UCHAMBUZI: Hakuna namna ligi za vijana ni muhimu kuanzishwa na kupewa kipaumbele

Monday May 13 2019

 

Hivi karibuni Serikali ya Uganda na Shirikisho la Soka Uganda (Fufa) walizindua programu maalumu ya mashindano ya mpira wa miguu kwa shule za msingi nchini humo ijulikanayo ‘Odilo’.

Mashindano hayo yatafanyika katika nchi nzima ya Uganda yakishirikisha wanafunzi wanaosoma shule hizo ambao wengi wana umri chini ya miaka 15.

Lengo la mashindano hayo ni kusaka vipaji vya soka vyenye umri mdogo kutoka shule za msingi nchini Uganda ambao wataandaliwa vyema ili baadaye waje kuzitumikia timu za Taifa kuanzia ile ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, 19, 20, 23 na ile ya wakubwa ya Uganda.

Kuanzishwa mashindano hayo ni muendelezo wa juhudi za Fufa za kuendeleza soka la vijana ambalo ndilo limekuwa moyo wa maendeleo ya mchezo huo katika nchi zote zilizopiga hatua.

Kabla ya kuanzishwa programu ya mashindano hayo, kumekuwa na idadi kubwa ya michuano ya soka ambayo imekuwa ikihusisha vijana wenye umri mdogo nchini Uganda kwa muda mrefu sasa.

Kuna mashindano ya soka kwa vijana wa shule za sekondari, vyuo na taasisi za elimu, Copa Coca Cola na Airtel Rising Stars ambayo huhusisha vijana wenye umri chini ya miaka 15 na 17, pia kuna ligi ya vikosi vya vijana vya timu zinazoshiriki Ligi Kuu.

Kupitia mashindano hayo, ni wazi Uganda imevuna na inaendelea kuibua vipaji vya soka vya wachezaji mbalimbali ambao wamegeuka nguzo ya timu za Taifa za nchi hiyo kufanya vyema kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa ambayo yanashiriki.

Kuna kundi la nyota wa Uganda ambao ni zao la mashindano hayo akina Emmanuel Okwi, Farouk Miya, Allan Okello, Ssekisambu Erisa, Khalid Aucho, Murshid Juuko, Hamisi Kiiza, Moses Waisswa na wengineo.

Wengi wao waliibuka na kung’ara wakitokea shuleni jambo ambalo lina faida kubwa kwao kwani mbali na kucheza soka, wana faida nyingine ya kuwa na elimu ambayo inawapa msaada mkubwa katika maisha ya kisoka.

Moja ya faida ya mchezaji wa aina hiyo ni kuwa na fikra na mtazamo mpana kuhusu mchezo wa soka anaweza kuishi katika mazingira yoyote na hilo linajidhihirisha kwa jinsi ambavyo wachezaji wa Uganda wamekuwa wakiondoka nchini mwao kila kukicha kwenda nje kucheza soka la kulipwa.

Jambo hili linalofanywa na Uganda linapaswa kuigwa na kutekelezwa hapa nchini kwa faida na maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu ambao bado haufanyi vizuri kulinganisha na nchi nyingine.

Kama nchi ni vyema sasa tukaanza kutilia mkazo soka la vijana kwa vitendo kupitia programu mbalimbali ambazo tutazifanyia uwekezaji mkubwa kama ambavyo Uganda wanafanya ili tuweze kupata idadi kubwa ya wachezaji bora vijana ambao watakuwa na faida kwa nchi siku za usoni.

Kwa sasa tuna upungufu wa mashindano ya soka kwa vijana jambo linalochangia tukose idadi kubwa ya wachezaji waliopevuka mapema ambao wanaweza kudumu na kuwa na mchango kwa Taifa ndani ya kipindi kirefu kulinganisha na wenzetu.

Kuna sababu ya kuimarisha mashindano ya vijana kama vile yale yanayohusu timu ndogo za klabu za Ligi Kuu zenye vijana wenye umri chini ya miaka 20 lakini pia yale ya Shule za Sekondari (Umisseta) na Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta).

Serikali inapaswa kuwekeza kwenye michezo kama moja ya sekta ambayo inatoa ajira za kutosha kwa watu kwa kushirikiana na TFF katika kuhakikisha kunakuwa na mtaala bora na walimu wazuri wa soka ambao watasaidia kuzalisha wachezaji wenye viwango vya juu shuleni, taasisi za elimu na vyuo.

Pia kuandaliwe utaratibu maalumu wa kuwafanya wazazi kuwa chachu ya maendeleo ya soka kwa watoto wao kwa kuwapa elimu ya kuwajengea msingi bora ili kuwa na maendeleo mazuri ya elimu na soka.

TFF inapaswa kutumia nguvu kubwa kushawishi kampuni na taasisi kuweka nguvu katika maendeleo ya soka la vijana kwa kuanzisha mashindano ambayo yatashirikisha timu na vituo vya soka kwa vijana wenye umri mdogo.

Mashindano kama Copa Coca Cola na Airtel Rising Stars yalikuwa chachu kubwa ya kuibua vipaji vya soka ambavyo baadhi leo hii vimekuwa tegemeo kwa timu ya Taifa Stars na klabu mbalimbali.