UCHAMBUZI: Hamasa ya vijana itawabeba wenzao katika Afcon 2019

Leo pazia la mashindano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Afcon U17 2019) linafunguliwa rasmi ambapo mechi zake zitachezwa kwenye viwanja vya Taifa na Chamazi nchini Tanzania.

Haya ni mashindano makubwa zaidi ya soka kuwahi kuandaliwa nchini ambayo yatakusanya wageni wengi kwa wakati mmoja kutoka nchi shiriki, waandishi wa habari, maskauti, mawakala wa soka na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF).

Jumla ya mataifa nane yatashiriki fainali hizo, mbali na wenyeji Tanzania “Serengeti Boys’, timu nyingine ni Morocco, Senegal, Guinea, Cameroon, Nigeria, Uganda na Angola.

Timu nne zitakazotinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo yatakayofanyika kwa wiki mbili kuanzia Aprili 14 hadi 28, zitafuzu fainali za Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Brazil baadaye mwaka huu.

Bila shaka ni matumaini ya Watanzania wengi kuwa timu mwenyeji Serengeti Boys ni miongoni mwa timu hizo nne zitakazoiwakilisha Afrika huko Brazil.

Kiuhalisia Serengeti Boys wakiwa kama wenyeji, hawana sababu ya msingi ya kushindwa kumaliza ndani ya kundi la timu nne.

Serengeti Boys ina kila sababu ya kwenda Brazil kwa sababu kwanza mechi zinachezwa viwanja vya nyumbani, kwa ujumla mtanange wote utakuwa kwenye eneo lao la kujidai, wanalolifahamu vyema.

Vijana wa leo wana msemo “Kila mmoja ashinde kwao”, kwa nini vijana hawa wasishinde kwao pia. Bila shaka watashinda.

Jambo la kujivunia Serengeti Boys ni kuwa gozi la michuano hii linapigwa kwao na kila litakapoangukia ni kwao.

Mbali na timu inayowakilisha nchi kupata faida ya kusukuma kabumbu kwenye viwanja vya nyumbani, wananchi pia watapata faida ya kupokea wageni.

Wageni hao ni pamoja na maafisa wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), waandishi wa habari na viongozi toka mataifa tofauti tofauti.

Wageni hao watakuwa faida kwa nchi katika nyanja mbalimbali ikiwamo za kikodi, biashara na uchumi wa nchi iwapo kila mmoja ataiangalia kama fursa utasisimka kwa muda wa wiki mbili watakazokuwa hapa nchini.

Hii niliyoanza nayo ilikuwa bashraf tu, lengo hasa la andiko hili ni namna ambavyo wananchi wataichukulia michuano hiyo na hamasa watakayowapa vijana.

Kila mmoja ana moyo na hamu ya kushinda hatua za awali za michuano hiyo kisha kwenda Brazil kuchukua kombe, swali ni je, hamasa iliyopo leo ambapo michuano hiyo imeanza kutimua vumbi inaonyesha dalili za kushinda?

Hata kama vijana wamejiandaa kiasi gani kama hakutakuwa na hamasa ya uwapo wa michuano hiyo kila kona ya nchi, hali hiyo itashusha hamasa yao.

Kumekuwa na tabia ya kuchagua mechi za kuhamasisha ikiwamo za fainali, katika michuano hii tafadhali uhamasishaji uanze mechi ya kwanza hadi ya mwisho.

Ushangiliaji wa kusubiri wachezaji wafanye jambo ikiwamo chenga, kufunga goli umepitwa na wakati, badala yake hata kama timu imefungwa ushangiliaji uendelee mwanzo mwisho kuwapa vijana hamasa ya kuhakikisha wanafanikiwa kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil.

Vijana wawe chachu ya kuhakikisha vijana wenzao wanapenya kwa kujitokeza viwanjani na kushangilia bila kuchoka kama ambavyo inaonekana kwenye mechi mbalimbali duniani.

Lakini angalizo pamoja na ushangiliaji ni vema kujiweka kando na vurugu iwe kwa wageni au wenyeji wenyewe kwa wenyewe wawapo uwanjani kwa sababu zitaondoa sifa ya nchi na zinaweza kusababisha kufungiwa kushiriki soka.

Inawezekana kufanya vizuri, kushangilia kwa ustaarabu na kuzitumia ipasavyo fursa zitakazopatikana kwenye kipindi cha wiki mbili za michuano hiyo kutaongeza hamasa ya nchi kuomba kuandaa michuano mingine mikubwa..

Vijana ambao wengi mpo kwenye mitandao ya kijamii, itumieni kuhamasisha uwapo wa michuano hii hapa nchini.

Mijadala hiyo ndiyo itazaa hamasa ya watu kujumuika viwanjani mkiwemo na kufanikisha kupata manufaa kwa timu lakini ya kiuchumi pia kwa sababu wenye biashara watauza bidhaa zao endapo tu kutakuwa na wingi wa watu viwanjani ukiachilia mbali wageni.

Watu hawawezi kumiminika viwanjani iwapo hakutakuwa na mijadala ya kutosha inayoashiria kuwa Afcon 2019 inachezwa Tanzania. Mavazi, picha mitandaoni, mijadala kwenye vijiwe vya kahawa inastahili kwa asilimia 100 kutawala kinachoendelea kwenye michuano hii.

Vijana wa Serengeti Boys kazi yao iwe moja tu kucheza soka la kideoni, vijana wa nje ya uwanja kazi yao iwe uhamasishaji kuhakikisha soka linachezwa, linatizamwa na linashangiliwa.

Tukutane kwa Mkapa na kwa Bakhresa kule Azam Complex Chamazi.