Mambo 10 kuchomoza Ligi Kuu Bara

Pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/2020 limefunguliwa rasmi juzi Jumamosi kwa mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya Simba na Azam uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ligi hiyo itachezwa kwa takribani miezi 10 kusaka bingwa ambaye ataiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo wakitwaa mara mbili mfululizo kombe hilo msimu wa 2017/2018 na ule uliopita wa 2018/2019.

Kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni mwanzo wa mtiririko wa matukio mbalimbali ya kufurahisha, kusikitisha na ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kuacha historia ya kipekee.

Spoti Mikiki inakuletea baadhi ya mambo ambayo kuna uwezekano mkubwa yakatokea katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020.

1.Ubingwa Simba au Yanga

Kuna uwezekano mkubwa, taji la Ligi Kuu Tanzania Bara likaendelea kuzunguka katika eneo la Kariakoo kwa kuchukuliwa ama na mabingwa watetezi Simba au Yanga kutokana na utofauti mkubwa wa kiubora wa wachezaji, maandalizi na huduma ambazo kila timu imekuwa ikipata.

Timu hizo zimesajili wachezaji wa kiwango cha juu wale wa kigeni na wazawa, zimekuwa na kambi za maandalizi za hadhi ya juu zinatoa huduma nzuri kwa wachezaji wao kwa maana ya malazi na matibabu, pia zina mtaji mkubwa wa mashabiki.

Azam inaonekana ni mpinzani wao mkubwa lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya wachezaji wake kushindwa kuziamua mechi ngumu ambazo huwa zinachangia ipoteze pointi na kuzinufaisha Yanga na Simba.

2. Viporo vya Mechi

Bodi ya Ligi Kuu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa nyakati tofauti walitoa ahadi kuwa Ligi Kuu msimu huu haitakuwa na viporo kutokana na ratiba yake kupangwa kwa kuzingatia kalenda ya mashindano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu na timu za taifa.

Hata hivyo, kabla hata ligi haijaanza, ratiba hiyo ilipanguliwa kutokana na timu nne za Tanzania Bara zinazowakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa, kupangwa kuanzia hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Ratiba hiyo imepanguliwa kabla ligi haijaanza na ikiwa timu hizo zitafanikiwa kusonga mbele katika hatua zinazofuata za mashindano hayo pamoja na kubana kwa ratiba ya mashindano mengine kama vile Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi na SportPesa, ni wazi viporo havitakosekana.

3.Wageni Kutamba Ufungaji

Kwa misimu miwili mfululizo iliyopita, nyota wawili tofauti wa kigeni wameibuka wafungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Msimu wa 2017/2018, Mfungaji Bora alikuwa ni Emmanuel Okwi na msimu uliopia, aliyeibuka mshindi alikuwa ni Meddie Kagere.

Kundi kubwa la washamubuliaji wazawa limeonekana kushindwa kuonyesha kiwango bora cha kufumania nyavu katika siku za hivi karibuni na hilo linaweza kuwa chachu kwa wageni kuwafunika tena.

4.Vita ya Namba

Idadi kubwa ya timu zimesajili wachezaji wenye ubora ambao unaelekea kufanana jambo ambalo litawapa wakati mgumu makocha wao katika upangaji wa kikosi cha kwanza.

Kwa upande wa klabu, vita hiyo ya namba itakuwa na faida kwani itamfanya kila mchezaji ajitume ili aweze kufanya vizuri ajihakikishie nafasi kikosini.

5.Namungo, Polisi Tanzania

Polisi Tanzania na Namungo FC ndio timu ambazo zinashiriki ligi hiyo zikiwa zimetoka kupanda daraja kwenye msimu uliopita.

Kila mmoja imeonekana kupania kufanya vizuri kwenye ligi kwa kuimarisha vikosi vya kwa kusajili wachezaji wazuri huku pia wakiimarisha mabenchi yao ya ufundi sambamba na kuingia kambini mapema kwa ajili ya programu za kiufundi.

Haitakuwa jambo la ajabu kuona Namungo FC na Polisi Tanzania zikiwa sio miongoni mwa timu zinazopigania kushuka daraja na kwa namna zinavyojiandaa zinaweza kuwa miongoni mwa timu zitakazofanya vizuri.

6.Manula, Shikalo

Kwa misimu mitatu mfululizo, Aishi Manula alifanikiwa kutwaa tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kiwango bora ambacho alikuwa akikionyesha lakini kuna uwezekano mkubwa awamu hii mambo yakawa tofauti.

Uhodari wa makipa wawili wa KMC, Juma Kaseja na Jonathan Nahimana, ujio a kipa Farouk Shikalo kwenye kikosi cha Yanga na usajili wa kipa Beno Kakolanya uliofanywa na Simba, unamuweka katika wakati mgumu Manula kuendeleza ubabe wake.

7. Kung’ara kwa Bocco

John Bocco ndiye mchezaji mzawa ambaye amekuwa na mwendelezo mzuri wa kufumania nyavu ambapo katika misimu minne mfululizo amekuwa akifunga zaidi ya mabao 10 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Aina ya usajili ambao Simba imeufanya msimu huu kwa kusajili kundi kubwa la wachezaji wenye uwezo wa kuchezesha timu na kupiga pasi za mwisho, unaweza kumnufaisha Bocco na kumfanya aendeleze makali yake msimu ujao.

8.Ligi bila Kavila

George Kavila ameitumikia Ligi Kuu Tanzania Bara kwa miaka takribani 21 tangu alipoanza kucheza mnamo mwaka 1998, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na mchezaji mwingine yoyote.

Hata hivyo kiungo huyo msimu ujao hataonekana uwanjani baada ya kuamua kutandika daluga baada ya kuitumikia Kagera Sugar msimu uliopita.

9. Uchakavu wa Viwanja

Changamoto ya uchakavu na ubovu wa viwanja vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wadau wa mpira wa miguu nchini na haionekani kama inaweza kumalizwa katika miaka ya hivi karibuni.

Pamoja na Bodi ya Ligi Kuu kupanga kuvifanyia ukaguzi viwanja hivyo, kuna uwezekano mkubwa vikaendelea kubaki na hali hiyo huku vikiwa vinatumika kwennye ligi kwa sababu wamiliki wake wanaonekana kutokuwa tayari kuvitafutia tiba ya kudumu.

10. Utemi Dar es Salaam

Uzoefu wa kushiriki mashindano ya kimataifa na nguvu ya kiuchumi ambayo timu za jiji la Dar es Salaam zimekuwa navyo, ni wazi kwamba vitakuwa chachu kwa timu za KMC, Yanga, Azam na Simba kuendelea kutikisa na zina nafasi kubwa ya kumaliza katika nafasi nne za juu kwa mara nyingine kama ilivyokuwa msimu uliopita.