Samatta atoboa siri Aston Villa England

Dar es Salaam. Mshambuliaji Mbwana Samatta amesema ana matumaini ya kufanya vyema Aston Villa kwa kuwa ni timu bora inayotengeneza nafasi za kufunga.

Akizungumza na gazeti hili jana, Samatta alisema baada ya kuona mechi ya kwanza juzi ambayo Aston Villa ilishinda mabao 2-1, ameona ina wachezaji bora wa kumtengenezea nafasi za kufunga.

Samatta alishuhudia mechi hiyo ya kwanza kwake baada ya kutia saini mkataba wa miaka minne na nusu akitokea Genk ya Ubelgiji.

Alisema mawinga wa Aston Villa hawana tofauti na wale wa Genk ambao walikuwa wakimtengenezea mabao, hivyo ana matumaini atafanya vyema Villa Park.

Samatta alisema uwezo mzuri wa kushambulia wa mabeki wa pembeni na mawinga wa Aston Villa utakuwa chachu ya kufunga mabao kama ilivyokuwa Genk alipokuwa akitengenezewa kutoka pembeni.

“Nimeona kuna wachezaji wenye kasi, nadhani tunaweza kushirikiana vyema katika kushambulia. Nimekuwa nikipenda kucheza na watu wenye kasi kwa sababu ni rahisi kwenda mbele na kushambulia kwa haraka,” alisema Samatta.

Nahodha huyo wa Taifa Stars alipokuwa Genk alifunga mabao mengi kupitia mipira ya pembeni kutokana na krosi za Junya Ito na Bryan Heynen ambaye ni kiungo aliyekuwa na uwezo wa kucheza pembeni.

Heynen ndiye aliyepiga mpira wa kona ambao Samatta alifunga bao dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao Genk ilifungwa mabao 2-1.

Kwa upande wa Aston Villa, Samatta huenda akachezeshwa na Jack Grealish mwenye mabao saba na Mahmoud Hassan (matatu) wanaoshambulia wakitokea pembeni .

Samatta anatarajia kukutana na krosi za Frederic Guilbert na Matt Targett ambao ni mabeki washambuliaji wanaotumika katika mfumo wa 3 - 4 – 3 unaopendwa na kocha Dean Smith.

Mshambuliaji huyo anatarajiwa kuiongoza Aston Villa, Januari 28 katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Leicester City kwenye Uwanja wa Villa Park. Awali, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliokuwa na kasi.