MAONI: Maandalizi ya Taifa Stars yanatutia shaka

Monday May 13 2019

 

Wapinzani wa Timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), Kenya, Algeria na Senegal wametangaza ratiba ya maandalizi yao kuelekea fainali hizo zilizopangwa kufanyika Misri mwezi ujao.

Timu hizo tatu pamoja na Taifa Stars zipo Kundi C katika mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Wakati timu hizo zikitoa ratiba za kambi, kwa Stars hadi sasa kilichowekwa wazi ni mchezo wake wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo Misri Juni 13 kwenye Uwanja wa Bourg Al Arab na kikosi cha awali kwa ajili ya michuano hiyo.

Kenya inayonolewa na kocha Mfaransa, Sebastien Migne imepanga kuingia kambini Ufaransa kuanzia Mei 30 hadi Juni 17 na imepanga kucheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki. Itacheza na Madagascar Juni 7 na wiki moja baadaye itacheza mechi nyingine dhidi ya majirani zao Uganda kati ya Juni 14 au 15.

Algeria itaweka kambi Doha na Abu Dhabi na imepanga kucheza mechi moja ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Mali huko Abu Dhabi, Falme za Kiarabu Juni 16.

Senegal kambi yake itakuwa Hispania na ikiwa huko itacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu za DR Congo na Nigeria.

Kwa kuangalia maandalizi ya wapinzani wetu na viwango vyao vya ubora, ni dhahiri kwamba Taifa Stars inajiandalia mazingira magumu katika michuano hiyo.

Timu zote tatu, zina wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa wakiwa wanachezaji ligi kubwa duniani ikilinganishwa na wachezaji wetu, hivyo katika hali ya kawaida tulitarajia kwamba Stars ndiyo ingeongoza kwenye upande huo wa maandalizi.

Kwa miaka nenda rudi, viongozi na makocha wetu wamekuwa na tabia ya ahadi tamtam za ‘tumejiandaa vya kutosha, tunakwenda kupambana, tutarudi na ushindi’ kila timu zinapokwenda kushiriki michuano mbalimbali na haohao wamekuwa wepesi kulalamikia maandalizi wanapofanya vibaya.

Tunataka hali hii ibadilike, hatutaki kusikia tena visingizio vya aina hii. Kila mwanamichezo anafahamu fika kwamba siri kubwa ya ushindi ni maandalizi, iweje hali hii ya kulalamikia maandalizi iwe inajitokeza tena pale timu husika inapokuwa imeaga mashindano?

Kwenye fainali za Afcon, Stars itafungua dimba na Senegal Juni 21 na kisha Algeria wakati mechi yake ya mwisho itachuana na ndugu zao wa Kenya. Kama hatutakuwa na maandalizi makubwa kulinganisha au kuwashinda wapinzani wetu, nafasi yetu kusonga mbele katika fanaili hizo itakuwa ni ya kubahatisha.

Hii ni mara ya pili kwa Stars kushiriki fainali hizi, mara ya kwanza ikiwa mwaka 1980 huko Nigeria ambako haikushinda mechi yoyote katika fainali hizo zilizokuwa na timu nane.

Kwa rekodi hiyo, tulitarajia kwamba katika fainali za mwaka huu ambazo zitashirikisha timu 24 kutoka utaratibu wa awali ambao ulikuwa ni timu 16, Stars itafanya vyema zaidi, lakini ikiwa itakuwa imeandaliwa vizuri. Lakini kwa hali ilivyo sasa, maandalizi yake yanatutia shaka.