Walianza shule 103 wakahitimu saba tu!

Hali halisi ya usafiri kwa wanafunzi wengi wilayani Bahi ni kama hivi inavyoonekana kwa wanafuzi hawa wa Shule ya Sekondari Chikopelo. Kwa sababu ya umbali wanalazimika kutumia usafiri wa baiskeli. Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

Taarifa rasmi katika shule hii zinaonyesha kuwa tatizo lilianza mara tu baada ya kuchaguliwa kwao, kwani wanafunzi 23 hawakuripoti hivyo walioanza kidato cha kwanza walikuwa 68 pekee.

       Kati ya wanafunzi 91 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Chikopelo, Wilayani Bahi, Dodoma mwaka 2014, ni 26 tu ndio wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.

Taarifa rasmi katika shule hii zinaonyesha kuwa tatizo lilianza mara tu baada ya kuchaguliwa kwao, kwani wanafunzi 23 hawakuripoti hivyo walioanza kidato cha kwanza walikuwa 68 pekee.

Kutokana na “ugumu wa safari ya elimu”, zaidi ya nusu ya wale walioripoti waliishia njiani. Waliopo ni wanafunzi 26, huku 42 wakiwa wameacha masomo miaka minne iliyopita. Kati yao 14 ni wavulana na 12 ni wasichana.

Hata hivyo, mwalimu wa taaluma shuleni hapo, Ahadi Mgando anasema hali hiyo siyo mpya shuleni hapo na kwamba idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu mwaka huu “ni kubwa” ikilinganishwa na miaka iliyopita!

Mgando anarejea takwimu za awali ambazo zinaonyesha kuwa mwaka 2011 walihitimu saba tu kati ya 103 walioingia kidato cha kwanza mwaka 2008, wakati mwaka 2013 walihitimu wanafunzi nane kati ya 42 walioandikishwa kidato cha kwanza mwaka 2010.

Mwaka 2014 walihitimu wanafunzi saba kati ya 36 walioandikishwa mwaka 2011 na mwaka jana kulikuwa na wahitumu wanafunzi 25 kati ya 256 waliojiunga na kidato cha kwanza 2013.

“Hii ni changamoto kubwa sana, shule yetu ina vyumba vya madarasa vingi lakini vingi vipo wazi kutokana na utoro wa wanafunzi,”anasema.

Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa kuwa suala la utoro linaonekana kuwagonganisha vichwa walimu na wazazi, ambao walishindwa kuelewana hata katika kikao kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili suala hilo.

“Kila siku wimbo ni utoro! utoro! Lini tutajadili masuala mengine? Mimi nadhani sisi tulio humu watoto wetu wapo tayari darasani, tumieni tu sheria kuwakamata wenye watoto watoro,”anasema mmoja wa wazazi, Charles Sales.

Shule hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 320, hivi sasa inao 192 lakini mkuu wake, Juma Idosa anasema ni wanafunzi 120 ambao wanahudhuria kikamilifu na kwamba waliobaki 72 wana mahudhurio hafifu.

Mwalimu Idosa anasema umaskini ndio sababu kubwa ya watoto wengi hasa wa kike kuacha shule. “…tumejitahidi kwa kila njia walau sasa hivi unaona kuna wanafunzi hao unaowaona,’’ anaeleza na kuongeza; Kwa kweli hali ni mbaya, ndio hapa nasukumana na wazazi tusaidiane ili wanafunzi hawa waweze wamalize shule.’’

Hali ilivyo Bahi

Utoro ni tatizo katika shule nyingi za Bahi. Katika Shule ya Sekondari Magaga, ni wasichana wawili tu ndio wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, kati ya saba walioanza kidato cha kwanza mwaka 2014.

“Tulikuwa saba darasani, wenzetu wengine waliishia njiani lakini sisi wawili tumesalimika. Sio kwamba hatukukutana na miiba, tulikutana nayo sana ila tunahitimu kwa neema ya Mungu,”anasema Mlekwa Matonya, mmoja wa wasichana hao.

Miba anayoizungumzia Mlekwa ni vishawishi kutoka kwa wanaume kwa sababu anakabiliwa na ugumu wa maisha, kutokana na kipato kidogo cha familia yake na wakati huo huo, amepanga chumba cha bei naafuu anakoishi peke yake.

Katika Shule ya Sekondari ya Bahi, kati ya wanafunzi 64 walioanza kidato cha kwanza miaka minne iliyopita ni 24 pekee ndio wanaotarajiwa kumaliza, huku 40 wakiwa wameishia njiani.

Tatizo la utoro liko hata katika shule za msingi. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chifuduka, Daniel Mchomvu anasema kama isingekuwa ukali, madarasa ya shule hiyo yangekuwa matupu.

“Tulilazimika kuwa wakali, hatukuwa na mzaha kwenye suala la utoro hivyo wazazi wakaanza kuogopa na kulazimika kuleta watoto wao shuleni,” anasema.

Vifungu namba 35 (1), (2) na (3) vya Sheria ya Elimu ya 1978 na marekebisho yake vinawalazimisha wazazi kuwaandishikisha watoto wao darasa la kwanza, baada ya kufikisha miaka saba na kuhakikisha wanahudhuria masomo ya elimu ya msingi.

Sheria hiyo inampa wajibu mwanafunzi yeyote aliyeandikishwa kwa ajili ya masomo kuhakikisha anahudhuria shuleni bila kukosa hadi atakapohitimu elimu husika.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chifuduka, Gasper Mhembano, anasema amekuwa akiwahimiza wazazi kusimamia mahudhurio ya watoto wao na kwamba wale wanaoonyesha ukaidi hushitakiwa.

Hata hivyo, anasema usimamizi wa sheria unakabiliwa na changamoto ya kutokuwapo kwa mahakama.

“Kutoka hapa hadi mjini ni kilometa 130 na usafiri ni duni hivyo wakati mwingine tunakosa jawabu,”anasema.

Ofisa elimu wa Sekondari Bahi, Hassan Mohamed anakiri kuwa utoro ni mzigo mkubwa kwa wilaya hiyo.

“Tulishawaagiza watendaji wa vijiji na kata kuchukua hatua kali za kisheria, ikiwamo kukamatwa na kupelekwa mahakamani wazazi wenye watoto watoro,”anasema.

Sababu za utoro

Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 inataja sababu za utoro kuwa ni umbali wa kutembea kwenda shuleni na kurudi, ujauzito, ndoa za utotoni, ajira za watoto, utoro, umaskini, kukosekana kwa mahitaji maalumu shuleni kwa baadhi ya wanafunzi na baadhi ya mila na desturi zinazokinzana na utoaji wa elimu kwa watoto wa kike.

Mkazi wa kijiji cha Zegere, Sebena Julius aliyeacha masomo kutokana na umbali kutoka kijijini kwake hadi shule ya sekondari ya Chikopelo alikokuwa akisoma anasema: “Nilikuwa natembea mbali na miguu inavimba, nikaamua kuacha shule nipo tu nyumbani”.

Mwingine ni Felista Martine wa kijiji cha Chali Igongo ambaye alisema umaskini ndio unaowasumbua wazazi wengi.

“Mwanangu alipofaulu niliugua kwa sababu sina kitu, nilihangaika nikapata mahitaji yake muhimu na japo anaendelea na shule, ila sijui kama atamaliza,”anasema Felista ambaye analea familia peke baada ya kutelekezwa na mumewe.

Mkazi wa Kijiji cha Isanga, Fadhil Wilfred aliitaja sababu nyingine ya utoro kuwa ni kukosekana kwa mwamko wa elimu miongoni mwa wananchi wa Bahi, akisema baadhi ya wazazi hufurahia watoto wao wa kike kuacha shule ili wapate mahari pale wanapoolewa.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu anasema moja ya kazi kubwa walizonayo ni kupambana na utoro.

“Kuna wakati tunatafuta vijana wasomi wa kuwaajiri kutoka kwenye hii wilaya tunashindwa, tatizo ni utoro. Kila siku huwa nawaambia mpaka lini watoto wenu watabaki bila elimu?”anasema.

Ni tatizo la kitaifa

Sio Bahi pekee, tatizo la utoro limetamalaki katika shule nyingi za umma nchini.

Kwa mfano, takwimu za msingi za elimu Tanzania (Best) zilizotolewa na Tamisemi Disemba 2016, zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 61,488 walioacha masomo, utoro unachukua asilimia 93.2 wakati mimba ni asilimia 5.6. Wanafunzi waliacha masomo kwa utoro asilimia 42.4 ni wasichana ikilinganishwa na wavulana ambao ni 51.5.