‘Diamond unazungumza na sisi au na Harmonize?’

Inawezekana kinachozungumzwa na wengi kuwa Mkurugenzi wa lebo ya WCB, Diamond Platnumz hajapendezwa na kuondoka Harmonize kuondoka kwenye lebo hiyo kuna ukweli.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na minong’ono kuwa wawili hao hawapo karibu na hawana mawasiliano kabisa hasa baada ya Harmonize ambaye Diamond alimkuza kisanii kuomba kujitoa kwenye lebo hiyo, akionekana kama hana shukurani baada ya mambo yote aliyofanyiwa ikiwamo kukuzwa kisanii lakini ameamua kutemana nao.

Kauli hiyo imeonekana ina mashiko kutokana na kile kilichosemwa na Diamond mara baada ya kukabidhiwa ubalozi wa kampuni ya Bomet inayozalisha sabuni ya unga ya Niceone, kuwataka vijana wakumbuke walikotoka.

“Kijana kumbuka sehemu uliyotoka na kumbuka na kuwaheshimu watu waliokuwezesha, mimi nisingeweza kufika hapa bila mameneja wangu na Watanzania ambao ni mashabiki wangu, nitaendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwapenda,”

“Naamini kila kijana ameandikiwa fungu lake kwenye maisha na hakuna mtu anaweza kukushusha au kukuzibia riziki yako cha muhimu ni kufanya kazi na kumuomba sana Mungu,” alisema.

Licha ya kutomtaja mtu, kauli hiyo ilizua minong’ono kuwa inawezekana anamfikishia ujumbe huo Harmonize.

Ikihusishwa na mchuano kati yao unaoendelea mtandaoni ambapo Septemba 22, 2019 zilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha Diamond akiwa Uwanja wa Taifa wakati wa uzinduzi wa tamasha la utamaduni la Afrika Mashariki (Jamafest), akionekana kazungukwa na vijana wengi wakimshangilia na kumwimbia.

Kesho yake Harmonize naye akaweka video inayomuonyesha akiwa kwenye uwanja huo siku ya mechi ya Taifa Stars na Burundi, ambapo naye alizungukwa na kundi la vijana kama ilivyokuwa kwa bosi wake wa zamani.

Mbali na hayo Diamond aliwakumbusha vijana kuwa ili kufikia mafanikio kama yake wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii.

“Unaweza kuniangalia ukanichukulia poa, nitolee mfano jana kuanzia asubuhi nilikuwa narekodi video hadi asubuhi ya leo, nimejiegesha saa chache nagongewa mlango niende kwenye miadi ubalozini, nimetoka huko safari ya kuja hapa Kilimanjaro Hoteli ikaanza unaweza kuona ni jinsi gani natumia muda mwingi kufanya kazi,”

“Kwangu muda huu wa ujana ndiyo wa kufanya haya ninayoyafanya, hivyo kijana yeyote anayependa muziki na anatamani kuwa na mafanikio kama mimi akubali kulala uzeeni, kupumzika uzeeni,” alisema Diamond.

Alisema mafanikio hayaangalii kazi, hivyo vijana popote pale walipo bila kujali wanafanya kazi gani, wasikubali kuchoka kabla hawajafanikiwa.