Mikataba mifupi inapogeuka kikwazo

Tuesday June 25 2019

 

By Charles Abel, Mwananchi [email protected]

Harakati za timu mbalimbali za Ligi Kuu kuimarisha vikosi vyao katika kipindi hiki cha dirisha kubwa la usajili zinaendelea kwa kasi ambapo kila moja imekuwa kwenye mikakati ya kunasa wachezaji wazuri ambao watakuwa msaada msimu ujao.

Mabenchi ya ufundi kwa kushirikiana na viongozi wa timu mbalimbali wanaendelea kuimarisha vikosi vyao kwa kunasa wachezaji wa nafasi mbalimbali ambao wanaamini watasaidia kuongeza ufanisi wa vikosi vyao huku pia ikiachana na nyota ambao walionekana hawana msaada kikosini kwenye msimu uliomalizika.

Lakini ukiondoa timu, wachezaji wenyewe nao wamekuwa wakitengeneza mazingira ya kupata vitita vya fedha kutokana na uhamisho wa kutoka timu moja hadi nyingine iwe kwa kujiunga kama wachezaji huru, kwa mkopo au kuuzwa.

Dirisha la usajili hasa kubwa kama hili la sasa linaweza kuwa na neema kwa timu iwapo itafanikiwa kupata wachezaji wazuri lakini linaweza kuacha kilio na majonzi kwa timu hasa pale inapowapoteza wachezaji muhimu.

Kwa bahati mbaya idadi kubwa ya wachezaji ambao wamekuwa wakivunwa na timu nyingine na kupelekea kuziacha kwenye wakati mgumu timu zao ni wale ambao walitia saini mkataba wa muda mfupi kama vile wa msimu mmoja kwenye mikataba yao ya awali jambo linalowaweka katika nafasi na fursa nzuri ya kutafuta malisho mazuri zaidi.

Kutokana na idadi kubwa ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu kuwa na hali ngumu kiuchumi kulinganisha nna klabu chache kama Simba, Yanga na Azam, zimekuwa zikijikuta kwenye wakati mgumu wa kuwabakiza mastaa wake ambao mikataba yao inakuwa imemalizika.

Advertisement

Na hii upelekea kuziumiza timu kama hizo kwa sababu zenyewe mbali na kukosa ushawishi wa kuwabakisha wachezaji wake ambao mikataba imemalizika lakini zinakabiliwa na changamoto nyingine ambayo ni kusajili wachezaji wa kuziba nafasi za wachezaji ambao wametimkia kwingine.

Spoti Mikiki inakuangazia baadhi ya klabu ambazo zimetikiswa kwenye dirisha hili la usajili kwa kukimbiwa kirahisi na wachezaji ambao ziliwasainisha mikataba ya msimu mmoja ambayo ilimalizika mwishoni mwa msimu.

Lipuli

Kama kuna timu ambazo zinateseka kipindi hiki cha usajili kwa kupoteza kirahisi nyota wake walioamua kutimkia kwingine mara baada ya mikataba yao ya kumalizika basi miongoni mwao ni Lipuli FC.

Sehemu kubwa ya kikosi cha kwanza cha Lipuli kitaparaganyika kwenye kipindi hiki lakini laiti kama wangewasajili wachezaji wao kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja leo wasingekutana na changamoto hii.

Beki Paul Ngalema amejiunga na Namungo FC, Miraji Athumani amesajiliwa na Simba huku Ally Mtoni akihusishwa na Yanga.

Ukiondoa hao, wachezaji wengine wote kila mmoja alitia saini mkataba wa mwaka mmoja na Lipuli ambao umemalizika na wako huru kwenda kokote kule bila bughudha.

Azam

Matajiri wa Azam FC nusura ampoteze mshambuliaji Obrey Chirwa baada ya mkataba wa awali wa mwaka mmoja kumalizika. Hata hivyo Chirwa baadaye alitia saini.

Laiti Azam wangemsainisha Chirwa mkataba wa miaka miwili na zaidi pindi walipomnasa, leo wasingepata taabu ya kumshawishi kubaki.

Mbao FC

Timu hiyo ya mkoani Mwanza iko kwenye hatari ya kuwapoteza wachezaji Amos Charles, Rafael Siame, Said Khamis, Athanas Pastory na Erick Mulilo ambao wako huru kujiunga na timu nyingine.

Ndanda FC

Moja ya timu ambazo zimekuwa na tabia ya kupenda kutoa mkataba wa mwaka mmoja kwa mchezaji ni Ndanda FC jambo ambalo limekuwa likiifanya kila wakati wa dirisha la usajili kuanza upya.

Klabu hiyo ipo kwenye wakati mgumu wa kuwapoteza Kigi Makasi, Emmanuel Memba, Vitalis Mayanga, Dyeri Makonga na wengineo katika kipindi hiki cha dirisha la usajili.

Alliance FC

Tayari imeondokewa na mshambuliaji wake Blaise Bigirimana ambaye ametimkia Namungo FC na kama isipojipanga inaweza kuwakosa kipa John Mwanda, Hussein Javu na Paul Maona ambao mikataba yao ya mwaka mmoja imeshamalizika.

Kagera Sugar

Wachezaji wao kama Edward Christopher, Ramadhani Kapera, Said Kipao, Juma Nyosso, Venance Ludovick na Japhet Makarai wanaweza kuachana na klabu hiyo ikiwa itashindwa kuwapa ofa stahiki.

Mwadui FC

Iliponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliomalizika na ililazimika kutegemea mechi za mchujo dhidi ya Geita Gold iwaokoe kubaki Ligi Kuu.

Hata hivyo wachezaji wake wengi walisaini mkataba wa mwaka mmoja na wanaweza kuondoka mfano ni mshambuliaji wake tegemeo, Salim Aiyee, nahodha Iddi Mobby na kiungo Abdallah Seseme.

Coastal Union

Wachezaji ambao wako hatarini kuwakosa ni Raidhin Hafidh, Ayoub Lyanga, Haji Ugando, Moses Kitandu na kipa Hussein Shariff ‘Casillas’

Mbeya City

Imeshampoteza Iddi Seleman ‘Nado’ ambaye ametimkia Azam FC iliyokoshwa na kiwango chake katika msimu uliopita.

Ukiondoa Nado, inaweza kuwakosa pia Mohammed Samatta na Frank Ikobelo kwani mikataba yao ya mwaka mmoja imeshamalizika.

Yanga

Wachezaji ambao iliwapa mikataba ya mwaka mmoja ambayo imeshamalizika ni pamoja na Haruna Moshi, Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko.

Tayari imeshamuongezea mkataba kipa Klauzi Kindoki baada ya ule wa awali kumalizika.

Ukiondoa wachezaji hao wa klabu mbalimbali tajwa hapo juu, nyota wengine ambao huenda wakaachana n klabu zao na kuziachia maumivu baada ya mikataba yao ya mwaka mmoja kwisha ni Adam Adam (Prisons), Juma Kaseja, Yusuph Ndikumana na Elias Maguli (KMC)

Advertisement