El Maamry: Nateseka kitandani, siachi kuifuatilia Stars

Tuesday September 10 2019

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Said El Maamry akiwa nyumbani kwake maeneo ya Daraja la Salenda jijini Dar es Salaam. Picha na Hellen Hertley 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Ni zaidi ya miezi 36 sasa, Said Hamad El Maamry yuko kwenye maumivu makali akisumbuliwa na maradhi ya kifua, shingo na mkono wa kulia kushindwa kufanya kazi, lakini anasema hali hiyo haijamfanya ashindwe kufuatilia mwenendo wa timu ya Taifa, Taifa Stars.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania, FAT (sasa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF) anaanza kuichambua Stars huku akizitaja timu kongwe za soka, Simba na Yanga kuwa na nafasi kubwa ya kuijenga au kuibomoa Stars.

El Maamry ambaye mwaka 1973 kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa FAT katika uchaguzi mkuu uliofanyika Tanga anasema licha ya maradhi yanayomkabili sasa bado ana mapenzi na soka, achilia mbali elimu na ujuzi aliona juu ya mchezo huo.

“Bahati mbaya tu maradhi ndiyo yamechangia nisiweze kwenda uwanjani kushuhudia mechi laivu, lakini sijawahi kuacha kufuatilia kila kinachoendelea hivi sasa,” anasimulia El Maamry katika mahojiano na gazeti hili nyumbani kwake Daraja la Selander, Dar es Salaam hivi karibuni.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa FAT anasema katika soka la Tanzania timu za Simba na Yanga zina nafasi kubwa ya kuijenga au kuibomoa Taifa Stars katika ushindani.

“Utulivu wa timu hizi mbili una faida kubwa katika soka la Tanzania, Simba au Yanga mojawapo ikikosa utulivu, basi upepo ule unaweza kuingia hadi kwenye timu ya Taifa,”.

Advertisement

Anasema hata ikitokea mgogoro kati ya TFF na Yanga au Simba, au mgogoro wa Simba na Yanga, au wa uongozi ndani ya mojawapo ya klabu hizo, unaweza kuathiri pia mwenendo wa timu ya Taifa.

“Simba na Yanga ni timu ambazo zina nguvu ya mashabiki na hata viongozi wa mpira kwa vyovyote vile lazima utakuta wana mapenzi na mojawapo ya hizi timu, hata mimi nilikuwa hivyo, lakini ukifanya kazi kwa mapenzi, lazima ufeli.

“Utaibua tu migogoro, kiongozi wa Shirikisho hapaswi kuonyesha mapenzi ya wazi wazi kwa timu moja na kuikandamiza nyingine, lazima utazigawa hizi timu na upepo huo utakwenda hadi kwenye timu ya Taifa,” anasema.

Anasema hata mgogoro wa klabu hizo mbili au mgogoro wa ndani ya klabu, unachangia kwa asilimia kubwa kuwakosesha utulivu hadi wachezaji, hivyo upepo huo utaiathiri pia timu ya Taifa kwani timu hizo mbili zimekuwa zikitoa idadi kubwa ya wachezaji wa Stars.

Kiongozi huyo aliyewahi kuwa mjumbe wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwaka 1980 hadi 1986 kabla ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa heshima mwaka 1998, anasema nafasi ya Stars kufanya vizuri kimataifa ipo kama kukiwa na mipango madhubuti.

“Nakumbuka nikiwa mwenyekiti wa FAT na mjumbe wa CAF, tulikuwa na mipango mikakati ya muda mrefu, tulikuwa tunajifunza kutoka kwa waliotutangulia na mara kwa mara tulikuwa tunatafuta mbinu gani tufanye ili soka letu lifanikiwe,” anasema.

El Maamry ambaye aliiongoza Stars kucheza fainali ya Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 1980, anasema bado Stars ina safari ndefu katika harakati za kufuzu kucheza Kombe la Dunia.

“Naiona nafasi ya Tanzania kufuzu Chan msimu huu, lakini kwenye Kombe la Dunia bado tuna safari ndefu, tunahitaji sapoti ya pamoja ili kujaribu kufika huko.

“Kwa kuwa tumeanza kujaribu kurudi katika ramani ya soka Afrika, tujipange kwa kuwekeza kwa vijana, miundombinu, vifaa, tuwe na ligi bora, wachezaji wetu wengi watoke wakacheze soka la kulipwa, tutafika,” anasema.

El Maamry pia amegusia nafasi ya timu za Yanga, Azam na Malindi ya Zanzibar ambazo zinaiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Shirikisho.

“Japo ni ngumu hasa kwa mashabiki wa Simba na Yanga kupeana sapoti kimataifa, lakini tunapaswa kuachana na kasumba ya kusapoti timu za nje zinapokuja kucheza aidha na Simba au Yanga, mfano kipindi hiki, mashabiki wote tungeungana kuisapoti Yanga, Azam na Malindi.

“Kwa kufanya hivi kungeongeza hamasa kwa wachezaji wetu, tofauti na sasa ambapo tunafahamu ubora wa Yanga, Azam na hata Malindi hivyo tulipaswa tuzipe sapoti ya uzalendo ili zipambane, lakini si kuzibeza hasa Yanga tena baadhi ya mashabiki wakiombea itolewe ili wafanane,” anasema.

Maradhi yamuengua CAF

Mwaka 1998 CAF walimteua El Maamry kuwa mjumbe wa heshima wa Shirikisho hilo la soka Afrika, nafasi ambayo anasema ameshindwa kuitendea haki ipasavyo miaka ya hivi karibuni kutokana na maradhi ambayo yanamsumbua kwa miaka mitatu sasa.

Licha ya kuonyesha kujikaza, lakini kiongozi huyo ambaye kitaaluma ni Mwanasheria anasema amekuwa akisumbuliwa na kifua, shingo kuvimba na mkono wa kulia kutofanya kazi.

“Alianza kuumwa mwanzoni mwa mwaka 2017, licha ya umri kusogea, lakini pia majukumu aliyofanya akiwa CAF, BMT (Baraza la Michezo la Taifa), Polisi na Tume ya mabadiliko ya katiba akiwa mjumbe yalimchosha,” anasema mmoja wa watoto wake, Ahmad El Maamry.

Anasema baba yao alijitoa sana katika majukumu ya kitaifa ikiwamo kuhudhuria mikutano ya CAF mara kadhaa, japo sasa hawezi tena kutokana na ugonjwa.

Huku akionyesha kusikitika, El Maamry mwenye miaka 84, anasema marafiki zake wamekuwa wakimtembelea na kumpa pole japo anahisi kama anawasumbua anataka kuwaondoa wasiwasi afya yake siyo mbaya na anaamini itaimarika na atakuwa sawa pamoja na mkewe (Naima) ambaye ni mgonjwa kwa miaka 10 sasa.

“Tuko katika harakati za kumpeleka mzee na mama India kwa matibabu zaidi, tunaamini watakuwa sawa baada ya matibabu kule,” anasema Ahmad ambaye ndiye anasimamia ofisi ya sheria ya baba yake iliyopo Posta, Dar es Salaam.

Ammwagia sifa JPM

El Maamry ambaye awahi kukaririwa na gazeti hili hivi karibuni akieleza kutamani kuzungumza na rais John Pombe Magufuli (JPM) kabla Mungu hajamchukua, anasema Watanzania hawakukosea kumchagua Magufuli kuwa rais wao.

“Nchi imepata mtu, hakuna ‘blah blah’ katika utendaji, mambo yanafanyika yanaonekana, pia ni rais ambaye anapenda soka hivyo anapaswa kuungwa mkono kwa timu kupata matokeo mazuri ili soka la Tanzania lifike mbali kimataifa,”

Alivyoondoshwa FAT

Mwaka 1976 Waziri wa Michezo, Mirisho Sarakikya alivunja Kamati ya Utendaji ya FAT iliyoongozwa na El Maamry kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utawala mbovu, akambakisha madarakani Katibu Mkuu, Hassan Chabanga Dyamwalle (sasa ni marehemu).

Ilikuwa Jumamosi ambapo Stars ilikuwa na mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Nigeria ikiwa ni moja ya maandalizi ya kuwania kufuzu kucheza Fainali za Afrika ambazo zilikuwa zikifanyika Addis Ababa Ethiopia.

Aliambiwa kuanzia siku ile si Mwenyekiti tena wa FAT lakini aendelee kuwa karibu na wageni mpaka watakapoondoka na kuondoshwa FAT kwa staili hiyo.

Hata hivyo, mwaka huo huo ukafanyika uchaguzi, aliruhusiwa na serikali kugombea akashinda alikaa madarakani hadi mwaka 1986 alipoondoshwa akiwa kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Mexico ambako alialikwa, aliporejea akapigwa marufuku kugombea baada ya mchujo wa wagombea kufanywa akiwa nje ya nchi.

Uchaguzi mkuu wa FAT ulifanyika Mbeya ambapo Mwenyekiti hakupatikana hivyo Makamu Mwenyekiti Mbeyela akakaimu nafasi ya Mwenyekiti hadi mwaka 1989 alipochaguliwa Mohamed Mussa kuwa mwenyekiti aliongoza FAT hadi mwaka 1992 huku El Maamry akabaki kuwa Mjumbe wa Heshima wa CAF tangu alipoteuliwa mwaka 1998.

Advertisement