Ushindi Taifa Stars uko hapa

Dar es Salaam. Wakati nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akitoa hamasa kwa wachezaji wa timu hiyo kupata ushindi dhidi ya Guinea ya Ikweta, safu ya ulinzi ya wapinzani wao ni dhaifu kipindi cha pili.

Akizungumza na gazeti hili, Samatta alisema wana deni kwa Watanzania katika mchezo huo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, saa moja usiku.

“Benchi la ufundi limeshatimiza wajibu wao, kazi iliyobaki ni wachezaji kucheza kwa nguvu, juhudi na maarifa ili kupata ushindi dhidi ya Guinea,” alisema Samatta.

Taifa Stars inatakiwa kutumia udhaifu wa mabeki wa Guinea inayofanya makosa zaidi kipindi cha pili kupata ushindi, ingawa inapaswa kucheza kwa nidhamu dakika zote 90.

Rekodi inaonyesha katika mechi 10 za mashindano ilizocheza Guinea imefungwa mabao 14, manane yalifungwa katika dakika za 52, 54, 57, 68, 74, 75, 83 na 90.

Taifa Stars katika mechi 10 imefungwa mabao 13 na imefunga manane, matano imefunga kipindi cha kwanza katika dakika za 6, 21 29, 39 na 40 ambapo matatu dakika ya 51, 57, 85.

Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji ana kazi kubwa ya kufanya katika mchezo huo. Mbali na Samatta, mshambuliaji anayecheza Difaa Al Jadida ya Morocco, Simon Msuva anapewa nafasi ya kung’ara katika mchezo huo kwa kuwa yuko katika kiwango bora.

Timu hizo zimecheza Afcon mara mbili kila moja na Guinea imewahi kucheza nusu fainali mwaka 2015 ilipokuwa mwenyeji huku winga wake Javier Balboa akiwa miongoni mwa wafungaji bora.

Taifa Stars imewahi kushinda idadi kubwa ya mabao 7-0 mara mbili dhidi ya Somalia, Desemba Mosi, 1995 na Desemba Mosi 2012 mechi zilizochezwa Uganda. Guinea ya Ikweta ilishinda mabao 4-0 dhidi ya Sudan Kusini Septemba 4, 2016.

Mchezaji hatari

Nahodha wa Guinea ya Ikweta Emilio Nsue anayecheza Apollon Limassol ya Cyprus ndiye tegemeo la mabao, amefunga mabao 11 kati ya 17 ambayo timu hiyo ilifunga katika michezo 10. Timu hiyo katika mechi 10 imeshinda mara tatu dhidi ya Sudan 4-1, Chad 2-1 na Sudan Kusini 1-0, imefungwa mbili ilipovaana na Saudi Arabia 3-2, Congo 1-0, imetoka sare tano dhidi ya Liberia 1-1,Chad 3-3, Sudan Kusini 1-1, Congo 2-2 na Togo 1-1.

Samatta, Nsue

Ukiachana na mabeki, Luis Maseguer, Carlos Akapo na Igor Engonga ambao kila mmoja amefunga bao moja, timu hiyo inamtegemea Nsue ambaye ndiye kinara wa kupachika mabao katika kikosi hicho.

Samatta katika michezo 50 amefunga mabao 17, Msuva (11) katika mechi 55 na Erasto Nyoni akiwa ni beki mwenye rekodi ya kufunga mabao matano Taifa Stars.

Mbali na Kelvin Yondani aliyecheza mechi 82 na Nyoni 88, kipa nguli Juma Kaseja anapewa nafasi ya kuibeba Taifa Stars kutokana na uzoefu wake kulinganisha na Felipe Ovono wa Guinea anayecheza Mekelle 70 Enderta ya Ethiopia. Wakati Kaseja akiwa na rekodi ya kucheza mechi 62, Ovono amecheza michezo 38.

Kauli za wadau

Kocha Kenny Mwaisabula alisema Taifa Stars ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo kama wachezaji wataamua.

Kocha wa Prisons, Mohamed ‘Adolf’ Rishard alisema Taifa Stars ikicheza kwa umakini itapata ushindi.

“Morali ya Watanzania kwa timu ya Taifa ni kubwa hiyo ni hamasa ya kutosha, pia wachezaji wetu wa kulipwa wamekuwa na mchango mkubwa wakishirikiana na wale wanaocheza nyumbani naamini kama watakuwa makini wana uwezo wa kushinda kwa idadi kubwa ya mabao,” alisema.

Mchambuzi Ally Mayay, alisema Guinea ya Ikweta sio timu nyepesi, lakini kama Taifa Stars itaweka dhamira ya kushinda mchezo huo nafasi ipo na utakuwa mwanzo mzuri wa kusaka tiketi ya kufuzu Afcon kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo 1980 na mwaka huu.

Kocha, TFF wafunguka

Rais wa TFF, Wallace Karia alisema mipango ni kuhakikisha Taifa Stars inafuzu kucheza Afcon na safari hiyo itaanza kesho. Karia alisema moja ya mikakati ya TF ni kuona Taifa Stars inashiriki mashindano ya CAF kwa kiwango bora na baada ya kufuzu Chan, sasa wameelekeza nguvu katika mchezo wa kesho ili timu hiyo ianze vizuri kampeni ya kufuzu kucheza Afcon 2021.

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alisema anaamini watakuwa na mwanzo mzuri katika mechi hiyo.

Ndayiragije ambaye ana historia ya kuiongoza Taifa Stars kucheza Chan 2020, alisema ameiandaa timu kwa kiwango bora katika mchezo huo.

“Tunahitaji kuanza vizuri kwa kupata ushindi mnono nyumbani, naamini vijana wangu hawataniangusha kwa sababu nia na uwezo wa kushinda wanavyo,” alisema Ndayiragije.

Kocha huyo raia wa Burundi amejaza nafasi ya Mnigeria Emmanuel Amunike aliyetimuliwa.