Himid Mao bado majanga

KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Himid Mao 'Ninja' amezidi kumnyima raha Kocha wake wa ENPPI nchini Misri, Helmi Toulan kwa kukosa huduma yake  kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
Toulan atamkosa Himid katika mchezo wa Ligi Kuu Misri utakaopigwa kesho dhidi ya Tanta.
Kocha huyo ambaye amekuwa akimtegemea Himid katika eneo la kiungo, imembidi kutumia mbinu mbadala kuhakikisha pengo lake linazibwa katika kikosi hicho ambacho maskani yake ni jijini Cairo.
Kukosekana kwa Himid, kumemfanya kocha huyo, kumtumia Mohamed Rizk katika michezi mitano ya  Enppi SC.
Akizungumzia maendeleo yake, Himid anayesumbuliwa na tatizo la misuli, alisema anaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi mepesi hivyo siku chache zijazo anaweza kuanza program na kikosi cha kwanza.
“Nipo katika hatua za awali za kurejea katika hali yangu ya kawaida baada ya kupata matibabu, nashukuru wote ambao wamekuwa pamoja namimi  katika kipindi hiki ambacho nilikuwa nikiuguza majeraha,” alisema.
Enppi SC ilikuwa miongoni mwa timu ambazo zipo katika hatari ya kushuka daraja, lakini kwa sasa wapo  nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi hiyo yenye jumla ya timu, 18 huku wakiwa wamejikusanyia pointi 23 katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.