KING'AMUZI CHA AFYA: Harufu mbaya ya miguu kwa wanamichezo

Monday May 13 2019Dk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Tatizo la harufu mbaya ya miguuni ni tatizo linaloweza kumpata mtu yoyote ikiwamo wanamichezo, kitabibu hujulikana kama Bromodosis. Ni tatizo linalomfanya muathirika na wanaomzunguka wasijisikie vizuri.

Chanzo kikubwa ni jasho linalotoka kwa wingi miguuni, tatizo huwa pana zaidi kama mhusika atakuwa ana ugua fangasi za miguuni. Wanamichezo ni kundi mojawapo la waathirika wa tatizo hili kwasababu ya kutokwa jasho jingi miguuni wakati wa kucheza.

Jasho linalotoka miguuni huwa lina kazi yakufanya eneo hilo kuwa na unyevunyevu na hivyo kuzuia msuguano, vile vile lina kazi ya kudhibiti joto la eneo hilo wakati wa joto au wakati wa mazoezi.

Eneo la miguuni chini ya ungio la kifundo cha mguu huwa kuna tezi jasho nyingi kuliko eneo lolote mwilini. Tofauti na tezi zingine, tezi jasho za miguuni huwa na kawaida ya kutoa jasho wakati wote na si lazima iwe ni wakati wa joto au mazoezi.

Harufu ya miguu hutokana na uwepo wa bakteria juu ya ngozi ambao hulivunja vunja jasho linalotoka katika vitundu vya ngozi. Kitendo hiki huambatana na utokaji wa harufu kama ya jibini.

Hali ya kutoa jasho na harufu mbaya husababishwa zaidi na mambo yafuatayo.

Kutumia vitu jozi moja mara kwa mara au kutobadili viatu vya kuchezea, hii husababisha na kunyonywa kwa jasho la miguuni katika viatu na kabla ya kukauka tena huvaliwa tena.

Mchezaji mwenyewe kutokuwa msafi na kutofuata kanuni za usafi wa mwili.

Mabadiliko ya vichochezi (hormons) yanaweza kumfanya mtu kutokwa jasho mwilini ikiwamo la miguuni kupita kiasi, hii inawagusa zaidi wanamichezo vijana.

Kuwa na tatizo la kiafya lijulikanalo kama hyperhidrosis, ambalo husababisha mtu kutokwa jasho isivyo kawaida na kuwa na ugonjwa wa fangasi za ngozi ya miguuni

Namna ya kuepukana na tatizo hili ni pamoja na kuhakikisha kuwa unakuwa msafi kimwili na kufuata kanuni za afya, hakikisha unabadili viatu mara kwa mara (usivae zaidi ya siku 2) na kila unapobadili vifanyie usafi.

Hakikisha unaosha miguu yako kwa maji safi na sabuni na ukaushe kwa kitambaa safi hasa katika maeneo kati ya kidole na kidole.

Badili soksi mara kwa mara, ni vizuri ukatumia soksi zilizotengenezwa kwa pamba kwa sababu zinanyonya jasho kirahisi ukilinganisha na soksi za nailoni.

Njia nyingine ni pamoja na kutumia poda au manukato maalum ya kupulizia ambazo hukata harufu mbaya miguuni.

Kutokana na dunia ya michezo kupiga hatua zipo soksi maalum ambazo huwa na kemikali inayowaangamiza bakteria wa ngozi wanaosababisha tatizo hili.

Inashauriwa kuvaa viatu vya michezo vya ngozi au vya raba iliyotengenezwa kwa turubai.

Vilevile zipo soksi na viatu vilivyo na matundu ambavyo husaidia kukauka jasho la miguuni kirahisi. Tumia viatu vyenye vikanyagio vya soli ya miguuni ambavyo unaweza kubadili kama kitaloa jasho na kuweka kingine kikavu.

Kwa wale wenye fangasi za miguuni vizuri watibiwe katika huduma za afya, pia zipo dawa za kupaka zinazosaidia kuondoa tatizo hili. Kama tatizo litakuwa kubwa tafuta huduma za afya kwa ushauri na matibu.