VIDEO: Failuna ang’ara, Giniki achemka Bagamoyo Marathoni 2018

Muktasari:

  • Failuna aliibuka kinara katika mbio za nusu marathoni (kilomita 21) akikimbia kwa saa 1:16:21 akimpiku Mkenya, Shelmitu Muriua aliyemaliza wa pili akitumia saa 1:17:36.

Bagamoyo. Mwanariadha, Failuna Abdi ameing’arisha Tanzania kwenye mbio za Bagamoyo Historical Marathoni zilizofanyika jana mjini hapa huku nyota Emmanuel Giniki akichemka.

Failuna aliibuka kinara katika mbio za nusu marathoni (kilomita 21) akikimbia kwa saa 1:16:21 akimpiku Mkenya, Shelmitu Muriua aliyemaliza wa pili akitumia saa 1:17:36.

Hadi wanafika kilomita 16, wanariadha hao walikuwa sambamba wakichuana kabla ya Failuna kumzidi mpinzani wake sekunde chache kabla ya kumaliza mbio.

“Mpinzani wangu alikuwa fiti, tulikwenda sambamba muda mrefu, tukiwa tunaelekea ukingoni niliongeza kasi hakuweza kunifuata,” alisema Failuna.

Giniki aliyeambulia nafasi ya sita akizidiwa na bingwa Bernard Musa kutoka Kenya aliyekimbia kwa saa 1:04:34. Mwanariadha wa timu ya Taifa, Ezekiel Ngimba alimaliza wa pili akitumia saa 1:04:35.

Hata hivyo, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) lilitangaza kutowapa zawadi wanariadha kutoka Kenya waliofanya vizuri kwa madai walikuja nchini bila kupata vibali vya Shirikisho la Riadha Kenya.

Naibu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla alitoa zuio hilo dakika chache kabla ya mchakato wa kutoa zawadi kuanza akidai ni maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wilhelim Gidabuday.

Tamko la RT lilisababisha wanariadha wa timu ya Taifa Marco Joseph, Emmanuel Giniki na Dickson Marwa kuondoka na zawadi za mshindi wa pili hadi wa nne, huku Jafari Ngimba aliyemaliza wa pili akichukua medali ya mshindi wa kwanza na fedha Sh1 milioni.

Kwa wanawake Angeli John na Catheline Modest walichukua zawadi za mshindi wa pili na watatu ambazo washindi wake walikuwa Wakenya.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla aliyekuwa mgeni rasmi aligeuka kivutio baada ya kuwa miongoni mwa wanariadha waliokimbia na kumaliza mbio za kilomita 21.

Kigwangalla alisema mbio hizo zina mchango katika utalii wa ndani kwenye mji wa Bagamoyo ambao una vivutio vingi na aliwapongeza waandaaji kufanikisha mbio hizo.

Mratibu wa Bagamoyo Marathoni, Deogratius Soka alisema mbio hizo zinafanyika kwa mara ya tano mfululizo na zimekuwa na hamasa kubwa. ndani na nje ya Bagamoyo.