MAONI: Serikali ifanyie kazi changamoto hizi

Leo imetimia miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli. Katika kipindi hicho kuna mafanikio mengi tumeyaona, lakini kukiwa pia na changamoto kadhaa.

Wakati wa kampeni na baada ya kuapishwa, Rais Magufuli alitambulika kwa jina la utani la ‘tingatinga’ kwamba ni kiongozi mchapa kazi na hasa baada ya kutumia kauli mbiu yake ya ‘hapa kazi tu.’

Miaka ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano ilianza kwa kudhihirisha ‘utingatinga’ na kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’ kwa kufuta baadhi ya sherehe za kitaifa ikiwamo tafrija ya kuwapongeza wabunge na fedha zake aliamuru zielekezwe kwenye maendeleo ya wananchi.

Fedha zilizohamishwa matumizi kuna zilizotumika kujenga barabara na zingine kununua vitanda kwa ajili ya wagonjwa waliokuwa wanalala sakafuni katika baadhi ya wodi za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Serikali ya Magufuli iliendelea kujijengea sifa kwa wananchi pale alipoanzisha kauli mbiu nyingine ya ‘utumbuaji majipu’ kwa kuwaondoa kwenye nafasi za uteuzi au uongozi watendaji walioshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Watumishi wengi wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi na watendaji wengine ndani ya Serikali na taasisi zake walipoteza nafasi zao kwa ama uteuzi wao kutenguliwa au kuhamishiwa sehemu zingine.

Imekuwa miaka minne ambayo tumeshuhudia maamuzi magumu yakifanyika ikiwemo utekelezaji wa baadhi ya maamuzi yaliyofikiwa miaka mingi iliyopita, mfano suala la Serikali kuhamia Dodoma ambako ndiko makao makuu ya nchi yaliko.

Ni kipindi ambacho tumeshuhudia wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki wakitolewa kazini jambo ambalo lilisaidia kuondoa ujanjaujanja katika ajira nchini.

Ni miaka minne ambayo tumeshuhudia huduma za afya zikiboreshwa na elimu bila malipo ikitekelezwa kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne.

Miradi mbalimbali inatekelezwa ikiwamo bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere la Rufiji, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam-Morogoro-Dodoma, ununuzi wa ndege za kisasa, ujenzi wa barabara maeneo mbalimbali na huduma za maji kuboreshwa na mambo mengineyo.

Hata hivyo, miaka minne imekuwa na changamoto zake kwa baadhi ya maeneo ikiwamo eneo la utungwaji wa sheria zinazominya uhuru wa habari na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Tunaamini yote yanayofanywa na Serikali yanafanyika kwa nia njema ya kujenga Taifa lenye umoja, mshikamano na lenye ushindani wa kimaendeleo katika anga za kimataifa.

Kwa kuwa Tanzania ilikubali mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kuna haja Serikali inayoongozwa na CCM kujenga utamaduni wa kuvumiliana, kwa vyama vya upinzani navyo viruhusiwe kufanya mikutano kama wanavyofanya viongozi wa CCM wanaozunguka nchi nzima kwa lengo la kuyafanya maeneo wanayozuru yawe ya kijani. Haya tunayoyasikia katika uchaguzi wa serikali za mitaa hayaleti picha nzuri.

Ni matumaini yetu wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikiadhimisha miaka minne ya kuwa madarakani huku tukiona maendeleo ya miradi mbalimbali, basi ijitathmini kwa kuyafanyiwa marejeo maeneo yanayolalamikiwa.