Mkude, Gadiel waibua mjadala

Thursday October 10 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Sakata la wachezaji wa Simba Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Gadiel Michael kuitwa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ licha ya kuondolewa ndani ya klabu yao kwa utovu wa nidhamu, limeibua mjadala.

Wakizungumza jana, wadau mbalimbali wametoa maoni tofauti kuhusu sakata la wachezaji hao ambao Kocha wa Simba Patrick Aussems amewaondoa katika kikosi chake kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Akizungumzia mkanganyiko huo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah alisema ni vyema timu ya Taifa ikaundwa na wachezaji wenye nidhamu.

“Kwa kawaida professional mwenzako anapofanyiwa vitendo vya utovu wa nidhamu, na wewe unakuwa na tahadhari na aliyemfanyia hivyo.

“Ndiyo maana makocha wa timu za taifa huulizia taarifa za wachezaji ambao wamekuwa na matatizo na klabu zao kabla ya kuwatangaza.

“Pia Stars ni timu ya Taifa na si kundi la watovu wa nidhamu. Ni vizuri kuwa na timu yenye wachezaji wanaojiheshimu si tu kwenye timu ya Taifa bali hata klabuni kwao na katika maisha ya kawaida.

Advertisement

“Paul Gasgoine aliondolewa timu ya taifa baada ya mkewe kuonekana ana michubuko iliyoelezewa kuwa ilitokana na kupigwa na mchezaji huyo. Iko mifano mingi ya wachezaji walioachwa timu ya taifa kwa sababu ya utovu wa nidhamu klabuni na katika maisha yao ya kawaida.”

Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema kitendo cha wachezaji hao kuitwa Taifa Stars ni ishara ya kubariki utovu wa nidhamu.

“Kuna mambo ambayo pengine yanaendelea lakini mchezaji mwenye utovu wa nidhamu tena imefika hatua ya klabu yake kumsimamisha hawezi kuitwa kutumika timu ya Taifa,” alisema Pluijm.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema hakukuwa na mawasiliano kati ya Aussems na Etienne Ndayiragije kujua kiini cha tatizo linalowakabili nyota hao.

“Si sahihi mchezaji mwenye utovu wa nidhamu kuitwa timu ya Taifa lakini katika hilo ni wazi kulikuwa na uhafifu wa mawasiliano,” alisema Kibadeni.

Mchambuzi Ally Mayay alisema huenda Ndayiragije ni aina ya makocha ambaye anaangalia zaidi mchango wa mchezaji uwanjani.

“Wapo makocha ambao hawayapi nafasi mambo mengine zaidi ya kuona faida ya mchezaji anayemtumia, angekuwa aina ya kocha mwingine wachezaji hao wasingeitwa timu ya Taifa,” alisema.

Katika sakata hilo yumo mchezaji wa kimataifa wa Zambia Clatous Chama ambaye pia ameondolewa katika kikosi cha Simba kwa utovu wa nidhamu.

Advertisement