Je, Huu unaweza kuwa mwanzo wa mwisho wa Tanzania kuwa sauti ya Afrika

Saturday January 20 2018

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wao uliofanyika makao makuu ya umoja huo jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, Januari 2017. Picha ya Maktaba. 

By Khalifa Said, Mwananchi [email protected]

Kuna hofu miongoni mwa wasomi na wananchi wa kawaida nchini kwamba hadhi iliyojijengea Tanzania katika kupigania utu na heshima ya Waafrika na wale wenye asili ya Afrika, hatimaye inaweza ikachukuliwa na mataifa mengine kutoka Afrika.

Hakuna shaka kwamba Tanzania inatambulika na historia yake kutukuzwa ndani ya bara la Afrika na dunia kwa ujumla. Heshima hii si tu inatokana na mchango wake katika kusaidia ukombozi wa Bara la Afrika, bali pia msimamo wake usiyoyumba wa kukemea kutoheshimiwa kwa Afrika na watu wake.

Hii inaenda sambamba na upigaji vita dhidi ya aina zote za ukandamizaji, udhalilishaji na unyonyaji dhidi ya Mwafrika.

Lakini, wasomi na wachambuzi waliozungumza na Mwananchi pamoja na wale waliochapisha maoni yao katika mitandao ya kijamii, hususan katika mtandao wa Twitter, wameonyesha kuvunjika moyo na jinsi historia hii adhimu inavyotunzwa na kudumishwa hadi inaanza kupotea.

Wametahadhirisha kwamba kwa sababu nchi imeweka mkazo zaidi katika dipolomasia ya kiuchumi inayotoa kipaumbele kwenye uwekezaji, mikopo, misaada na ushirikiano wa biashara huria kati ya mataifa, huku ikionekana kutokuweka mkazo katika masuala ya heshima na utu wa Mwafrika, kunaifanya nchi kuwa hatarini kupokwa hadhi yake iliyojijengea kwa muda mrefu kama mfano wa kuigwa katika umajumui wa Afrika.

Maoni hayo yamekuja kufuatia kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump kwamba nchi za Afrika pamoja na Haiti na El Salvador ni mataifa machafu, lakini ikakosa mwitikio wa Tanzania kama nchi katika kuilani na kuikemea kauli hiyo.

Kauli hiyo ya Trump iliripotiwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Marekani la Washington Post, kuwa Trump alihoji ni kwa nini wananchi kutoka nchi hizo zilizotajwa wanaruhusia kuingia nchini Marekani badala ya kuchukua watu kutoka nchi tajiri na zilizo na watu weupe wengi, kwa mfano, Norway.

Trump mwenyewe amekanusha kutumia neno ‘nchi chafu’ (shitoles) ingawaje amekiri kutumia lugha kali wakati wa majadiliano na wajumbe wa bunge la Congress la nchi hiyo, juu ya masuala yahusuyo uhamiaji.

Nchi kadhaa za Afrika zimelaani kauli hiyo ya Rais Trump. Si tu kwamba nchi hizi zimetoa kauli za kukemea matamshi hayo yanayodaiwa kuwa ya kibaguzi bali pia zimewaita mabolozi wanaoiwakilisha Marekani nchini mwao.

Botswana ilikuwa ni nchi ya kwanza kulaani matamshi hayo ya Trump ambapo Serikali ya taifa hilo la kusini mwa Afrika ilimwita Balozi wa Marekani nchini humo kuelezea kukasirishwa kwake na kauli hiyo ya Trump na kutaka kujua kama miongoni mwa nchi alizozitaja Trump kama nchi chafu na Botswana ni moja wapo.

Akizungumzia kauli hiyo ya Botswana ambayo ilikuwa ikisimbaa sana katika mtandao wa Twitter, Profesa Issa Shivji, mmoja kati ya wanazuoni wa Umajumui wa Afrika wanaoheshimika nchini na kwingineko duniani, alisema:

“Kuna wakati ambao sisi (Tanzania) tungekuwa wa kwanza kulaani kauli kama hizi.”

Profesa Shivji, ambaye pia ni mkurugenzi wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere alitanabahisha kuwa katika zama hizo mataifa yote ya Afrika yalikuwa yanaisubiri Tanzania itoe tamko ndipo wao wafuate.

“Sijuwi sasa tuko wapi!” aliandika kwa mshangao.

Profesa Safari asema

Kwa upande wake, Profesa Abdallah Safari anaunguna na wengine kusikitishwa na jinsi Serikali ya Tanzania ilivyokabiliana na kauli hiyo, akibainisha kwamba kulikuwa na haja, kama nchi, kutoa tamko ambalo lingeweza kujipambambanua na kuonyesha msimamo wake.

Profesa Safari ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema na wakili wa kujitegemea, ameiomba Tanzania na nchi zingine za Afrika kwa ujumla “kujitathmini” na “kujisahihisha” katika namna wanavyoendesha nchi zao hususan katika maeneo ya utawala bora, haki za binadamu, pamoja na ugawaji sawa wa rasilimali za Taifa.

Kiongozi huyo ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Masomo na Programu wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa kilicho chini ya Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa anasema, “Kama kuna chochote kinachoweza kutufanya tuwe ‘wachafu’ basi itakuwa ni kwa namna gani tunashughulikia mambo haya. Wakati tukilaani kauli ya Trump, tusipuuze kauli yenyewe. Ikiwa ni kweli basi tujisahihishe.”

Tanzania sehemu ya AU

Haijajulikana kama bado Serikali itaonyesha ukinzani rasmi dhidi ya Serikali ya Marekani nchini na kumwita balozi wake kwa ufafanuzi kama nchi zingine zilivyofanya au la.

Si waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga wala naibu wake, Dk Susan Kolimba aliyepatikana kuzunmgumzia msimamo wa Tanzania kuhusu matamshi hayo yaliyoonyesha kuwakera watu wengi.

Hata hivyo, kwenye mahojiano aliyofanya na gazeti hili awali baada ya habari kuhusu matamshi ya Trump kuripotiwa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda alisema msimamo wa Tanzania umewakilishwa katika kauli ya Umoja wa Mataifa ambako nchi 54 za Afrika ni wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

“Tanzania ni sehemu ya AU na hivyo ni sehemu ya kauli ya UN,” anasema.

Profesa Mkenda alikuwa anarejea kauli ya UN ambayo ilisema hakuna namna yoyote ya kuilezea kauli ya Trump isipokuwa kuwa ni ya kibaguzi.

Trump mwenyewe amekanusha hadharani kwamba yeye ni mbaguzi akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua kama kweli yeye ni mbaguzi au la.

Pamoja na msimamo huo usioonyesha wazi nafasi ya Tanzania kama nchi, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu ambaye chama chake kililaani kauli hiyo ya Trump, anasema kutoa kauli chini ya mwavuli wa AU tu haitoshi.

Anasema hiyo haiakisi nafasi na heshima ambayo kama nchi imejizolea huko nyuma katika kusimama mstari wa mbele kulinda na kuenzi utu na heshima ya Mwafrika.

“Tulitakiwa kama nchi, tutoke hadharani kulaani kauli hii ya kibaguzi. Hiyo ndiyo Tanzania watu wanayoijua na kuiheshimu,” anasema.

Anaongeza kuwa wananchi wana kila sababu ya kuwa na wasiwasi ikiwa hii ndiyo itakuwa desturi ya nchi yao.

“Utambulisho wetu kama Taifa na nafasi yetu inapokwa, tutajivunia nini tena?” anauliza Shaibu.

Serikali ya Afrika Kusini imefuata mkondo wa Botswana kuonyesha ukinzani wa wazi dhidi ya kauli ya Trump kwa kuutaka ubalozi wa Marekani nchini humo kuitoloea ufafanuzi kauli hiyo.

“(Serikali) itatoa fursa kwa balozi (wa Marekani nchini) kufafanua kauli kwamba mataifa ya Afrika pamoja na yale ya Haiti na El Salvador ni machafu,” taarifa iliyotolewa na Idara ya Mahusiano ya Kimataifa ya nchi hiyo ilisema.

Marekani yakiri mabalozi kuhojiwa

Akihojiwa na CNN, Naibu katibu mkuu wa Mambo ya nje wa Marekani, Steve Goldstein anakiri kuwa maofisa wao kadhaa wa kidiplomasia wa ngazi za juu kutoka Afrika Kusini na Ghana wamehojiwa na Serikali za nchi hizo.

Serikali za Haiti, Botswana na Senegal pia zimewahoji mabalozi wa Marekani nchini mwao katika siku za hivi karibuni, CNN imeripoti.

“Rais ana haki ya kusema lolote analohisi linafaa na tunamheshimu,” Goldestein aliiambia CNN lakini akabainisha kuwa mabalozi wameelekezwa “kusisitiza kwamba Marekani bado ina dhamira ya kuendeleza mahusiano yaliyopo na nchi hizi na inajali sana kuhusu watu wake.”

Umoja wa Ulaya na mabalozi wa Afrika katika Umoja wa Mataifa waliipinga kauli hiyo ya Trump ambayo imezua mjadala duniani kote na kumtaka aitengue na kuomba radhi.

“Umoja wa Ulaya Unapenda kuelezea hasira na kutoridhishwa kwake na kauli ya bahati mbaya iliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump ambayo inaonyesha kutoheshimu tunu ya Marekani na heshima katika utofauti na utu wa binadamu,” linasema tamko la AU.

Serikali zingine barani Afrika zimejibu kauli hiyo ya Trump kwa jazba.

“Nimeshtushwa na maneno ya Rais Trump juu ya Haiti na Afrika,” aliandika Rais wa Senegal, Macky Sall katika ukurasa wake wa Twitter.

“Nayakataa na kuyalaani vikali. Afrika na watu weusi wanastahili heshima na mazingatio ya watu wote. Inaonekana kama habari ya uongo kwangu,” anasema Waziri wa habari wa Somalia, Omar Osman alipohojiwa na CNN.

0716 874501

Advertisement