Halmashauri hazitimizi wajibu kudhibiti uhalifu

Friday October 5 2018

 

By Anthony Mayunga

Matukio ya uhalifu yanayoendelea katika maeneo mengi ya nchini, yanachangiwa na udhaifu wa mamlaka zilizopo hasa Serikali za Mitaa

Sheria ya Serikali za Mitaa namba 7 ya mwaka 1982, imebainisha kazi za lazima na za hiari kutekelezwa na kila halmashauri ya wilaya.

Kazi za lazima ni pamoja na kulinda amani, utulivu na utawala bora katika eneo lote la wilaya, kuleta na kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kutokomeza uhalifu, kulinda amani, utulivu, kulinda mali za umma na za watu binafsi.

Hata hivyo, tunashuhudia matukio mengi ya watu kuuawa, kuporwa mali na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia. Haya yanatokea huku Serikali za mitaa zikiwa watazamaji na kulalamikia Jeshi la Polisi.

Kwanza hata kwenye bajeti, halmashauri nyingi hazitengi fedha zinazohusiana na masuala ya ulinzi na usalama ili kutimiza wajibu huu wa kisheria kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Ukifuatilia taarifa nyingi za kamati za maendeleo za kata, utagundua zinazungumzia miradi ya maendeleo pekee.

Masuala ya uhalifu huja kwa sura ya lawama kwa Polisi ama uongozi wa wilaya kushindwa kudhibiti matukio. Kwao kwao kazi za hiari ndizo zinazopewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982, kuna vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria ndogo katika wilaya; navyo ni halmashauri ya wilaya na vijiji.

Vijiji na halmashauri nyingi zina sheria hizo ambazo zinaharamisha mambo mengi, kwa lengo la kuleta ustawi wa jamii.

Hata hivyo, watendaji wa vijiji, mitaa, kata na hata ngazi ya wilaya, hawasimamii utekelezaji wake hivyo uhalifu kuzidi kushamiri.

Kwa mfano, ipo sheria ya kupiga marufuku watu kutembea na silaha za jadi kama mapanga, sime, visu na nyinginezo, lakini hatuoni viongozi wa serikali za mitaa wakishughulika kuwadhibiti watu ambao wanakiuka maagizo hayo.

Matukio ya uhalifu ni mengi mikoa yote, lakini kwa mkoa wa Mara yamefurutu ada. Matukio haya ni kama mauaji ya mara kwa mara, wizi wa mifugo, watu kujichukulia sheria mkononi, wazazi kutopeleka watoto shule, ukeketaji na ukatili mwingine wa kijinsia.

Aidha, kuna watu wanaowahifadhi wahalifu kama wahamiaji haramu, majangili, lakini viongozi wa vitongoji na vijiji hawashughuliki kuwakamata wala kutoa taarifa kwa ngazi nyingine.

Laiti kungekuwa na kuwajibishana kuhusu kushindwa kusimamia kazi za lazima za serikali za mitaa, matukio mengi yasingekuwepo hadi sasa kwa kuwa kila kiongozi angekuwa mstari wa mbele kuibua na kudhibiti uhalifu eneo lake.

Hata yale mabaraza ya kisheria ya kata ambayo ni chombo kilichoko karibu zaidi na wananchi kwa kutatua migogoro na matatizo, hayafanyi kazi.

Licha ya mabaraza hayo kuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za jinai zilizoorodheshwa katika sheria nyingine za nchi na zilizowekwa kwenye sheria ya baraza la kata, katika baadhi ya maeneo hayajaundwa.

Kwa kutotambua wajibu wao, halmashauri zimeshindwa hata kuwaandaa wananchi kuwa walinzi wa kuhakikisha sheria hazivunjwi, ikiwamo pia kuwadhibiti wanaokwenda kinyume na sheria ndogondogo.

Kama tunaweza kufanya chaguzi za marudio kila wakati, naamini inawezekana viongozi wa ngazi zote wa serikali za mitaa kupata semina, ili wajue wajibu na mipaka yao kiutendaji.

Tukijipanga inawezekana kabisa kuzuia uhalifu, kwani kuna matukio mengine yanaweza kuepukika.

0787239480.