Messi afichua siri nzito kuondoka Barcelona

Madrid, Hispania. Lionel Messi ametamka kwa mara ya kwanza alitaka kuondoka Barcelona kutokana na sakata la ukwepaji kodi.

Nahodha huyo wa Barcelona alisema kitendo cha kudaiwa na Serikali amekwepa kodi ya Pauni2.95 milioni kilimuweka njiapanda.

Messi alipigwa faini ya Pauni 223,000 kwa kosa hilo ambalo alisema lilitaka kuharibu maisha yake Nou Camp mwaka 2017.

Hata hivyo, alisema anashukuru kashfa hiyo ilimkumba wakati watoto wake wakiwa na umri mdogo.

“Nilitaka kuondoka si Barcelona tu nilitaka kuihama Hispania. Nilidhani sikutendewa haki na sikutaka kuendelea kuishi hapa,” alisema Messi.

Mshambuliaji huyo alisema alikuwa na wakati mgumu yeye na familia yake kwa kuwa kashfa hiyo ilikuwa kubwa kwake.

Tangu alipojiunga na Barcelona Novemba 2003, amefunga mabao 604 katika mechi 692 alizocheza Barcelona.