Kuwa makini na matumizi ya dawa

Miezi michache iliyopita nilimhudumia mgonjwa baada ya kupitia dalili kadhaa kama maumivu wakati wa kukojoa, maumivu wakati wa tendo la ndoa, maumivu ya kiuno na mgongo yaliyodumu kwa muda mrefu na kutokwa na damu ukeni kulikozidi ratiba ya mzunguko wa hedhi ya kawaida.

Ndipo wahudumu wake wa afya walimpa rufaa ya kuja hospitali ninayofanyia kazi kwa ajili ya vipimo zaidi baada ya kupatiwa matibabu tatizo lake likendelea kudumu, ndipo tulipomfanyia vipimo na kumgundua ana saratani ya mfuko wa uzazi.

Japo wakati tunamfanyia vipimo alikuwa amechelewa kidogo kwa kuwa tuliibaini saratani katika hatua ya pili lakini tulijitahidi kumuingiza kwenye mpango wa matibabu ambao ungeweza kumsaidia apate matibabu yake kikamilifu.

Mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 33, alitakiwa akamilishe mizunguko kadhaa ya ya mionzi, dawa pamoja na kufanyiwa upasuaji na kumuhimiza awe anakuja hospitali mara kwa mara kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya afya yake wakati akiendelea na matibabu.

Siku moja alipofika hospitali baada ya uchunguzi tukaona kuwa matibabu yamemsaidia kiasi tofauti na awali tulipompokea na hata yeye alikiri kuona mabadiliko.

Lakini tukiwa kwenye chumba cha vipimo tukiendelea na majadiliano kuhusu afya yake, aliniuliza, “Daktari ninaweza kutumia dawa zingine zaidi ya hizi?”

“Inategemea. Ni dawa za aina gani unazofikiria kuzitumia? Nikamuuliza kwa shauku kidogo.

“Naifikiria nijaribu kutumia dawa ya vitamini na mchanganyiko wa madawa mengine mbadala ambayo niliambiwa kuambia na mtu fulani,” akajibu huku akionesha hali ya kutojiamini.

“Kwa bahati mbaya utaratibu wa matibabu na hasa kwa tatizo lako hauruhusu utumie dawa zingine mbadala hata kwa kuchanganya. Na hasa ukizingatia ukweli kuwa usalama wa dawa hizo kiafya bado haujaonekana na hasa tukizingatia dawa hizo bado hazijafanyiwa vipimo na kuthibitishwa kitaalamu kwa matumizi,” nikamjibu. “Sawa daktari nimekuelewa!,” akanijibu.

Ni vibaya kuchanganya matibabu ya hospitali na ya tiba mbadala hasa kwa wagonjwa wa saratani. Nawakumbusha, ni vyema kuzifuatilia dalili za saratani kwa ukaribu na kupata vipimo kwa wakati.

Mwandishi wa makala haya ni daktari kutoka Hospitali ya TMJ SUPER SPECIALIZED POLYCLINIC.