Eymael apewa onyo, Yanga yapigwa faini Sh1.2 milioni

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Luc Eymael amepewa onyo huku wachezaji wake, Mrisho Ngassa, Ramadhani Kabwili na Cleofas Sospeter wakifungiwa mechi tatu na faini ya Sh500,000 Kila mmoja.

Eymael amepewa onyo baada ya hivi karibuni kutoa malalamiko juu ya ubaguzi wa rangi kutoka kwa mwamuzi Hans Mabena baada ya kumalizika mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Azam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mng'uto amesema kikao cha Kamati ya Saa 72 nilichokaa Januari 20 kimetoa uamuzi wa kumpa onyo Eymael kwa kutoa maneno makali ya ubaguzi wa rangi huku wakiitaka Yanga kutoa tamko ya kupiga kauli ya kocha huyo.

"Haiingii akili mtu anapewa kadi halafu nampa mkono mwamuzi pale pale. Na maneno aliyoyasema kuwa amebaguliwa sio sawa kwani nchi yetu haijawahi kuwa na jambo kama hilo," amesema Mng'uto.

Wakati huo huo Ngasa, Kawili na Sospeter pamoja na wachezaji wawili wa Mbeya City, Kelvin John na Majaliwa Shabani wamefungiwa mechi tatu na faini ya Sh 500,000 kila mmoja.

Mng'uto alisema wachezaji hao walitegeana kutoka uwanjani kwenda katika vyumba vya kubadilisha nguo katika mchezo kati ya Mbeya City dhidi ya Yanga jambo lililosababisha Polisi kuingilia kati kuwatoa kwa nguvu.

"Hairuhusiwi Polisi kuingia katika sehemu ya kuchezea (pitch), lakini wachezaji hao walisababisha kutokea Polisi kuingia uwanjanj nankutumia nguvu,hivyo wamepewa adhabu kwa mujibu wa kanuni ya 38(9)e.".

Pia Yanga na Prisons zimepigwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kutowasilisha vikosi vyao wakati wa kikao cha kabla ya mechi.

Adhabu kwa Yanga haikuishia hapo kwani imepigwa faini ya Sh 500,000 kutokana na mashabiki wake kurusha chupa uwanjani na kuwarushia chupa waamuzi katika mchezo wa Simba na Yanga uliofanyika Januari 4.

"Pia wamepigwa tena faini ya Sh200, 000 kwa kosa la kutumia chumba kisicho rasmi katika mchezo dhidi ya Simba" amesema Mng'uto.