KONA YA MAKENGEZA : Uamuzi wa Bunge bangua bongo

Sunday May 8 2016

 

By Richard Mabala

Mheshimiwa Makengeza,

Unajua watu wengine ni wehu. Hebu nipe sababu moja kwa nini mijadala ya Bunge irushwe laivu na mimi nitakupatia sababu kumi kwa nini isirushwe kabisa.

Tena nakuambia kama mwananchi wa kawaida kabisa. Mungu aniepushe na misokoto ya mijadala yao. Tena siku hizi wenye uamuzi siyo wao hivyo nina haja gani kuwasikiliza huku wakipashana kama vile wako vijiweni badala ya masponjini. Hebu nikupashe kanuni kuu za ulinzi na usalama wa taifa.

Linda wajinga

Katika nchi inayoheshimu haki sawa, hatuna budi kuwalinda wadhaifu ndani ya jamii. Naam. Iwapo sifa pekee ya kuwa mbunge ni kuweza kujua kusoma na kuandika tu, wakati hata kuwa dereva, lazima uwe na cheti cha Kidato cha nne, kwa nini viti vya sponji visiwe kimbilio la wakosefu?

Mheshimiwa hajaomba kuwa waziri. Hajaomba kupewa kazi inayohitaji akili. Ameomba kuwa mbunge tu ili mkono uende kinywani na mapochopocho kochokocho.

Advertisement

Mtu akishakuwa mbunge, hana budi kusema bungeni maana ndiyo hadidu rojorojo ya mheshimiwa. Sasa iwapo kauli inateleka mbele ya kadamnasi ya nchi nzima, tunamtendea haki kweli. Siyo kosa lake, hajasoma, kwa nini aumbuliwe?

Kwani tunaonyesha makosa ya profesa darasani? profesa mzima anatoa maneno ya ajabuajabu lakini anasitiriwa na chuo chake hivyo wanaojua upumbavu wake ni wale wanafunzi wake. Kama profesa analindwa kwa nini mheshimiwa ambaye anajua kusoma na kuandika tu asilindwe?

Ndiyo maana, kwa kuwa Tanzania ni nchi ya watu wanaomcha Mwenyezi Mungu ni dhahiri kwamba tunapaswa kulinda hadhi ya hawa waheshimiwa waliosota kutafuta kazi inayoendana na sifa zao.

Linda lugha ya Taifa

Kwa kuwa tunapenda lugha yetu ya Taifa na hatupendi itiwe doa, hatuna budi kutambua kwamba wako wengine ambao hawajui lugha yetu ya Taifa vizuri. Hata ya kigeni ni shida. Kwa mfano, mtu anapotumia neno ‘beibii’ anajua maana yake?

Siyo kosa lake kama alikuwa anasinzia wakati mwalimu anafundishia darasani. Au kwa kuwa amezoea kukaa vijiweni na lugha ya vijiweni ni vibaya kabisa wananchi wengine waambukizwe Kiswahili kibovu.

Kwa hiyo, ili kuwalinda wananchi wetu dhidi ya matumizi mabaya ya lugha yanayoweza kuwapotosha au kuwafadhaisha, matumizi haya yabaki siri. Papohapo na laani kabisa wale ambao wanatoka nje ili waweze kuhojiwa na kusambaza maneno mabaya yaliyosemwa kwenye faragha ya usponjini.

Linda imani, amani ya wapiga kura

Juzi walimiminika kumchagua huyu au yule. Sidhani kama wengi wao walimwangalia sana mgombea wao wa ngazi ya sponji. Waliangalia rangi ya nguo yake bila kujali yaliyomo ndani ya rangi ile bila kusahau wale walioangalia rangi ya manoti au fulana au waliotomatiki.

Kama huniamini, wangapi walienda kwenye mikutano ya kampeni ya waheshimiwa watarajiwa wa jimbo lao? Sasa wakija kutambua kwamba yule mwenye rangi pendwa anafanya mambo pondwa, hii inaweza kuwakatisha tamaa. Watashindwa kufanya kazi. Watashindwa kutunza familia yake. Watashindwa kujenga nchi.

Ndiyo. Nilipokuwa mdogo mimi, tuliwaamini sana viongozi wetu. Tuliwaheshimu siyo kwa sababu walikuwa waheshimiwa, tena hili neno lilikataliwa kabisa. Tuliwaheshimu kutokana na maneno na vitendo vyao vya heshima. Ndiyo maana tulijitolea kufa na kupona kujenga Taifa.

Tulilima kwa nguvu hata tukiwa wanafunzi. Tulienda kuwafundisha baba zetu na mama zetu na dada zetu na kaka zetu kusoma na kuandika … bila kudai hata senti tano, kwa sababu tuliamini viongozi wetu. Tuliamini kabisa tulikuwa katika safari moja.

Siyo tusote sisi wengine watambe na suti. Sasa hebu fikiria, wakiona maneno mengine ya kipuuzi yanayotolewa na mheshimiwa wao, watu watakuwa na mori kweli wa kujenga Taifa.

Linda masilahi

Huu ni msingi wa msahafu, walio nacho wataongezewa na narudia kusema kwamba, kwa bahati nzuri, nchi hii imejaa wacha Mungu ambao wanapenda kufuata misahafu moja kwa moja. Walio nacho, jumuiko la washindi, wana haki ya kulinda walicho nacho bila kusumbuliwa na jicho la wenye husuda upande wa pili. Hii ndiyo amri ya kwanza. Linda masilahi yako usilinde masilahi ya wengine.

Ndiyo maana mtu akiwa kwenye viti vya sponji, anaangalia kitu kimoja tu. Akiwa ni mwanamke na wanawake wa upande wa pili wanadhalilishwa na mwanaume upande wao, atawekaje mbele utu na heshima ya wanawake. Lazima aweke masilahi ya kundi lake mbele. Lazima atalinda wenzake wenye masilahi pamoja.

Vivyohivyo, akiwa ni mtu wa eneo fulani, potelea mbali kama mwenziye anatusiwa, walio nacho kwanza, mengine ni ndoto za alinacha.

Hata hivyo, siyo vizuri kuonekana maana unaweza kueleweka vibaya na wananchi wasiojua kanuni hizi au wenye husuda kwa nini hawa wamepata na wao wamekosa. Ndiyo maana tunaweza pazia ya kuwasititi watu katika kulinda maslahi yao.

Linda mfumo dume

Usishangae Makengeza. Nchi hii ina utamaduni wake. Utamaduni wake ni mfumo dume upende usipende. Mabeibii wanaobisha wanapoteza muda. Mimi mwenyewe nawatafuta mabeibii kila kona na wakinifurahisha lazima niwape zawadi. Kuna ubaya gani.

Nafanya hivyo kwa sababu ndivyo tulivyo wanaume. Beibii mbele. Sasa kama mtu anafanya hivyo katika maisha yake ana kosa gani kuona wanawake wote wako hivyo? Siyo mawazo yake jamani? Lakini mbele ya wananchi wenye uelewa finyu na hasa mabeibii wenyewe ambao ndiyo wapigakura walio wengi, unaweza kueleweka vibaya. Ndiyo maana tunatumia usiri kulinda utamaduni mtamu.

Usiniambie kwamba siyo kweli. Hii siyo hoja. Hoja ni kwamba lazima tulinde utamaduni wetu wa kuwaona hawa kama mabeibii maana tusipofanya hivyo, mwisho wa siku watu watakujua kugundua kwamba kumbe wana akili kuliko sisi. Mmmh kiama!

Linda soko huria na mtandao huria

Umeona mwenyewe Makengeza. Hatutaki matangazo ya jumla kwa sababu zilizopo hapo juu, lakini haya ya rejareja kuna ubaya gani? Hapa kila mheshimiwa anaweza kuamua kujionyesha laivu kwa wakati anaoutaka mwenyewe.

Siyo wakati ameshikwa na usingizi kutokana na kufakamia dhifa ya taifa au wakati kichwa kinagonga kutokana na mijadala mizito kwenye baa ya karibu. Ni wakati anaweza kujionyesha vizuri.