Samatta awafunika Salah, Mahrez Ulaya

Tuesday October 8 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta amesema hakuwahi kuwaza kuwa kuna siku inaweza kutokea kuwa nahodha wa KRC Genk ya Ubelgiji, inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kutoanza kwa Sebastien Dewaest ambaye ni nahodha wa KRC Genk katika kikosi cha kwanza dhidi ya Napoli ya Italia kulitoa nafasi kwa Samatta kuvaa kitambaa cha unahodha.

Samatta ameweka rekodi ya kuvaa kitambaa cha unahodha kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Awali, Samatta aliwahi kuvaa kitambaa cha unahodha kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’ dhidi ya Oostende, Septemba 21.

“Kuwa kiongozi si jukumu geni kwangu kwa sababu nimekuwa nikifanya majukumu hayo, nikiwa na timu ya Taifa ya Tanzania, lakini pia hata nikiwa huku Ubelgiji nimekuwa kiongozi kwa wengine.

“Kuwa kiongozi sio lazima mchezaji avae kitambaa cha unahodha. Nilikuwa nikifanya majukumu hayo kwa lengo la kuona tunapata matokeo mazuri katika kila mchezo,” anasema.

Advertisement

Samatta amewazidi kete Riyad Mahrez wa Manchester City, Maxwel Cornet (Lyon), Hakim Ziyech (Ajax) , Sadio Mane na Mohamed Salah wa Liverpool kwa kuvaa kitambaa cha unahodha katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza.

Tangu Mahrez ajiunge na Manchester City akitokea Leicester City, hajawahi kupata nafasi ya kuvaa kitamba cha unahodha hata katika mchezo wa kirafiki ambacho kimekuwa kikivaliwa na David Silva.

Pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kufunga, Cornet ambaye anafanya vizuri katika kikosi cha Lyon, hajawahi kufikiriwa kuiongoza timu hiyo, ambayo imekuwa ikiongozwa na Jean-Michel Aulas.

Ziyech aliyeonyesha uwezo mkubwa kwenye mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao Ajax iliifunga mabao 3-0 Valencia nchini Hispania, ameishia kumuona Dusan Tadic akivaa kitambaa cha unahodha ambacho msimu uliopita alikuwa akivaa libero wake wa zamani Matthijs de Ligt ambaye aliyejiunga na Juventus.

Washambuliaji hatari wa Liverpool, Mane na Salah hawajawahi kuvaa kitambaa cha unahodha kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, anayekivaa kwa majogoo hao wa Jiji ni Jordan Henderson.

Katika mchezo ambao Samatta aliweka rekodi hiyo huku KRC Genk ikitoka suluhu dhidi ya Napoli, alikuwa akipambana na Kalidou Koulibaly na Kastas Manolas ambao wanacheza nafasi ya beki wa kati katika kikosi hicho kinachonolewa na Mtaliano Carlo Ancelotti.

Kila alipokuwa akigusa mpira nyuma yake mmoja wa mabeki hao alikuwepo ili kumzuia mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Tanzania asilete madhara kwenye lango lao jambo ambalo walifanikiwa.

Samatta alionekana kutokuwa na madhara kwa Napoli hasa kipindi cha pili kutokana na KRC Genk kuamua kurudi nyuma kwa lengo la kutoruhusu bao kutokana na miamba hiyo ya soka Italia kushambulia kwa kasi.

Akizungumzia mchezo dhidi ya Napoli, Samatta anasema haikuwa kazi nyepesi kupata pointi moja kutokana na wapinzani wao hao kuwa na uzoefu wa kushiriki mashindano hayo makubwa Ulaya ngazi ya klabu.

“Nilicheza mbele ya mabeki bora . Hilo lipo wazi huwezi kutaja mabeki wanaofanya vizuri Italia na duniani kwa ujumla ukaacha majina yao, nilijitahidi kupambana ili kuhakikisha naisaidia timu yangu kwa asilimia zote,” anasema nyota huyo wa zamani wa Simba na TP Mazembe ya DR Congo.

Anaendelea, “Ugumu ambao tumekutana nao umeniachia somo na hata timu kwa ujumla tunapaswa kujiandaa kikamilifu kufanya vizuri mbele ya Liverpool kwa sababu ubora wa Napoli unaendana nao.”

Katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa ambao KRC Genk ilicheza dhidi ya FC Red Bull Salzburg, Samatta aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mashindano hayo makubwa Ulaya.

Pia Samatta alikuwa mchezaji wa kwanza wa Afrika Mashariki kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza.

Advertisement