Man United yamtengea dau nono Alderweireld

Thursday May 17 2018

 

Manchester, England.Manchester United inajiandaa kupeleka ofa ya Pauni 40 milioni kwa Tottenham ili kumnasa beki Toby Alderweireld kwa lengo la kuimarisha safu yake ya ulinzi, ambayo huenda ikaondokewa na nyota kadhaa wanaoonekana kutomridhisha kocha Jose Mourinho.

Mourinho ametajwa kuwa kwenye mpango wa kufanya mabadiliko kadhaa kwenye safu yake ya ulinzi ikidaiwa yuko mbioni kuwatema Daley Blind, Luke Shaw na Phil Jones na kuleta nyota wapya, ambao wataimarisha ukuta wa timu hiyo na anaamini kumpata Alderweireld kutasaidia kutimiza hilo.

Hamu ya Man United kumtengea dau beki huyo anayeweza pia kucheza kama kiungo mkabaji, imekuja baada ya kuwepo taarifa kwamba klabu yake iko mbioni kumruhusu aondoke kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayonolewa na Mauricio Pochettino.

Inatajwa kuwa Spurs inataka kumuuza Alderweireld kwa dau hilo ili ipate fedha zitakazoiwezesha kumsajili nyota wa Ajax Amsterdam, Matthijs de Ligt ambaye klabu yake imemuweka sokoni kwa dau la Pauni 50 milioni. Hata hivyo, Manchester United wanapaswa kutumia nguvu kubwa kumshawishi beki huyo ajiunge nao kwani amekuwa akinyatiwa na klabu nyingine kubwa kama Barcelona, Chelsea na PSG.

Advertisement