Samatta azuiwa kwenda russsia

Thursday August 22 2019

 

By OLIPA ASSA

ACHANA na ile ‘hat trick’ aliyotupia wikiendi iliyopita dhidi ya Waasland Beveren, klabu iliyokuwa ikimtaka straika wa zamani wa Yanga, Heritier Makambo, unaambiwa isahau kabisa kumuona Mbwana Samatta akicheza soka Russia.

Hii ni baada ya baba yake kuzuia kabisa nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania kwenda nchini humo na kutaja sababu ya kumchomolea mwanaye dili hilo nono.

Samatta amepata dili tamu la kujiunga na Dynamo Kiev ya Urusi kwa dau la Euro 20 milioni (zaidi ya Sh 50 bilioni) ambalo ni kubwa kuzidi lile la klabu nyingine zikiwemo za Ligi Kuu England zilizokuwa zikimtaka kabla ya kuendelea kukipiga klabu yake ya Genk.

Licha ya dili hilo kuwa na dau nono, unaambiwa baba yake Mzee Ally Pazi Samatta, hataki kabisa kusikia na kutoa sababu kubwa ni aina ya soka la nchi hiyo, haamini kama litamuinua mwanaye badala yake anaona asubiri mpaka mwakani atakapomaliza mkataba wake ndipo asepe zake England.

Kama hujui ni kwamba msimu huu Samatta atacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na klabu yake ya Genk na hivyo ni moja ya sababu ya kugomewa na baba yake kukimbilia Russia, akiamini kupitia michuano hiyo atajitangaza kwani atacheza soka la ushindani zaidi.

“Samatta alikuwa tayari kwenda kucheza Dynamo Keiv ya Urusi baada ya kufikia dau ya Euro 20 milioni ambalo ilikuwa inataka Genk, sikumuunga mkono kwani naelewa soka la kule haliwezi kuendana naye,” alisema Mzee Samatta na kuongeza;

Advertisement

“Unajua Genk awali ilitangaza kumwachia Samatta kwa Euro 12 milioni (zaidi ya Sh 30 bilioni) na timu zikafikia dau, wakapandisha hadi Euro 15 zikafika na kuongeza tena hadi Euro 20 milioni, klabu ya Galatasary ya Uturuki ikafika mpaka 18 wakagoma hao wa Urusi ndio wakaja na hiyo ambayo sijataka aende.”

Mzee Samatta alisema anataka kumuona Samatta anacheza soka la England hata yeye ndio ilikuwa ndoto yake, lakini ameshauri saikolojia yake ielekeze afanye maajabu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA), kwani huko ataonekana huko na mkataba wake ukimalizika mwakani ataondoka akiwa huru.

“Ingawa alikuwa anaongea nami akionyesha ameumia, ila lazima apambane na changamoto hizo ili kufikia malengo yake,” alisema Mzee Samatta.

Msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, Samatta aliisaidia Genk kubeba taji, huku naye akinyakua tuzo ya Mwanasoka mwenye asili ya Afrika na kumaliza nafasi ya pili kwenye ufungaji bora wa ligi hiyo maarufu kama ‘Jupiler Pro’.

Msimu huu ligi ikiwa imeanza kuchanganya, Samatta tayari ameshatupia mabao manne katika mechi nne za ligi hiyo ikiwamo hat trick aliyofunga wikiendi iliyopita.

Advertisement