Michezo inayoweza kudumaza uwezo wa mtoto

Tuesday December 12 2017Christian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

Hivi karibuni, niliongea na mwalimu wa shule moja ya msingi mjini Moshi. Kwake, michezo na masomo ni vitu viwili visivyoweza kwenda pamoja. Mwalimu huyo alinieleza: “Ukiruhusu michezo shuleni, akili za watoto zitawaza michezo muda wote. Hawawezi kuzingatia masomo.”

Akaongeza: “Hapa shuleni kuna watoto wengi wanaopenda sana games (michezo ya kidijitali inayochezwa kwenye kompyuta na vifaa maalum vya kielektroniki.) Michezo kama hii imeathiri uwezo wao kufuatilia masomo wanaporudi nyumbani.”

Mwalimu ana hoja kwa upande mmoja. Pamoja na umuhimu wa michezo katika ukuaji wa watoto wetu, ipo haja ya kuangalia aina ya michezo inayomfaa mtoto.

Michezo ya kisasa

Teknolojia imebadili namna watoto wetu wanavyocheza. Wakati zamani tulikwenda viwanjani na kwenda nje ya nyumba tukifukuzana na kukimbia, leo watoto wa mjini wanacheza michezo karibu yote wakiwa sebuleni au kwenye vyumba vyao vya kulala.

Kama alivyosema mwalimu, michezo ya kisasa kama ‘games’ imekuwa maarufu kwa watoto. Mtoto anaweza kutumia kifaa kidogo cha kielektroniki kucheza mchezo wa kuunda maumbo mbalimbali, kuigiza hali ya kufikirika (simulation) kwa kupanga mikakati, mathalani, ya kumshinda mpinzani wake wakati mwingine kwa kumpiga risasi na mabomu.Pia, watoto wanaweza kucheza kwa mfumo wa kutazama kinachofanywa na watoto wenzake waliorekodiwa tayari, kama katuni zinazoonyeshwa kwenye video au vituo vya televisheni.

Katika michezo kama hii, mtoto hafanyi shughuli yoyote zaidi ya kukaa, kubofya vitufe kwenye kifaa vya kielektroniki, au kufikiri namna ya kupambana na ‘maadui’ wake wa kufikirika kwenye michezo.

Sambamba na michezo hii ya kiteknolojia, ipo michezo inayotumia vifaa vilivyotengenezwa tayari. Mtoto kwa mfano anaweza kununuliwa mwanaserere, midoli ya gari, nyumba, wanyama na kazi yake inabaki kujifunza namna ya kuitumia kwa mujibu wa waliotengeneza vifaa hivyo.

Uraibu

Michezo kama hii inayotumia teknolojia ina tabia ya kutengeneza tabia ya uraibu. Uraibu ni ile hali ya kuzoea kitu kiasi cha kutoweza kuachana nacho kirahisi.

Michezo hii imetengenezwa kwa kufuata mfumo wa kamari inayotengeneza shauku ya mtoto kuendelea kucheza ili kujua nini kitatokea.

Shauku hiyo, hujengwa, aghalabu, na motisha ya kushinda kwa kuwaua maadui wa kufikirika, kupata pongezi za sauti au alama za ushindi.

Michezo ya namna hii inaweza kumfanya mtoto akawa na aina fulani ya ulevi kwa kuuzoea mchezo kiasi cha kukosa utulivu asipocheza mchezo huo.

Ingawa ni kweli michezo hii huweza kukuza uwezo wa mtoto kufikiri kwa haraka kama ilivyo kwa michezo ya asili, changamoto yake ni kutegemea ubongo na vidole pekee.

Tukiongeza na uraibu, kwa hakika, michezo hii inaweza kuwa hatari si tu kwa malezi ya watoto, bali hata kwa maendeleo ya mtoto shuleni.

Kukosa uzingativu

Kuna malalamiko mengi kutoka kwa walimu kuwa watoto wa siku hizi, hasa mijini, hawana uzingativu darasani. Walimu wanasema kumpa mtoto kazi inayohitaji uzingativu wake kwa dakika kadhaa inaanza kuwa vigumu.

Sababu moja wapo inaweza kuwa ni mazoea ya aina fulani ya vitu anavyoviona kwenye michezo yake ya kiteknolojia isiyopatikana katika mazingira ya darasani.

Kwa mfano, mtoto aliyezoea tabiti kucheza michezo yake ya ‘kutafuta namna ya kutoroka kwenye kambi ya jeshi,’ hawezi kuona uwezekano wa kujifunza lolote kupitia maelezo yanayotolewa kwa kuchorachora ubaoni.

Umakini ni sifa muhimu katika masomo. Ili mwanafunzi afanikiwe lazima awe na uwezo wa kufuatilia kwa umakini kile kinachosemwa na mwalimu. Awe na uwezo wa kutumia macho na masikio yake kuchunguza wakati anapohitajika kufanya majaribio.

Mtoto asiyeweza kusikiliza maelezo ya mwalimu kwa sababu tu yanasemwa kwa namna isiyomvutia, anakuwa kwenye hatari ya kufanya vibaya kwenye masomo yake.

Kuiga tabia zisizofaa

Kuna visa vingi vya watoto kujifunza tabia za ajabu kupitia michezo inayopatikana kwenye ‘games.’ Ili kuifanya michezo hii ya kiteknolojia iwe na mvuto kwa watoto, wabunifu wake hutengeneza mazingira yanayoongeza msisimko.

Namna moja ya kuweka vionjo vya msisimko ni kumfanya mtoto apigane na maadui wakufikirika. Ili ashinde mchezo husika, mtoto hulazimika kutumia silaha kama bunduki na makombora kuwamaliza ‘wabaya’ wake.

Wakati mwingine, mtoto hutazama katuni zenye wahusika wanaoonyesha ukatili. Mara nyingi wahusika wenye ukatili na ubabe ndio wanaopendwa na watoto.

Albert Bandura, mwanasaikolojia maarufu wa karne ya 20, anasema michezo kama hii inawafundisha watoto kuiga tabia wanazoziona kupitia vifaa vya mawasiliano.

Siku hizi tunafahamu, mathalani, watoto wengi huwa wakorofi, wagomvi kwa wenzao. Kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto hujifunza tabia hizi kupitia michezo wanayoicheza chini ya uangalizi wa wazazi wao.

Matatizo ya afya

Michezo mingi ya kisasa haimhitaji mtoto kutumia viungo vya mwili wake kama ilivyokuwa hapo zamani. Badala ya mtoto kwenda mtaani kurukaruka na wenzake, anabaki sebuleni akishikashika kifaa chake.

Mtoto huyu anaweza kucheza mchezo unaokuza uwezo wake wa kufikiri, lakini akajikuta muda mwingi hana anachofanya kinachoweza kutumia nguvu za mwili wake.

Hali kama hii kwa kiasi kikubwa huchangia matatizo mengi ya afya, ikiwamo kuongezeka kwa uzito kupita kiasi, maumivu ya mgongo, matatizo ya macho katika umri mdogo na changamoto nyingine za kiafya.

Ushauri

Pamoja na kukua kwa teknolojia inayobadili namna watoto wanavyoweza kushiriki michezo, wazazi tuna wajibu wa kuhakikisha muda unaotumiwa na watoto kucheza michezo hii unadhibitiwa.

Kila inapowezekana, mzazi afanye ukaguzi wa michezo anayocheza mtoto kujiridhisha kuwa hakuna chembechembe za tabia mbovu zinazoweza kuoteshwa kwenye ufahamu wa mtoto bila yeye kujua.     

Advertisement