Chakula, mapenzi na chuki kuhusu wanyama uzunguni

Sunday January 14 2018Freddy Macha

Freddy Macha 

Wanyama ni kitu kikubwa sana uzunguni. Sana.

Wiki hii habari za mshashi aliyeua paka, kunaswa na maaskari, zimestawisha gumzo na vifua vya wenyeji. Bado madai hayana hakika (kisheria), lakini mshukiwa (miaka 31) alishasababisha vifo lukuki vya paka. Hapendwi asilani. Mbali na kuwakata kata paka na kuwatupa nje ya nyumba za wenyewe, anashutumiwa kuunguza nyumba za watu moto.

Bila sababu. Wazungu wanahusudu sana wanyama. Sana.

Wanahusudu kiasi ambacho asilimia 94 ya wananchi wameafiki kufungwa kwa vituo vyote vinavyofuga wanyama wacheza sarakasi Uingereza. Vimekuwepo karne mbili na nusu sasa. Wanyama walioletwa toka mabara yenye joto– Asia, Afrika na Marekani ya Kusini, walihifadhiwa kuwa vivutio vya kibiashara (“zoo”) kwa watalii na familia.

Sisi Afrika huwinda wanyama (ujangili) kuuza sehemu za miili yao au kuwatafuna.

Nyama pori tamu.

Wenzetu huwafanya burudani ya macho; na hilo limesemwa ni unyanyasaji. Kampeni zimefanyika miongo mingi.

Mmoja wa wanyama maarufu mathalan ni tembo - umri miaka 60 – jina Anne- aliyeletwa angali mdogo. Leo mgonjwa : mifupa na viungo, hasa miguu.

Mapenzi kwa wanyama si madogo.

Siyo, nini?

Hapo hatujazungumzia kufuga mbwa, paka, panya, sungura, mamba, sokwe, nyoka nk.

Refu zaidi ni chakula

Vuguvugu la kutokula nyama linazidi kufura kutokana na sababu za kibiashara. Matumizi ya dawa na utesaji wa kuikuza mifugo haraka ili kuchuma fedha yamezua wanaharakati wanaoyapigania maslahi ya viumbe hawa kwa vyama, silaha, fedha, siasa na hasira.

Moja ya upinzani ni kuzuia wanayasansi kushughulisha wanyama kutafiti maradhi yasiyo na ufumbuzi mfano, saratani. Ingawa sababu ya kutumia wanyama (kama nguruwe, nyani na panya) ni kwa manufaa ya afya zetu wanadamu, makundi haya ya Ukombozi wa Wanyama (“Animal Liberation”) yamekuwepo zaidi ya miaka 40. Wasanii na watu maarufu walioshastaafu na wanahangaika usiku na mchana kutetea haki za wanyama. Mfano adhimu ni mwigizaji mashuhuri wa Kifaransa, Brigitte Bardot, aliyesisimua dunia miaka 50-60 iliyopita.

Wiki jana mwimbaji na mtangazaji maarufu, Alexa Dixon alidai siku akishinda mamlaka ya kisiasa atapiga marufuku kabisa kula nyama na sigara.

Yapo makundi matatu ya walaji

La kwanza ni “Vegetarian” wanaokula majani na matunda tu. Wanaofuata ni “Pescatarian” kama Alexa Dixon anayependa mboga, matunda na samaki tu.

“Pesca” – (“Pisces” lugha ya Kinajimu) , kwa Kilatino ni kuvua samaki. Hudai ni afya zaidi kula wanyama wa majini kuliko wa ardhini. Utata uliopo ni habari za kujazana plastiki baharini. Imetabiriwa utupaji plastiki ukiendelea kasi ulivyo, hatutakuwa na samaki mwaka 2050!

Wa tatu ni “Vegans.”

Vuguvugu la Mavegan linatisha Uzunguni. Vegan hali chochote cha mnyama, kuanzia mayai, maziwa ya wanyama, nk. Maradhi mengi hutokana na ulaji nyama mathalan : unene, kiharusi, kisukari, jongo na figo.

Vegan na Vegetarian ni pia watetezi wa usafi wa mazingira.

Mwezi Oktoba 2017, lilifanyika tamasha la siku mbili, London, kutangaza Vegan. Takwimu za gazeti la Evening Standard, London karibuni zilidai Vegans wameongezeka kwa asilimia 150 miezi 12 iliyopita. Vuguvugu hili (la kibiashara) linasisitiza vyakula asilia visivyogusa nyama pamoja na vinywaji vinavyotokana na matunda, kongwa, mbegu, nazi, miti, mimea, nk.

Advertisement