa elimu