CAG akitua Yanga Zahera asemaje dili la Kindoki?

Muktasari:

  • Na Harmonize akasema atatii wito wa Rais. Halafu mambo yakimnyookea hivyo, kaka zao, Ali Kiba na Diamond Platnumz wao wanagombea penseli! Hili linajadilika vipi kwa Luqman Maloto na Dk Levy.

DK John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimpigia pande la ubunge Harmonize kiaina, aliposema angetamani awe mbunge wa Tandahimba.

Na Harmonize akasema atatii wito wa Rais. Halafu mambo yakimnyookea hivyo, kaka zao, Ali Kiba na Diamond Platnumz wao wanagombea penseli! Hili linajadilika vipi kwa Luqman Maloto na Dk Levy.

LUQMAN: Tuanze na mada ipi? Penseli au Zahera?

DK LEVY: Hata sielewi bado nasubiri matokeo ya Misri, maana runinga zetu hazikuonyesha. Nawasubiri wakifika airport waniambie wametandikwa ngapi?

LUQMAN: Toa maoni yako ukijenga hoja yenye vielezi na vihisishi bila vivumishi, ukiongozwa na matokeo ya Yanga kuwatandika Pyramids 3-0.

DK LEVY: Sasa umri huu nitoe maoni ya umbea? Sina matokeo nasubiri watue pale Kipawa ndo wanijulishe. Wakishanijulisha ndo utapata maoni yangu. Mimi sipendi kuamini katika maneno ya kuambiwa na watu sampuli yako. Maana ninyi ndiyo mliotuaminisha kuwa Bigirimana na Sibomana ni mafundi wa Kinyarwanda. Molinga na yule mwenzake anayecheza mpira kama roboti ni mafundi. Na ninyi ndo mliotuaminisha kuwa Shikalo ni kipa bora kuwahi kutokea. Pia ninyi ndo chanzo cha mimi kuamini kuwa yule dalali wa vumbi la Kongo ni kocha mzuri. Niacheni kwanza mpaka wafike.

LUQMAN: Basi toa maoni kutokana na minong’ono kuwa Yanga wamebugizwa na Pyramids 3-0.

DK LEVY: Naona umeamua kutonielewa au umeamua kunisumbua. Sipendi kujadili minong’ono wala tetesi. Sipendi kuishi kwa kudhani na kuhisi. Napenda uhakika. Mimi

nilipoona yule dalali wa vumbi la Kongo anatuaminisha kuwa yule Kindoki ni bora kuliko Kabwili. Nikaona kabisa hapa hamna kitu na anatakiwa kushitakiwa kwa utakatishaji pesa.

Kumlipa mshahara Kindoki kama golikipa ni utakatishaji pesa wa wazi kabisa ule. Na ndo hapo sasa nakosa imani na uwezo wa kujua soka kwa watu wa Gongowazi. Kuanzia viongozi, wanachama na mashabiki pamoja na wafurukutwa. Mnaishi na wapiga dili miaka miwili bila kujua kuwa hawa ni wapigaji mnaona ni wachezaji na wafundishaji? Kwenye hili Masela wale wauza vijora wa Msimbazi wangeshitukia kwa mechi ya kwanza tu ya watan ambayo dalali yule aliopaki basi dakika ya kwanza mpaka ya tisini.

LUQMAN: Basi nakupa nafasi uwakaribishe Yanga nyumbani washughulikie viporo. Kimataifa ndio hivyo tena.

DK LEVY: Unajua ubongo wangu nimeusuka kimataifa. Hapa nyumbani sifuatilii chochote. Ligi haina mdhamini. ‘Kariakoo Dabi’ mechi ya mzunguko wa kwanza na wa pili

wanakutana kwenye mzunguko mmoja wa pili. Msimu uliopita Gongowazi na Wauza Ukwaju walikutana mechi mbili zote ndani ya raundi ya pili. Ligi gani usajili tu unatosha kukuonesha nani bingwa wa msimu? Ligi gani makocha wazawa waliochezea timu kubwa wakifundisha timu ndogo wanapokutana na timu zao za zamani wanafungwa kirahisi? Halafu wa timu kubwa

wanajisifu wazi kabisa kuwa yule kocha ni wetu hatusumbui? Ligi gani kiongozi akiwa shabiki wa timu fulani basi hiyo timu inafanya vyema mpaka aachie madaraka? Unaacha kumfuatilia mwanao anaendeleaje na masomo unafuatilia ligi ya vigodoro? Achana na mimi aiseee.

LUQMAN: Niachane na wewe au Ligi ya Tanzania Bara ndio iachane na wewe? Naona unataka kuniunganisha kwenye msongo wako wa mawazo. Simo huko aisee.

DK LEVY: Tunakoelekea tutasikia Steve Nyerere kawa kiongozi wa TFF au Yanga. Maana siku hizi ukiwa maarufu tu unaweza kuwa mtangazaji, mwanasiasa, mchambuzi wa soka na msemaji wa timu kubwa kubwa. Achana na vyeti na uzoefu siku hizi hangaikia jina tu.

Waliowalipa watangazaji ili watajwe kwenye redio ndiyo wamekuwa watangazaji wa kuaminiwa. Najua utashangaa mbona nimehamisha ‘topiki’. Nami nitakushangaa wewe kushanishangaa.

LUQMAN: Kati ya Steve Nyerere au Idris Sultan nani anafaa kuwa kiongozi wa Yanga au TFF? Usiniulize nimekuuliza kwa nini. Mimi nauliza zangu tu.

DK LEVY: Tatizo lako unapenda kushindanisha vitu badala ya watu. Hao siyo watu ni vitu. Ni ngumu sana kujua wale jamaa kama ni wachekeshaji, wazururaji, waburudishaji au wazugaji. Nasisitiza tena na tena usishangae Steve Nyerere akawa kiongozi mkubwa wa Yanga.

LUQMAN: Kwani Steve Nyerere mbali na kuchangisha rambirambi na uongozi anauweza? Naona unamsifia sana. Mimi naona bora timu apewe Pierre Liquid.

DK LEVY: Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Laiti kama angekuwa na fursa ya kupitia hesabu za Simba na Yanga. Viongozi wengi wa mpira wangekuwa jela.

Misiba ya Bongo Movie na Bongo Fleva. Kuna msela angekuwa jela toka 2012 huko. Na angepitia hesabu za familia ambazo zina mababa mafuska. Ingependeza sana. Wazee wengi wangekuwa jela kwa matumizi ya ovyo ya vipato vyao. Ujue kuna dada anakuambia kazi yake ni msanii wa Bongo Movie. Halafu hana hata filamu yake moja. Hata alizoshirikishwa hazizidi mbili. Lakini uwezo wake wa kipesa ni zaidi ya Naibu Waziri. Hana kazi nyingine yoyote. Anapata wapi? Ujue kuna madingi ya ovyo yanakatunza kwa njia za panya.

LUQMAN: Kwani wale wanaogombea penseli hawahongi? Na wenyewe si tunaambiwa wana mkwanja mrefu?

DK LEVY: Wale wazee wa kuongeza sifuri wajanja wajanja? Wale ni Zahera mmoja kwenye miili ya watu wawili. Wameshatufanya watu mabwege. Lakini safari hii wameelewa kuwa utoto wao wa kitapeli umeshitukiwa. Akili zao zitafutika kama penseli zenyewe zinavyofutika.

LUQMAN: Hebu fafanua hapo Daktari, wanafutikaje?

DK LEVY: Kwani upenseli wao unaona umebamba kama zamani? Muda wao na kile kizazi chao walichokishikia akili za kiki kinaanza kupata majukumu. Wako ‘bize’ kimaisha zaidi. Wanachotakiwa kwanza ‘bifu’ lao la uzushi lile waliue waje kivingine. Masikio ya watu yametoa talaka rejea na mtindo wao wa kusutana kama wake wenza kabla ya kutoa ngoma au kufanya kitu. Kifupi ni kwamba Team Konde Gang itawatawanya kikatili sana wakiendelea na mtindo wa kale wa kulumbana kama Khadija Kopa na marehemu Nasma Khamis Kidogo.

Umesahau kuwa hata Choki na Banza walikuwa hivi baadaye watu wakawachoka? Umesahau Nice na Dudu? Hukumbuki hata O Ten na Afande wa Moro? Nature na Inspekta? Wote hao ilifika wakati kusutana kwao kukawa siyo dili mjini. Sasa hawa kama wako vyema kimkwanja wafanye maisha kuwa kitu chepesi kama jivu la karatasi. Ujue hata upinzani wa Simba na Yanga umeanza kupungua makali? Ndo maana Simba wanajaza kuliko Yanga. Ina maana Simba wamekuwa wengi kuliko Yanga.

LUQMAN: Tatizo wewe jamaa mbaguzi sana. Kama penseli angekuwa kaibiwa Diamond ungezoza weeee, ila kwa vile kaibiwa Kiba na anamtuhumu Diamond, unaamua kujenga hoja za mikausho.

DK LEVY: Hivi sasa mwanamuziki ni kufanya muziki au biashara. Sasa wengine wanaanzisha miradi wengine wanaanzisha malumbano. Haya nieleze na wewe sasa huu mwaka wa ngapi unasikia malumbano tu?

LUQMAN: Si unajua mimi nilichelewa kuja mjini? Sielewi chochote. Ninachojua Harmonize sasa hivi anamfunika Diamond kwa mabaunsa.

DK LEVY: Unapenda sana kuchelewesha kesi kwa kutoa ushahidi wa uongo. Konde Boy anawafunika kila sehemu. Unataka kusema nini mtu anayepewa Ubunge na rais wa nchi kwa ubora wa ngoma zake? Unataka kusema nini zaidi ya mtu anayealikwa kwenye tukio kubwa kama kuzima mwenge siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa hili? Anatumbuiza na kuwashusha viongozi wote jukwaani kwenda kuimba naye? Wabongo mnachelewa sana kuelewa yanayoendelea. Sasa wewe endelea kuwaamini vipenseli wakati dunia yote imehamia Konde Gang.