Tumegawanyika! Ni kitu gani cha kutuunganisha?

Wednesday February 14 2018

 

Mchakato wa kuelekea kuandika Katiba Mpya ya taifa letu ulifichua siri kubwa ya Watanzania: Tumegawanyika.

Ingawa kwa kiasi kikubwa kila Mtanzania anaililia Katiba Mpya, lakini hatuiangalii kwa jicho moja la utaifa, bali kisiasa, kidini na kijamii.

Vyama vya siasa vinataka kuhakikisha Katiba inalinda maslahi, sera, malengo na matumaini ya vyama vyao vya siasa. Viongozi wa dini nao hawako nyuma, Waislamu wanataka izungumze wazi juu ya OIC na mahakama ya kadhi na mambo mengine muhimu zaidi kwa waumini wa madhehebu haya. Wakristu nao wanataka kuona inahakikisha hakuna ndoa za mashoga na suala la mahakama ya kadhi lisiingizwe; wanapenda kuona inabeba maadili ya madhehebu yao.

Makundi yanayopigania haki za binadamu na usawa wa jinsia yanataka kuzingatia haki za makundi yao, hivyo mchakato wa kuitafuta Katiba mpya uliifichua siri hii ya ufa mkubwa katika umoja wa Taifa letu.

Tumemsikia Edward Lowassa akilalamika kwamba Chadema walinyimwa uwanja wa kumuaga marehemu Tambwe Hiza. Kama ni kweli, hii ni dalili mbaya za kuligawa Taifa letu kwenye itikadi ya vyama na kuleta uhasama ambao matokeo yake ni hatari.

Ina maana kila chama kitakachoingia madarakani, kitahakikisha kinachukua kipande kikubwa cha keki tamu ya Taifa letu. Kwanini Chadema wanyimwe uwanja wa shughuli muhimu ya kibinadamu kama msiba? Nani hatakufa? Ni nani hatazikwa? Kweli tumegawanyika, na ni hatari sana.

Kama miaka 15 iliyopita niliandika sana juu ya hekalu. Kwamba Watanzania tunahitaji kitu cha kutuunganisha kama Taifa. Kwamba tunahitaji kitu ambacho kila Mtanzania atalazimika kupiga magoti na kunyenyekea kwa uaminifu na kutoa moyo wake, akili zake, nguvu zake na kila kitu chake kwa heshima na utukufu wa hekalu letu.

Na hekalu hili lisiwe na dini, madhehebu wala makabila. Liwe hekalu la Watanzania wote. Wakati nikiandika haya, kuna watu walifikiri nimechanganyikiwa, kuna watu walifikiri nataka watu wote wawe Wakristo.

Wakati ule baadhi ya watu walikuwa na upofu wa kutoona mbali, maana tulikuwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Kwa kipaji chake, hekima na busara, aliweza kuzima kwa nguvu zote dalili mbaya za kuligawa Taifa letu. Daima alikuwa mkali kama pilipili, pale mtu, watu au kikundi cha watu kilipoonyesha dalili yoyote ya kutaka kuleta mgawanyiko. Tunakumbuka kundi la wabunge 55 maarufu G 55 lililotaka Serikali ya Tanganyika, tunakumbuka matukio yaliyomlazimisha Mwalimu kuandika kitabu juu ya Hatima ya Taifa letu, tunakumbuka jinsi alivyokemea kwa nguvu zote Uzanzibari na Uzanzibara, tunakumbuka jinsi alivyotaifisha shule za kidini, ili watoto wote wa Tanzania wapate elimu bila ya ubaguzi.

Kwa vile Mwalimu aliyazima, watu walifikiri tunaweza kuendelea hivyo milele yote. Mbaya zaidi ni kwamba “upofu” huu unaendelea hadi leo hii.

Hoja yangu kubwa wakati nikisisitiza umuhimu wa hekalu ilikuwa kwamba hatuwezi kuendelea bila kuwa na kitu cha kutuunganisha, kujenga uzalendo wetu na kuchochea mshikamano miongoni mwetu.

Ingawa Mwalimu aliweza kutuunganisha, tulihitaji kitu fulani cha kudumisha mshikamano wetu hata baada ya kifo chake; cha kutusaidia lazima kutanguliza utanzania wetu zaidi ya kitu chochote.

Mbali na Muungano wetu kuyumba baada ya kifo cha Mwalimu, matukio mengine ya kidini kama vile OIC na Mahakama ya Kadhi, yaliyochomoza kwa nguvu zote wakati wa mchakato wa Katiba, yalionyesha kwamba mshikamano wetu kama taifa umejengwa mchangani na msingi si imara.

Wakati mjadala wa mahakama ya Kadhi, jambo hili la mgawanyiko lilijionyesha wazi. Wabunge Wakristo walitupitilia mbali tofauti zao za siasa na kushikamana kupinga hoja ya mahakama ya kadhi, vivyo hivyo wabunge Waislamu walitupilia mbali tofauti zao za siasa na kushikamana kutetea hoja hiyo.

Kinachoshangaza ni kwamba hoja hizi zinajadiliwa kwa misingi ya kidini. Hazijadiliwi kwa misingi ya “utaifa” kwa misingi ya “Utanzania”. Tunajigawa kwenye makundi mawili ya Waislamu na Wakristu na kuwaacha nje Watanzania wenye dini zao za jadi. Hawa nao ni Watanzania, ni lazima wawe na haki zote za kikatiba kama wengine

Wakristu wanashindwa kuelewa ni kwa nini Mahakama ya Kadhi iendeshwe kwa fedha za Serikali, fedha za walipa kodi. Waislamu nao wanashikilia hoja ya kwamba Hospitali Teule kwenye Wilaya mbalimbali ni za Wakristu na zinaendeshwa kwa fedha za Serikali, za walipa kodi.

Tunaweza kujiuliza: Je, hospitali hizi teule zinawatibu Wakristu peke yao? Je, zinaajiri Wakristu peke yao? Kwanini tusiangalie huduma zinazotolewa kwa Watanzania wote? Je, mtu anapokwenda kutibiwa anaulizwa dini yake?

Mara kwa mara hujitokeza malalamiko, mara Serikali ya imejaa Wakristu na wakati mwingine kwamba imejaa Waislamu. Nina shaka kama hili huwa ni kweli. Lakini hata hivyo, kwa nini tuangalie dini ya mtu badala ya kuangalia utendaji wake. Je, Wakristo na Waislamu hao waliojazwa serikalini wana sifa? Je, wanafanya kazi kwa moyo wa kizalendo? Je, wanatoa huduma kwa kuangalia kwanza dini ya mtu?

Kuna malalamiko kwamba vyuo vikuu vinachukua namba kubwa ya madhehebu fulani. Hili kweli? Na kama ni kweli, je wanaochukuliwa wana sifa au wanaingizwa bila sifa? Na kama wana sifa, kwa nini tusiwaangalie kama Watanzania badala ya kuwaangalia kama watu wa dini fulani. Na wasomi hawa wanapohitimu, je wakifanya kazi, wanatoa huduma kwa watu wa madhehebu yao peke yao au wanatoa huduma kwa wote?

Ni kipi kinatufanya kuwa Watanzania? Ni dini zetu za kigeni tulizozipokea zaidi ya miaka mia iliyopita, au ni “uzawa” wetu unaokwenda nyumba maelfu ya miaka? Ni kipi kinachotangulia? Ni dini zetu za kigeni au ni “utaifa” wetu? Tukijibu maswali haya, hatuwezi tena kuwa na dukuduku na masuala ya kidini .

Kwenye maandishi yangu ya nyuma, nilishadokeza kwamba dini hizi za kigeni ziliingia na kupokewa “kiushabiki”. Nikimaanisha theolojia ya dini hizi haikufundishwa kwa waumini. Viongozi wa dini hizi waliifanya theolojia, kuwa ni “siri”.

Masuala mazito ya dini yanabaki kuwa wazi kwa viongozi na kuwaacha waumini katika giza nene. Matokeo yake zinapoibuka hoja nzito za kidini mijadala inatawaliwa na ushabiki kama ule wa kwenye viwanja vya mpira. Hakuna hoja za kitheolojia zinazotolewa na waumini wa kawaida.

Hoja ninayoijenga ni kwamba, ni lazima tuwe na kitu cha kutuuganisha kama taifa. Tusitangulize dini zetu, bali tutangulize “Utaifa” wetu. Mtanzania Mwislamu, akiwa serikalini au akiwa anafanya kazi yoyote ya kitaifa, tuamini kwamba anaifanya kazi hiyo kama Mtanzania na wala si kama Mwislamu. Mkristu Mtanzania, akifanya kazi au akiongoza Serikali tuamini kwamba anafanya kazi hiyo kama Mtanzania na wala si kama Mkristu.

Tukiendekeza “udini” tunaweza kufikia hatua ya kuligawanya taifa vipande viwili, kama zilivyofanya nchi nyingine za Kiafrika. Tunahitaji hekima na busara za viongozi wetu wa dini (ninamaanisha dini zote hata na zile za jadi) na viongozi wetu wa Serikali.

Tukishapata kitu cha kutuunganisha kama Taifa, ni lazima tuwe na vipaumbele vya Taifa. Kila Mtanzania hata na mwendawazimu afahamu kwamba kitu fulani ni kipaumbele cha Taifa. Hadi sasa inatia shaka kama kweli kuna vipaumbele vya taifa.

Ukiangalia jinsi tunavyoshughulikia kilimo chetu, huwezi kusema kwamba hiki ni kipaumbele cha taifa. Bado tunatumia jembe la mkono na kumsubiri Mwenyezi Mungu, atuletee mvua. Hatupanui mashamba yetu, kule Kagera, mibuni na migomba iliyopandwa na babu zetu ndio hiyohiyo hadi leo hii. Ukiangalia afya, miundombinu, nishati, elimu na mengine, huwezi kusema kitu fulani ni kipaumbele cha Taifa.

Kila mkulima angekubali kukatwa senti hamsini kwa kila kilo ya zao aliuzalo. Wafugaji nao wangekubali kukatwa senti hamsini kwa kila mfugo wauzao. Na hili lisingefanyika kila mara, maana mikopo ya elimu inazunguka – wanaomaliza wanalipa. Kwa njia hii tungeweza kuwapatia wanafunzi wote wa elimu ya juu mkopo wa asilimia mia moja.

Wimbo kwamba serikali haina fedha, hauna kikomo. Hakuna siku itakayotokea serikali ikawa na fedha. Kazi ya kufanya kama kuna vipaumbele ni serikali kubuni vyanzo vya mapato. Serikali yenye uwezo wa kuwashawishi watu wake kwamba ni maskini, ikibuni vyanzo vya mapato ni lazima wananchi waikubalie.

Tatizo la Tanzania, pamoja na ukweli kwamba vipaumbele vyetu haviko wazi ni kwamba Serikali yetu imeshindwa kuwashawishi wananchi wake kwamba ni maskini.

Kama watu wawili wanaweza kuisababishia Serikali hasara ya bilioni 11, na wengine wakajichotea zaidi ya bilioni 123 Benki Kuu, na wengine kwa ujanja wakawa wanalipwa zaidi ya milioni 152 kwa siku, ni kiasi gani serikali hii ni maskini?

Ingawa haikuandikwa popote, kwa kuangalia tu, mtu unaweza kusema kwamba kipaumbele namba moja katika Taifa letu ni kuboresha maisha ya viongozi. Kuhakikisha wana usafiri mzuri, wana majumba mazuri, wana ulinzi wa kutosha, familia zao zinatunzwa vizuri, wanasafiri daraja la kwanza kwenye ndege na kutibiwa nchi za nje kila wanapokuwa na matatizo kiafya.

Umakini, fedha, juhudi zinazotumika kuhakikisha viongozi wetu wanaishi maisha mazuri – vingeelekezwa kwenye elimu, kilimo na nishati – taifa letu lingepiga hatua kubwa ya maendeleo. Kuna haja ya kutafuta kitu cha kutuunganisha kama taifa, na kuna kazi ya ziada ya kukaa chini na kupanga vipaumbele vya taifa. Hitaji la kuwa na Katiba mpya lituelekeze huko; kujenga taifa moja lenye mshikamano na si kuendelea kutugawanya kwenye makundi ya kisiasa, kidini na kijamii.

Padri Privatus Karugendo.

+255 754 6331 22

Advertisement