Chirwa ameipeleka Yanga Fifa kisa...

Tuesday March 24 2020

 

MSHAMBULIAJI wa Azam, Obrey Chirwa ameipeleka klabu yake ya zamani Yanga katika Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), kutokana na madai ya fedha ambayo anaidai timu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili alichokuwa anaitumikia kuanzia mwaka 2016-18.

Chirwa anasema baada ya kuondoka Yanga na kwenda katika timu ya Nogoom FC ya Misri aliwaandikia barua uongozi wa timu hiyo kuomba pesa zake ambazo alitakiwa kupewa katika kipindi anasaini mkataba pamoja na nyingine ambazo alitakiwa kupata akiwa ndani ya mkataba.

“Niliandika barua kwa uongozi wa Yanga kuomba wanilipe pesa zangu ikiwemo mshahara na ile ambayo hawakunimalizia wakati nasaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo, lakini mpaka sasa nimerudi hapa nchini nacheza Azam hakuna chochote ambacho nimepata,” alisema mchezaji huyo huku akifanya siri kiwango halisi.

“Baada ya kuona hili linashindikana niliamua kufuata kanuni ambazo zinaeleza kwa kwenda TFF na kuwaeleza nikiwa na barua mkononi niliyowatumia Yanga na ni zaidi ya mwaka uliopita bila ya majibu yoyote.

“TFF waliniita na kunisikiliza kwa siku tofauti lakini napo sikupata majibu juu ya malipo ya pesa yangu ndio wao wakanipatia barua ya kwenda Fifa, kuwaeleza hili na wamelifanyia kazi kutokana na vielelezo ambavyo ninavyo kutoka TFF na Yanga na wamenipatia barua,” alisema.

“Fifa baada ya kusikiliza malalamiko yangu wamenipatia barua ambayo inaonyesha natakiwa kuipeleka Yanga na wao watoe majibu pesa yangu watanipatia lini au watanilipa kwa namna gani mpaka yote imalizike,” alisema Chirwa ambaye amekuwa na kiwango kizuri kwa sassa ndani ya Azam. “Leo (Jana) asubuhi nimeichukua barua hiyo na kuipeleka katika ofisi za Yanga zilizopo Jangwani na baada ya muda mfupi nategemea kupata majibu kutoka Fifa, nitalipwa lini na kwa njia ipi kwani wao ndio wana jukumu la kulisimamia hili kwa hapa lilipofikia,” aliongezea Chirwa.

Advertisement

Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kwa vile wao ni wapya madarakani hawana taarifa na suala hilo lakini kama mchezaji huyo atawapelekea vithibitisho kamili watalifanyia kazi.

Advertisement