Kabla ya Bunge, Serikali iwe inatoa mrejesho

Muktasari:

Bunge hilo litafuatiwa na mkutano ujao ambao kwa kawaida hujadili na kuipitisha bajeti ya mwaka unaofuata.

Bunge la Jamhuri ya Muungano jana lilimaliza mkutano wake wa wiki mbili ambao ulijadili masuala kadhaa, yakiwemo ya kodi ambazo ni kero ambazo wabunge wamesema zinasababisha biashara nyingi kufungwa.

Bunge hilo litafuatiwa na mkutano ujao ambao kwa kawaida hujadili na kuipitisha bajeti ya mwaka unaofuata.

Katika mkutano ulioisha, wabunge wamejadili mlolongo wa masuala ya kitaifa, kuuliza maswali, kutoa maoni kuhusu utendaji na kufikia maazimio ambayo yatatakiwa yatekelezwe na Serikali.

Ni dhahiri kuwa kila mbunge aliyechangia alikuwa na nia njema ya kutaka nchi yetu ishike njia sahihi ya maendeleo itakayoleta ustawi wa jamii kwa Taifa zima na hivyo maoni hayo yanatakiwa yafanyiwe kazi na Serikali ili kufanikisha lengo hilo.

Ni matarajio yetu kuwa Serikali itazingatia maoni yote na kuyafanyia kazi yale ambayo yanaonekana yanafaa na pengine kuyaboresha yale ambayo yana kasoro, na bila shaka kuyaacha yale ambayo hayawezekani.

Lakini uzoefu unaonyesha kuwa kila wanaporudi bungeni, wabunge wamekuwa wakilalamika kuwa Serikali haifanyii kazi yale yanayoafikiwa na Bunge na matokeo yake huwa ni kama Bunge kupoteza muda kuzungumza yaleyale badala ya kusonga mbele, kitu ambacho ni sawa na kutumia kodi za wananchi kwa mambo ambayo hayawasaidii walio wengi.

Kuna wakati wabunge wamediriki kuwatuhumu mawaziri kuwa wana kiburi kutokana na kutopokea ushauri na maazimio ya Bunge na kuyafanyia kazi, kitu ambacho si kizuri kwa nchi yenye amani na utulivu ambao unaruhusu maoni na ushauri kutolewa kwa njia zilizowekewa utaratibu mzuri tofauti na nchi nyingine.

Ni muhimu kwa Serikali na viongozi wake kuona umuhimu huo wa maoni na maazimio ya wabunge katika kusaidia kuiendesha Serikali ili nchi ifikie kule ambako kila mtu angependa.

Hata pale inaposhindikana kutekeleza maazimio na mapendekezo ya Bunge, angalau Serikali ingekuwa ya kwanza kukieleza chombo hicho sababu ya baadhi ya maazimio kutotekelezwa badala ya kusubiri hadi ihojiwe ama ilaumiwe na kukosolewa wakati ya mijadala.

Yaani, kama Bunge lingekuwa na utaratibu wa kupata mrejesho wa utekelezaji wa maazimio ya Bunge kabla ya mkutano kuanza, ingekuwa jambo zuri kwa kuwa hiyo ingeweza kupunguza muda ambao wabunge huuliza mambo yaleyale kila kikao.

Kwa hali ilivyo hivi sasa, Waziri Mkuu ndiye anayetoa taarifa ya utekelezaji na masuala mengine mengi kila wakati Bunge linapokuwa linamaliza mkutano wake. Lakini ingekuwa vizuri zaidi kama chombo hicho kingekuwa na utaratibu wa kuiwezesha Serikali kutoa mrejesho wa utekelezaji wa maazimio na maamuzi ya mkutano ulioisha wa Bunge kabla ya mpya kuanza.

Huu ni utaratibu bora ambao hutumika kwenye vikao vingi kwa ajili ya kuongeza uwajibikaji kwa wanaopewa majukumu na kuepusha kujadili jambo moja kila wakati.

Hilo likifanyika, wabunge watajua kuwa maazimio yao yalifanyiwa kazi kwa kiwango gani na yale ambayo hayakufanyiwa kazi yalishindikana kwa sababu gani na hivyo kuendelea kuiamini Serikali yao na kuona umuhimu wa chombo hicho cha kutunga sheria katika kuisimamia Serikali na kuisaidia kuendesha nchi.

Mkutano ulioisha ulikuwa na mambo mengi yanayohusu kodi na taarifa kadhaa za kamati ziliishauri Serikali kuhusu kodi na ukusanyaji wake, zikitaka uwe bora ili kuziwezesha biashara kukua badala ya kufungwa.

Tunatarajia kuwa hayo yatazingatiwa katika mkutano ujao utakaojadili bajeti ya mwaka 2019/20, ambayo moja ya mambo yake makuu ni sheria ya fedha, hasa kodi.