Azam yajitoa rasmi mbio za ubingwa Ligi Kuu, ni vita Simba na Yanga

Tuesday May 14 2019

 

By THOMAS NG’ITU

SARE ya 0-0 waliyoipata Simba dhidi ya Azam, imezidi kuwaondoa Azam katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu licha ya kwamba walifanya usajili mkubwa kwa ajili ya kufanya vizuri.

Azam msimu huu ilifanya usajili wa washambuliaji Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Danny Lyanga ili kuweza kuongez nguvu katika eneo la ushambuliaji.

Hata hivyo kwenye Ligi Kuu wameshindwa kuendana na kasi ya kugombea ubingwa na kuwaachia mbio hizo Simba na Yanga ambao wanafukuzana kileleni.

Azam wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 69 katika michezo 36 waliyocheza huku Yanga inayoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 80 katika michezo  35 waliyocheza wakati upande wa Simba wanashika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 82 katika michezo 33.

Gepu hili la pointi hata kama Azam wakishinda michezo yao miwili iliyobaki watakuwa wanafikisha pointi 75 kitu ambacho hakitofikia hata pointi za Yanga anayeshika nafasi ya pili.

Hata hivyo kubwa ambalo wanaweza kulingia hivi sasa ni baada ya kufanikiwa kuingia katika fainali ya Fa, ambapo watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Lipuli.

Azam bila shaka baada ya kupoteza matumaini ya kuchukua ubingwa msimu huu, nguvu zao watageuzia upande wa Fa ili kuhakikisha wanaweza kupata tiketi ya kushiriki katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Advertisement