Aussems atua Dar usiku akagoma kuzungumza

Muktasari:

Usiku wa leo Jumatano saa 4:15 kocha huyo aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa hapa Dar es Salaam, na kupokelewa na dereva wake.


Achana na taarifa za kocha wa Simba, Patrick Aussems kuwa ameshaoneshwa mlango wa kutokea baada ya kutokuwepo katika kituo cha kazi kwa muda wa siku tatu.

Usiku wa leo Jumatano saa 4:15 kocha huyo aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa hapa Dar es Salaam, na kupokelewa na dereva wake.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa limeweka kambi katika uwanja huo wa ndege tangu mchana lilimshuhudia Aussems akiwasili uwanjani hapo na kupokewa na dereva wake na Mwanaspoti alipomuona na kumfuata ili kuongea nae alikaa kata kata.

"Hapana, hapana, hapana," ndicho alichosema Aussems baada ya kufatwa na waandishi wa Mwanaspoti.

Aussems alikwenda moja kwa moja katika gari yake huku akiwa anamsubiri dereva wake ambaye alikwenda kulipia gharama za kuegesha gari na baada ya muda wakaondoka.

Wakati Aussems anawasili baadhi ya madereva wa taksi, wanaofanya kazi uwanja wa ndege walionekana kumuita kama kawaida yao uchebe! Uchebe! Uchebe! huku mwenyewe alionekana kuitikia akiwa anaelekea kwenye gari.