Mkoa wenye fursa za kutoa wataalamu wa kilimo, ufugaji

Muktasari:

  • Jambo mojawapo ambalo mkoa huo unaweza kujivunia ni kuwapo kwa vyuo ambavyo vimeweza kutoa wataalamu wa mifugo na kilimo na mpaka sasa bado vyuo hivyo vinaendelea kuzalisha wataalamu hao ambao wanaweza kujiajiri na kuajiriwa kutokana na taaluma walizonazo.

Morogoro ni mkoa ambao unasifika kwa kutoa wataalamu wengi katika masuala mbalimbali hususan wa kilimo na mifugo.

Jambo mojawapo ambalo mkoa huo unaweza kujivunia ni kuwapo kwa vyuo ambavyo vimeweza kutoa wataalamu wa mifugo na kilimo na mpaka sasa bado vyuo hivyo vinaendelea kuzalisha wataalamu hao ambao wanaweza kujiajiri na kuajiriwa kutokana na taaluma walizonazo.

Vyuo hivyo ambavyo wakazi wa mkoa huo wa Morogoro wanatakiwa kujivunia ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) na Wakala wa vyuo mafunzo ya Mifugo ( Lita).

Lita enzi za ukoloni kilikuwa kikitoa elimu ya kilimo pekee na ilipofika mwaka 1963 kilibadilishwa na kuwa chuo cha mifugo hadi sasa na kimetoa wataalamu wengi huku mwaka huu 2016 pekee, waliohitimu ngazi ya stashahada na astashahada mchanganyiko ni 301.

“Wanafunzi wanapohitimu chuoni hapa si kwamba wanategemea kuajiriwa na Serikali pekee bali tunawafundisha na fursa ya kujiajiri na tumekuwa tukiwaelimisha kuwa hata mtaji mdogo unaweza kumuinua katika kupata kipato,” alisema Jaspar Mallya, Mkuu wa Kampasi ya Lita Morogoro.

Akizungumzia fursa ambayo wakazi wa Mkoa wa Morogoro wanaweza kuitumia kupitia chuo hicho ni kupata mafunzo ya mifugo kama sungura, ng’ombe, kuku, nguruwe na kilimo cha migomba na kuwapo kwa changamoto ndogo ambazo zinaweza kuvumilika.

Mmoja wa wahitimu ngazi ya cheti katika chuo hicho katika masomo ya afya ya wanyama na uzalishaji, Erick Godfrey alisema tangu akiwa chuo aliona fursa ya kujiajiri mwenyewe ndipo alipoomba kiasi cha fedha kutoka kwa wazazi wake kwa nia ya kununua ng’ombe mmoja wa maziwa.

Godfrey ambaye kwa sasa anafuga ng’ombe wa maziwa watatu alisema baada ya kuhitimu masomo yake ameendelea na ufugaji na kwamba ndiyo imekuwa kazi yake.

“Kwa sasa ng’ombe niliyenaye anatoa maziwa kwa siku lita tisa, changamoto zilizopo sehemu ya malisho hasa kipindi cha kiangazi, soko kusumbua na kutokuwa la uhakika hivyo kufanya ufugaji kuwa mgumu,” alisema.

Ushauri kwa vijana wahitimu (wataalamu) kupitia Chuo cha Lita kutumia fursa nyingi zilizopo kwa kujiajiri si kwa kufuga tu bali hata kuwaelimisha wananchi hasa vijana ili waweze kupata uelewa juu ya kilimo, ufugaji huku akiwataka kutumia nguvu ya ziada kama umwagiliaji.

Mkuu wa chuo Mallya alisema pamoja na kuwapo kwa fursa mbalimbali chuoni hapo bado kumekuwa na changamoto ya wakazi wa Mkoa wa Morogoro kutojitokeza kwa wingi kwa ajili ya kusoma badala yake wengi wa wanafunzi waliopo ni kutoka nje ya mkoa.

Mallya alisema chuo hicho kimekuwa kikipokea wanafunzi zaidi ya 400 kwa mwaka mmoja na wengi wao husoma kwa lengo la kupata ajira serikalini ama taasisi binafsi za ndani na nje ya nchi.

Mkufunzi kutoka chuo hicho katika masuala ya kilimo cha migomba, Monica Ligoha alisema fursa ya kuwapo kwa chanzo cha maji katika chuo hicho imewawezesha kupanda migomba iliyopatikana kutoka Sua na kwa watu binafsi.

Ligoha alisema kilimo cha migomba siyo lazima kuwa na mtaji mkubwa ambao unaweza kuanza kwa kutumia nguvu kazi huku akieleza faida ya inayopatikana kwa mwezi ya Sh300,000 na lengo ni kuvuna mikungu 160 kwa mwezi.

Aliongeza kuwa wakazi wa Morogoro hutumia fursa ya kuwapo kwa maji mengi na mbolea za wanyama kuzalisha kwa wingi.

“Vijana wetu waache kukaa vijiweni badala yake watumie mbinu mbalimbali kuweza kujipatia kipato halali na kuondokana na wizi ama kupora mitaani wajiingize katika kilimo na ufugaji,” alisema.

Mkuu wa Lita, Mallya anasisitiza kuwa kama taasisi ya Serikali wana jukumu la kutoa elimu bure na kuwashauri vijana na wakazi wa Morogoro kubadilika na kujifunza ufugaji wa kisasa na bora zaidi kwa gharama nafuu.