Madhara ya mvua yapate ufumbuzi wa kudumu

Saturday May 11 2019

 

By Mhariri

Mvua za masika zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Kama ilivyozoeleka katika baadhi ya maeneo mvua hizi licha ya kuwa muhimu kwa kilimo na shughuli nyingine, pia husababisha madhara mbalimbali kama mafuriko, kuharibu miundombinu ya usafiri, usafirishaji na kusababisha milipuko ya magonjwa.

Kila mara Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) hutoa taarifa za kutaka watu wajiandae kukabiliana nazo kutokana na uwezekano wa kusababisha maafa hayo na kuharibu makazi na upungufu wa chakula baada ya kuharibu mazao. Hivyo, katika matangazo ya TMA wananchi hukumbushwa kuhakikisha maisha hayawi hatarini kwa kuhama kutoka maeneo hatarishi, kama vile mabondeni na kusafisha mitaro ya maji machafu ili kuhakikisha maji ya mvua yanapita bila kikwazo kuelekea sehemu yalikoelekezwa.

Serikali nayo ilitakiwa kuchukua hadhari kwa kufanya jitihada kubwa za kutoa elimu kwa watu waishio mabondeni kuhama, kusafisha mitaro ya maji machafu na kuimarisha miundombinu, kuandaa makazi ya muda ya watu watakaoathiriwa na mvua hizo na kukiweka tayari Kitengo cha Maafa ili kikabiliane na janga lolote linaloweza kusababishwa na mvua hizo.

Pamoja na athari zote hizo ambazo huelezwa mapema na mamlaka husika, bado mvua hizo zikinyesha huleta madhara yaliyotabiriwa mapema. Ni kama ambavyo sasa maambukizi ya ugonjwa wa dengue yanavyoongezeka katika maeneo mengi na tusipokuwa makini hata kipindupindu kinaweza kupiga hodi.

Kwa miaka mingi unakuta madhara ya mvua yanayotokea ni yaleyale na maeneo yanayoathirika hayabadiliki kila mwaka lakini hakuna juhudi za makusudi zinazoonekana za kumaliza tatizo hilo moja kwa moja.

Advertisement

Chukulia mfano wa eneo la Jangwani, kila mvua ikinyesha maji yanajaa yanaopita hadi juu ya barabara ya Morogoro. Magari yanafungiwa kwa muda kupita, mabasi ya mwendokasi yanahamishwa. Watu wanahama au wanahamishwa lakini tatizo halimaliziki miaka nendarudi.

Ukiuliza unakosa jibu, hivi nini kinashindika kuupanua Mto Msimbazi kwa kina na upana na kujengea kuta zake hadi bahari ili kukomesha tatizo la maji kujaa na kusababisha mafuriko?

Hata kama tulishaamua kutosikia kelele za kituo cha mabasi ya kasi kujengwa bondeni, lakini kingo za mto huo zingeweza kufanyiwa kazi na kumaliza tatizo kabisa.

Tumetoa mfano wa Msimbazi hasa eneo la Jangwani kama mfano wa maeneo mengine yote, ya Dar es Salaam na mikoa mingine ambayo madhara ya aina ileile yamekuwa yakijirudia mwaka hata mwingine.

Waathirika wakubwa matatizo yatokanayo na mvua ni wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni na karibu na kingo za mito ambayo mara kwa mara hujaa maji. Na maeneo yanayoathirika zaidi ni mfano eneo la Msasani Bonde la Mpunga, Mikocheni, Tegeta, Tandale, Tabata Kisiwani, Kigogo na mengineyo kama ya Kilosa na Dumila mkoani Morogoro.

Tatizo lililopo ni kwamba mvua hizo tunazichukuliwa za kawaida kama vile ni za dharura na hazikutarajiwa. Lakini ukweli ni kwamba mvua zina msimu unaofahamika, zinajulikana zitanyesha miezi gani. Zaidi TMA hutabiri kila mara na kueleza kiwango cha mvua kinachotarajiwa kunyesha na madhara yanayotarajiwa.

Hivi ni wajibu wetu kusikia tahadhari au kuacha na kukabiliana na athari kama tulivyozowea. Lakini tukiendelea na mtazamo wa sasa, mvua zitaendelea kuwa na madhara kwetu hata kama watu wote watahama mabondeni.