Mfunze mwanao bila adhabu ya viboko

Sunday January 21 2018

 

Wengi wetu tunajifunza kulea tukiwa tayari ni wazazi. Yaani ‘mafunzo kazini’, unaingia katika malezi bila uzoefu wa aina yoyote kwani katika maisha yako hujawahi kulea mtoto. Hivyo mara nyingi tunategemea aina ya malezi tuliyopewa na wazazi / walezi wetu kama sehemu ya ‘uzoefu’ wa namna ya kulea watoto wetu wenyewe. Utakubaliana nasi kwamba wengi tulichezea mikong’oto ya aina mbalimbali kuanzia kwenzi, vibao, fimbo na hata kutukanwa na walotulea kama sehemu ya maonyo ya kujenga tabia. Tumezungumza na mzazi na mwalimu aliyelea na kuishi na watoto bila kuwapa mikong’oto. Jongea nasi.

Mwalimu Patricia mwanzilishi wa shule ya chekechea ya Pat Pre-School anasema inawezekana.

Anaeleza kuwa alipopata ajira International School of Tanganyika miongo kadhaa iliyopita alipigwa butwaa juu ya namna gani anaweza kuwafundisha watoto bila fimbo. Anasema shule hiyo ilimtambulisha katika ulimwengu wa malezi bila viboko. Watoto wanapokosea zipo adhabu mbadala ambazo hutumika. Mfano wa adhabu hizi ni pamoja na kumnyima mtoto fursa ya kutoka mapumziko pindi muda huo unapotimu. Wenzake wanapokwenda kucheza nje ya darasa, yeye anabaki darasi kutumikia adhabu yake. “Hakika kwa ‘kifungo’ hiki, atajutia kosa lake na hawezi kutaka kurudia kosa lile.” Mwalimu Patricia.

Mwalimu Patricia anasema yeye amewalea watoto wake wote bila ya viboko na wamefikia utu-uzima pasi na chembe ya mushkeli. ‘Iwapo lengo la malezi ni kujenga tabia ya mtu-mzima unayemtaka mtoto hatimaye afikie. Mtu mzima mwenye maadili na mchango katika jamii yake. Habari gani kwamba viboko vitamjenga?’ Anauliza Mwalimu Patricia.

Daktari Joan Durrant mtaalamu mwandamizi wa malezi, anasema kulea ni kufundisha.

Anatabainisha kwamba lengo la adhabu zitolewazo kwa hakika ni funzo kutokana na kosa alilotenda mtoto. Funzo lenye lengo la kujenga misingi ya tabia ili mtoto afikie ‘ubinadamu’ wa matamanio yako mzazi / mlezi. Kwamba chimbuko la adhabu mbadala wa mikong’oto ni kuheshimu utu wa mtoto kama kichanga mwenye kiu ya kujifunza. Pafanye nyumbani kwako kuwa sehemu sahihi ya kujifunza. Ambapo vijiswali vingivingi toka kwa watoto vinaonekana kana kwamba ni fursa adhimu ya kujenga misingi ya maadili.

Zungumza

Wataalumu wa malezi wanasema jambo la muhimu katika malezi mbadala wa viboko ni kuuliza maswali. Maswali kama: je nataka mtoto wangu akikua awe mtu wa namna gani? Vipi awe mkarimu na mwenye mchango muhimu kwa jamii?

Mwenye hekima-katika-maamuzi? Asiwe mgomvi. Anipende na aipende familia yake - mwenza wake na watoto akijaaliwa. Iwapo una matamanio kufikia walau moja ya malengo hayo, huihitaji kiboko kama nyenzo. Unachohitaji ni mkakati. Mipango mama, mipango baba.

Kwamba mikong’oto itakusaidia kutoa hasira zilizokujaa wakati huo wa kosa la mtoto. Mazungumzo yatakusaidia kumfanya mtoto sehemu ya mipango ya kufanikisha kujenga tabia ya mtu mzima wa matamanio yako.

Mfahamu mtoto – anawaza nini? Anahisi nini?

Umri wa mtoto unatueleza matarajio ya uelewa na hisia zake. Tuchukulie mfano wa mtoto mchanga. Yeye haelewi mambo mengi. Hajui hata maana ya kukasirika. Anapolia mara zote hana lengo la kukuudhi na kwamba mara nyingi huogopeshwa hata na sauti za kulia kwake yeye mwenyewe. Hivyo yawezekana mtoto akapiga mayowe kwa kilio kuogopa sauti anayoisikia akilia! Alaa! Fundisho hapa ni kwamba ukijua uwezo wa kuelewa kwake itakusaidia kuwa na matarajio halisia yanaorandana na umri wa mtoto wako.

Advertisement