UCHAMBUZI: Mapenzi kwa kadi za posta yalivyopotea

Tuesday January 28 2020

 

By Rainer Ebert

Kabla ya kuja kwa mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Instagram, kulikuwa na kadi za posta.

Vijana waliozaliwa miaka ya hivi karibuni huenda hawajawahi kutumia njia hii kwa mtu yeyote yule.

Siku hizi mawasiliano ni ya haraka, na kadi za barua zinaonekana kupitwa na wakati, wakati mwingine jamii kubwa ya kidijitali huuita mfumo huu “konokono”.

Tangu kadi ya posta ya kwanza ya picha itumwe kwa mwandishi wa London-Theodore Hook mwaka 1840, kadi ya posta imepata umaarufu mkubwa kwa kuwa njia kuu ya kutumiana picha na kushirikishana mawazo na tamaduni mbalimbali kutoka maeneo tofauti.

Katika siku za hivi karibuni, umaarufu huo umepungua kwa sababu ya simu za rununu na mitandao ya kijamii.

Nyakati hizi kutuma kadi za posta huchukua muda mrefu na nguvu nyingi kuliko kutuma baruapepe au ujumbe kwenye mitandao ya kijamii.

Advertisement

Kutuma kadi ya posta kunahitaji utulivu na umakini mkubwa na kupokea kadi moja tu huleta hisia fulani kuliko kupokea ujumbe kwenye kifaa cha kielektroniki.

Kadi ya posta inashikika na ni kuponi inayojidhihirisha, cha ajabu zaidi ni kujua kuwa kipande cha karatasi ulichoshikilia mikononi mwako kilisafiri umbali mrefu na kupitia mikono ya watu wengi ili kukufikishia ujumbe wa mtu mwingine.

Mitandao ya kijamii hupendwa na mara nyingi hupewa kipaumbele. Kuandika barua posta kwa mtu ni zoezi la uvumilivu, uangalifu, na linalodhiirisha kuwa unajali sana.

Mwaka 2005, mapenzi kwa kadi za posta yalionyeshwa na mwanafunzi wa chuo kikuu kimoja kutoka Ureno, Paul Magalhães, kadi zilimfanya kuanzisha mradi wa utumaji wa kadi unaovuka mipaka. Mradi huu ni jukwaa la mtandao linalowaunganisha watu kutoka kote ulimwenguni.

Mbinu ni rahisi: kwa kila kadi ya posta utakayotuma, utapokea kadi nyingine ya posta. Mtu yeyote anaweza kujiunga, bila kujali umri, jinsia, rangi, au imani.

Ikiwa unataka kujiunga na kuwa mwanachama katika mradi huu, unachotakiwa kufanya ni kwenda kwenye tovuti ya www.postcrossing.com na kuunda akaunti.

Mara baada ya kuwa na akaunti, unaweza kuomba kutuma kadi ya posta. Tovuti itakupatia anwani ya mtu usiyemfahamu pamoja na namba ya utambulisho ya kadi ya posta. Kisha utatuma kadi ya posta kwa anwani hiyo.

Kadri kadi itakavyokuwa ya kirafiki na ya heshima, unaweza kuandika chochote unachopenda.

Unaweza kutuma kitu cha kuvutia kutoka sehemu unayoishi, tukio kutoka katika maisha yako, au shairi uliloandika.

Mpokeaji wa kadi yako ya posta atatumia namba ya utambulisho kusajili kadi ya posta kwenye tovuti mara tu atakapoipokea.

Halafu utaarifiwa kuwa kadi yako ya posta imemfikia kisha mtu mwingine atakutumia kadi ya posta.

Hivi sasa, tovuti hii ina watu karibu 800,000 wanaotumia barua pepe. Hadi sasa wametumiana zaidi ya kadi milioni 55, katika umbali wa kilomita 280,683,219,245 kwa pamoja.

Kama tovuti inavyoeleza, umbali huo ni sawa na safari 7,003,948 za kuzunguka dunia au safari 365,089 kwenda na kurudi mwezini au safari 938 za kwenda na kurudi kwenye jua, ndivyo ambavyo maelfu ya kadi za posta zinavyosafiri.

Watumiaji zaidi ya 3,000 wa kadi za posta katika Afrika wanaishi Afrika Kusini huku 19 tu wakitoka Tanzania.

Kwa ujumla, zaidi ya kadi 750 zimetumwa kutoka Tanzania. Idadi hiyo inaiweka Tanzania katika nafasi ya 133 kati ya nchi 248 zinazotumia mfumo huo.

Nilizungumza na Watanzania wawili ambao ni watumiaji wa mfumo huo juu ya matarajio yao. Wilson ambaye ni mkulima mwenye miaka 28 kutoka Bagamoyo, alijifunza juu ya mfumo wa utumaji wa kadi za posta kuvuka mipaka kutoka kwa rafiki yake wa Ujerumani.

Aliamua kujiunga na kuungana na watu wengine kujifunza juu ya maisha kutoka sehemu nyingine za dunia, kama njia ya kuitangaza nchi yake na tamaduni zake.

Mwingine ni Harrison mwenye umri wa miaka 32. Ni mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya habari ambaye anaishi jijini Arusha. Amekuwa akiandika barua tangu utotoni, akianza na barua aliyomwandikia baba yake mwaka 2001, na alifurahi pale aliposikia kuhusu kadi za posta kutoka kwa rafiki yake wa Facebook.

Kwake yeye mfumo huu ni njia ya kupata marafiki wa kalamu. Wilson na Harrison wameambiwa na marafiki kuwa kujihusisha na kadi za posta ni kupoteza pesa, ila hilo halijawazuia.

Furaha ya kupata kadi ya posta katika sanduku la posta ni nzuri sana na ya thamani kama ilivyo kwa mambo mengine.

Mfumo huu unawaleta watu kutoka asili tofauti pamoja na kukuza uelewa wa kitamaduni na urafiki, na huleta tabasamu kila kona ya ulimwengu.

Dk Rainer Ebert ni mwanachama wa kituo cha Maadili ya Wanyama cha Oxford. wavuti www.rainerebert.com