UCHAMBUZI: Kocha Stars wachezaji wapo wengi si Simba, Yanga

Monday October 28 2019Abdallah  Mweri

Abdallah  Mweri 

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtangaza Etienne Ndayiragije kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’.

Kocha huyo ndiye atakayeiongoza Taifa Stars katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika Kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan) zitakazofanyika Cameroon, mwakani.

Mbali na fainali hizo, Ndayiragije anakabiliwa na mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia zilizopangwa kuchezwa Qatar mwaka 2022.

Taifa Stars imekata tiketi ya kucheza Chan baada ya kuitupa nje Sudan. Katika mechi ya kwanza Sudan ilishinda bao 1-0 kabla ya Stars kushinda mabao 2-1 ugenini na hivyo Stars kunufaika na bao la ugenini.

Hii ni mara ya pili Taifa Stars kucheza fainali hizo, awali ilishiriki mwaka 2009 nchini Ivory Coast baada ya kuing’oa Sudan kwa jumla ya mabao 5-2.

Ndayiragije raia wa Burundi ameingia katika rekodi nzuri katika soka la Tanzania kwa kuipeleka Taifa Stars kwenye mashindano hayo akitanguliwa na Mbrazili Marcio Maximo aliyefanya hivyo mwaka 2009.

Advertisement

Jina la Ndayiragije limechomoza katika orodha ya makocha 200 kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo ya Ulaya walioomba kazi ya kuifundisha Taifa Stars.

Mafanikio ya Ndayiragije tangu akiwa ngazi ya klabu akizinoa Mbao, KMC na Azam, yamempa nafasi ya kurithi mikoba ya Emmanuel Amunike ambaye mkataba wake ulisitishwa muda mfupi baada ya Stars kurejea kutoka Misri katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Caf).

Ni vyema kocha wa Stars akawezeshwa kuzunguka mikoa mbalimbali kuangalia mechi za Ligi Kuu ili awe na wigo mpana wa kuchagua wachezaji wa kikosi chake.

Imezoeleka idadi kubwa ya makocha wa Stars wamekuwa na tabia ya kukariri wachezaji wa Simba, Yanga na Azam jambo ambalo si sahihi kwa ustawi wa soka nchini.

Ligi Kuu inachezwa katika mikoa mingi nchini, hakuna sababu ya msingi inayosababisha Stars iundwe na idadi kubwa ya wachezaji wa Simba na Yanga.

Ni vyema kocha ajaye akaaandaliwa mazingira bora ya kufika mikoani ambako kuna idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu na Daraja la Kwanza wenye uwezo mzuri wa kuitumikia timu ya Taifa.

Kitendo cha Ditram Nchimbi kuipeleka Taifa Stars katika fainali za Chan kinathibitisha Tanzania ilivyosheheni idadi kubwa ya wachezaji wenye vipaji lakini hawaonwi.

Nchimbi aliitwa dakika za mwisho Taifa Stars ikiwa ni siku chache baada ya kuifunga Yanga mabao matatu katika mchezo wa Ligi Kuu akiitumikia Polisi Tanzania. Timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3 Oktoba 3, mwaka huu.

Inawezekana wadau wengi na hata pengine makocha wa Stars hawakuwa wakimfuatilia Nchimbi hadi pale alipofunga mabao matatu ndipo wakashituka.

Mshambuliaji huyo ni ingizo jipya lililoibeba Stars dhidi ya Sudan baada ya kufunga bao la pili akitanguliwa na Erasto Nyoni aliyefunga bao la kwanza.

Tanzania ina akina Nchimbi wengi ambao wamefichwa kwa kuwa tu hawachezi Simba, Yanga au Azam. Namungo ina Reliant Lusajo na Lucas Kikoti ambao ni washambuliaji hodari.

Lusajo alikuwa mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita akifuatiwa na Kikoti, lakini majina ya wachezaji hao hayazungumzwi.

Kagera Sugar wapo vijana wawili Awesu Awesu na Yusuf Mhilu ambao tangu kuanza msimu huu wamekuwa moto katika kufunga mabao.

Hao ni kwa uchache, lakini wapo wachezaji wengi mikoani wenye sifa za kuichezea Stars.

Ni vyema tukarudisha utamaduni wa miaka ya 1980 uliotoa fursa kwa kocha kuwa na wigo mpana wa kuchagua wachezaji kutoka maneo mbalimbali nchini.

Kitendo cha kocha kupanua wigo wa kuangalia wachezaji wengine wa mikoani kitatoa nafasi kwa wachezaji chipukizi kujiona ni sehemu ya timu ya Taifa kuliko hivi sasa ambapo idadi kubwa wanatoka klabu za Simba, Yanga au Azam za Dar es Salaam.

Itakumbukwa kuwa Stars ilikuwa na beki aliyecheza kwa muda mrefu kwa kiwango bora Leopald ‘Tasso’ Mukebezi ambaye alikuwa akiichezea klabu ya Balimi ya Kagera.

Stars pia iliwahi kuundwa na wachezaji nyota wa Coastal Union akina Said Kolongo, Douglaus Muhani, Joseph Lazaro, Juma Mgunda, Razack Yusuf ‘Careca’, Hussein Mwakuruzo na Ally Maumba.

TFF kupitia mkurugenzi wa ufundi Oscar Mirambo itengeneze mfumo bora ambao utampa fursa kocha wa timu hiyo kuchagua idadi kubwa ya wachezaji wenye sifa kutoka kila pembe ya Tanzania.