Man City yampa raha Guardiola

Tuesday August 13 2019

 

Licha ya Pep Guardiola kumuita Raheem Sterling ‘mtu maalumu’, kocha huyo amesifu kazi nzuri ya wachezaji wote wa Manchester City.

Guardiola alitoa kauli hiyo baada ya Man City kupata ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya West Ham United katika mchezo wa Ligi Kuu England msimu huu.

Sterling alifunga mabao matatu katika mchezo huo akionyesha kiwango bora na kuanza vyema kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu.

Tangu kuanza mechi za maandalizi ya msimu mpya, mshambuliaji huyo wa England, amecheza vyema na kocha huyo amemtaja ni mchezaji wa aina yake Man City.

Sterling amefunga mabao matano katika mechi za maandalizi ya msimu mpya akionyesha ubora wake.

“Wachezaji wote wamecheza kwa kiwango bora, wameonyesha namna ambavyo tumenza msimu mpya kwa kishindo,” alisema Guardiola.

Advertisement

Nahodha wa zamani wa England, Alan Shearer, amemtaja Sterling ni mchezaji mwenye kiwango bora.

“Anapopata nafasi ya kufunga ndani ya eneo la hatari hawezi kukuacha lazima atakufunga tu. Ni mchezaji mwenye kujiamini, anajituma,” alisema Shearer.

Guardiola alisema Sterling hawezi kuwa mchezaji bora kama wachezaji wenzake hawatampa nafasi ya kuonyesha kiwango chake.

‘Kipindi cha kwanza walicheza vizuri, lakini kwa ujumla wake timu nzima ilionyesha dhamira ya kutaka matokeo mazuri,” alisema kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

Guardiola alisema ana wachezaji wenye kiwango bora ambao wana sifa ya kuitumikia Man City.

Advertisement