Bosi Simba kufyeka masalia ya Aussems

Saturday December 14 2019

 

By Thobias Sebastian

UONGOZI wa Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, wanaendelea kufumua benchi la ufundi la timu hiyo baada ya kuachana na makocha wawili.

Simba walianza kuvunja mkataba wa kocha mkuu Patrick Aussems raia wa Ubelgiji na baadaye kocha msaidizi, Denis Kitambi na sasa mwingine anafuata.

Habari ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya bodi hiyo, zinaeleza baada ya kuachana na makocha hao sasa ni zamu ya mtaalamu wa misuli Mjerumani Paul Gomez, na kubwa linalomwondoa ni kukosa sifa sahihi ya kuwepo hapo.

Simba ilimwajiri Gomes walipoweka kambi yao Afrika Kusini wakijiandaa na msimu huu wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo walitolewa hatua ya awali. “Unajua tupo katika wakati wa kujenga timu bora maeneo yote na kuwaweka watu sahihi ambao wanastahili, kwa maana hiyo tunaboresha kila mahala na mpaka tumeamua kuachana na Gomez basi kuna mambo hayapo sawa.

“Ambalo nafahamu Ofisa Mtendaji mkuu wetu Senzo Mazingisa, kwa sasa anajenga timu na kila mahala kuwa na mtu sahihi, kwa maana hiyo alipofika upande wa Gomez, kuna vitu alimwomba nadhani alishindwa kumpatia, hilo ndio tatizo nafikiri linaweza kumwondoa.

“Wakishindwana basi ataondoka na nafasi yake itachukuliwa na mtu mwingine sahihi wa kusaidia wachezaji weweze kupona kwa haraka pindi wanapopata majeraha. Sababu nyingine ambayo nadhani imemweka katika wakati mbaya Gomez ni majeraha ya John Bocco, ambayo yameonekana kutokuwa ya kukaa nje kwa muda mrefu lakini kwake limeonekana tatizo mpaka yakafanyika maamuzi ya kumpeleka Afrika Kusini.”

Advertisement

Wakati huo huo, kuna taarifa nyingine uongozi wa Simba upo kwenye mpango wa kuachana na kocha wao wa makipa Mharami Mohammed ‘Shilton’ na nafasi yake itachukuliwa na Mkenya Iddi Salim, aliyewahi kuwanoa makipa wa timu hiyo miaka ya nyuma.

Hata hivyo, alipotafutwa Senzo kuelezea taarifa hizo, alikuwa mzito kuzitolea ufafanuzi huo ingawa alisema kila kitu ndani ya Simba kinazingatia muda wa kujibu baada ya kufikia maamuzi na kwa sasa hana taarifa zozote kuhusu makocha hao.

Wakati hayo yakiendelea, Gomez na Shilton walikuwepo katika mazoezi ya jana yaliyofanyika kwenye uwanja wao wa Mo Simba Arena uliopo Bunju B, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

MATOLA AFUNDWA

Jana Ijumaa mchana, Kocha mkuu wa Simba Mbelgiji Sven Vandenbroeck, alikutana na benchi la ufundi la timu hiyo kisha kufanya nao kikao ambacho muda mwingi alikuwa akizungumza na msaidizi wake, Seleamni Matola.

Kikao hiko kilichofanyika kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Mbweni, Sven baada ya kumaliza kuzungumza na viongozi wengine wa benchi la ufundi alionekana kuwa na Matola ambaye alimpa ruhusa ya kuwa na nguvu ya kushauriana masuala ya kiufundi na muda mwingine kusimamia mazoezi.

Matola alisema amepata kocha ambaye atakuwa akishauriana naye kwani hata katika kikao chao walipanga mipango na ratiba kamili ya timu, kushirikiana masuala ya kiufundi na mambo mengine yote ya kimsingi.

“Tumezungumza vizuri na mambo mengine ya ndani ambayo nina imani tutakwenda kuyafanyia kazi kwa pamoja tukishirikiana ili kuhakikisha timu inafikia yale malengo ambayo tumejipangia kwa pamoja,” alisema Matola.

Advertisement