MAONI: Wabunge jiandaeni sasa kwa ajili ya haya

Jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango aliwasilisha kwa wabunge Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20. Dk Mpango alizungumzia mambo mbalimbali yanayohusiana na maendeleo, lakini pia mapendekezo ya Serikali kuhusiana na bajeti ya mwaka ujao, akiainisha baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana kutokana na bajeti inayoelekea ukingoni.

Katika hotuba yake alilitaja Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuwa limepata ndege nyingine tatu na hivyo kufanya idadi ya ndege zilizonunuliwa kuwa sita na kulipia sehemu ya gharama ya ndege mbili mpya zinazotarajiwa kuwasili mwaka huu.

Pia, alizungumzia miradi ya umeme ambayo imefanyika, huduma za maji mijini na vijijini, uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa ajili ya uendeshaji biashara na uwekezaji na pia kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu ambapo miradi mingi eneo hili ina lengo la kuendeleza huduma na miundombinu ya aina mbalimbali.

Waziri huyo alizungumzia Mpango wa Maendeleo wa 2019/20 ambao utakuwa wa nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016-2021), unaolenga kujenga uchumi wa viwanda.

Pamoja na hoja mbalimbali alizozungumzia, yapo maeneo ambayo tunaamini kwamba yanahitaji mjadala mpana na huru ili kuweza kufanikiwa, hususan katika bajeti ijayo. Miongoni mwa mambo hayo ni suala la viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda. Hili ni eneo muhimu, na ni vyema wabunge watakapokuwa wakiujadili mpango huu pamoja na bajeti husika inayozungumzia viwanda wakaweka tofauti zao za kisiasa na uchama pembeni ili kuhakikisha kwamba wanaisaidia Serikali kuufanya utekelezeke. Ni wazi kwamba sekta ya viwanda haiwezi kufanikiwa bila kuwa na mpango bora ‘ulioshiba’ utakaoiwezesha kufanikiwa. Huu ni mpango unaohitaji mawazo na mchango wa wabunge watakapokuwa wakijadili bajeti ijayo.

Si hivyo tu, Dk Mpango alizungumzia mchango wa wahisani katika bajeti ya 2018/19 iliyokuwa na jumla ya Sh32.5 trilioni akisema mpaka sasa wamechangia asilimia sita ya fedha walizoahidi. Hili ni jambo linaloshangaza kwani mkwamo wa utekelezaji wa bajeti ni wazi utakuwa umeonekana katika maeneo fulani fulani.

Tunatarajia kwamba wabunge wataisaidia Serikali kuainisha vyanzo vipya vya mapato visivyo sumbufu kwa wananchi vitakavyotumika kukusanya fedha kwa ajili ya bajeti ijayo iliyotajwa kuwa ya Sh33.1 trilioni.

Si hivyo tu, lakini pia wabunge wajiandae kwa mchango wa mawazo unaoweza kuifanya bajeti ikawa pungufu ya hiyo, lakini inayotekelezeka kulingana na mapato yetu ya ndani. Hatutarajii kusikia kwamba kwa vile wahisani ambao nao wana mchango katika bajeti wamelegalega kusaidia, basi wananchi watwishwe mzigo mzito usiotekelezeka kwa urahisi. Ni vyema Serikali na wabunge wakakubaliana.

Huko nyuma uzoefu ulionyesha kwamba kuna wakati wananchi walitwishwa mzigo wa kodi za ‘ajabu’, mfano ni ile ya kichwa ambayo iliwafanya wengi kukimbia makazi wakati mwingine kukimbilia porini ili wasikamatwe, na matokeo yake uzalishaji uliathirika kwa sababu hawakuwa wakizalisha ipasavyo kwa hofu ya kukamatwa.

Ni matarajio yetu kwamba, baada ya Dk Mpango kuwasomea wabunge mpango wa mwaka ujao na ukomo wa bajeti hiyo, sasa wabunge watafakari namna gani wataisaidia Serikali kufanikisha yaliyotajwa, lakini pia Serikali iwe tayari kukubali ushauri wao.