Simba yaichia Yanga msala Ligi ya Mabingwa Afrika

Muktasari:

  • Kutokana na utaratibu ambao Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ulivyo, Yanga inaonekana haina mtihani mkubwa katika raundi ya awali. Yanga kwenye raundi ya awali italazimika kukutana na timu moja miongoni mwa 41 kati ya 50 ambazo kila moja imetwaa ubingwa katika nchi yake. Katika kundi hilo la timu 50, tisa zinatoka kwenye nchi zitakazoingiza timu mbili mashindanoni.

UKISIKIA msala ndio huu. Ni wazi ratiba ya Ligi Kuu Bara iliyotolewa hivi karibuni inadhihirisha, Simba wataanzia raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wa 2019/2020, hivyo kuwaachia msala watani wao Yanga katika michuano hiyo ya CAF.

Kitendo cha Simba kupangwa dhidi ya JKT Tanzania kwenye ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, Agosti 23 ni uthibitisho kwamba mabingwa hao hawataanza raundi ya awali michuano ya Afrika, lakini watani wao wakipangwa kuanzia huko kama ilivyo kwa Azam na KMC zitakazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Kutokana na utaratibu ambao Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ulivyo, Yanga inaonekana haina mtihani mkubwa katika raundi ya awali. Yanga kwenye raundi ya awali italazimika kukutana na timu moja miongoni mwa 41 kati ya 50 ambazo kila moja imetwaa ubingwa katika nchi yake. Katika kundi hilo la timu 50, tisa zinatoka kwenye nchi zitakazoingiza timu mbili mashindanoni.

Vigogo hivyo tisa ni Wydad Casablanca (Morocco), USM Alger (Algeria), TP Mazembe (DR Congo), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Zesco United (Zambia), Al Merrikh (Sudan), Enyimba (Nigeria), Horoya (Guinea) na 1º de Agosto ya Angola. Timu hizo ukijumlisha na Simba zina uwezekano mkubwa wa kuanzia hatua ya kwanza zikizisubiria baadhi ya timu ambazo zitaanzia kwenye raundi ya awali, ikiwemo Yanga.

Kundi la timu 41 yoyote inaweza kukutana na Yanga kwenye hatua ya awali ni pamoja na SO de l’Armée ya Ivory Coast, Gor Mahia (Kenya), UD Songo (Msumbiji), AS Otoho (Congo), KCCA (Uganda), Asante Kotoko (Ghana), Rayon Sports (Rwanda), FC Platinum (Zimbabwe), Green Mamba (Eswatin), Mekelle 70 Enderta (Ethiopia), Township Rollers (Botswana), ASC Kara (Togo), UMS de Loum (Cameroon), Rahimo (Burkina Faso) na Cercle Mbéri Sportif (Gabon). Nyingine ni Buffles du Borgou (Benin), Aigle Noir (Burundi), CS Mindelense (Cape Verde), AS Tempête Mocaf (Afrika ya Kati), Elect-Sport (Chad), Fomboni (Comoro), AS Port (Djibout), Cano Sport (Guinea ya Ikweta), Brikama United (Gambia), UDIB (Guinea Bissau), Matlama (Lesotho), LPRC Oilers (Liberia), Fosa Juniors (Madagascar), Big Bullets (Malawi), FC Nouadhibou (Mauritania), Pamplemousses (Mauritius) na Black Africa (Namibia).

Pia kuna AS Sonidep (Niger), JS Saint-Pierroise (Reunion), UDRA (Sao Tome & Principe), Generation Foot (Senegal), Côte d’Or (Shelisheli), East End Lions (Sierra Leone), Dekedaha (Somalia), Atlabara (Sudan Kusini) na KMKM (Zanzibar). Hata hivyo wakati Simba akiponyeka na raundi ya awali, huku Yanga akiwa na dalili za kukutana na vibonde, wawakilishi hao wa Tanzania huenda wakakutana na kibarua kizito kwenye raundi ya kwanza.

Pia upo uwezekano kwao kukutana na kundi la timu nyingine 10 ambazo hazijatwaa ubingwa ila zimeingia kwa vile nchi zao zina nafasi ya kuingiza timu mbili kwenye mashindano hayo.

Timu hizo ambazo hazijatwaa ubingwa, lakini zitashiriki ni Raja Casablanca (Morocco), Etoile Du Sahel (Tunisia), Al-Ahly (Misri), JS Kabylie (Algeria), AS Vita Club (DR Congo), Orlando Pirates (Afrika Kusini), Green Eagles (Zambia), Al Hilal (Sudan), Kano Pillars (Nigeria), Hafia (Guinea) na Petro de Luanda (Angola).

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa amezitaka kujiandaa kikamilifu ili zifanikiwe kufanya vizuri kwa kuwa ndio silaha pekee ya ushindi.