Alisson, Matip warejea Liverpool tayari kuivaa Manchester United

Muktasari:

Liverpool kwa sasa wanashikiria rekodi nzuri ya kushinda mechi zake nane ilizocheza hadi sasa katika ligi hiyo.

London, England. Liverpool imezidi kuimalika zaidi kuelekea katika mchezo wake dhidi ya Manchester United, baada ya kipa Alisson Becker na beki Joel Matip kurejea kikosini.

Kipa Alisson alikuwa nje ya uwanja tangu alipoumia misuli katika mchezo walioshinda dhidi ya Norwich City katika wiki ya kwanza ya msimu huu.

Matip naye aliumia wakati waliposhinda 1-0 dhidi ya Sheffield United alikosa mechi moja ya nyumbani ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Red Bull Salzburg pamoja na ile ya ligi dhidi ya Leicester City.

Wawili hao wamefanya mazoezi jana Jumanne kwenye Uwanja wa Melwood wakijianda kwa mchezo wa Jumapili dhidi ya Manchester United utakaopigwa Old Trafford.

Wakati Liverpool ikienda katika mchez huo ikiwa na kikosi bora wapinzani wao Manchester United wanaidadi kubwa ya wachezaji waliokuwa majeruhi kama Anthony Martial, Paul Pogba, Luke Shaw, Aaron Wan-Bissaka pamoja na kipa David de Gea.

Kikosi cha Klopp kinaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya point inane mbele ya mabingwa watetezi Manchester City. Liverpool kwa sasa wanashikiria rekodi nzuri ya kushinda mechi zake nane ilizocheza hadi sasa katika ligi hiyo.

Norwich, Southampton, Arsenal, Burnley, Newcastle, Chelsea, Sheffield United na Leicester zote zimefungwa na Liverpool pamoja na kuwa na mwanzo mzuri wa msimu, sasa miamba hiyo ya Anfield wanakwenda kwa watani zao wa jadi Manchester United, kwa lengo la kulinda rekodi yao ya ushindi ndani ya Old Trafford.

Mara ya mwisho zilipokutana hapo zilitoka suluhu, lakini sasa Man United kocha wake Ole Gunnar Solskjaer wamekuwa katika wakati mgumu kutokana na matokeo yasiyoridhisha.