Jicho la Mwewe: Hizi hapa hesabu za kilevi kundi la Taifa Stars

Muktasari:

  • Na sasa tumeanza mapema kupiga hesabu za kilevi kuelekea Afcon 2021 pale Cameroon. Kwanza kabisa wageni wetu hawakuwa tishio. Guinea ya Ikweta ilikuwa moja kati ya timu mbovu ambazo Taifa Stars imewahi kucheza nazo Uwanja wa Taifa.

SALUM Aboubakar ‘Sure boy’ ndiye mchezaji aliyeturudisha katika hesabu za kilevi za Kundi J katika pambano kati ya Taifa Stars dhidi ya Guinea ya Ikweta Ijumaa usiku pale Uwanja Mpya wa Taifa. Tutaiuta uwanja mpya mpaka lini? Sijui.
Katika dakika nne za mwisho za nyongeza alipokea pasi kutoka kwa Ditram Nchimbi akiwa amesimama mita 25 kutoka katika lango ya Guinea ya Ikweta na kupiga shuti kali ambalo lilikwenda moja kwa moja katika nyavu.
Lilikuwa bao la ushindi kwa Taifa Stars. Bao la pili. Baada ya bao la kwanza la kizembe la wageni. Naamini Juma Kaseja hakulitendea haki shuti la bao la wageni. Baadaye Simon Msuva akalazimisha na kusawazisha. Baadaye ndio likaja bao hili la Sure Boy.
Na sasa tumeanza mapema kupiga hesabu za kilevi kuelekea Afcon 2021 pale Cameroon. Kwanza kabisa wageni wetu hawakuwa tishio. Guinea ya Ikweta ilikuwa moja kati ya timu mbovu ambazo Taifa Stars imewahi kucheza nazo Uwanja wa Taifa.
Bao lao lilikuja likiwa shuti la kwanza ambalo waliliielekeza katika lango la Kaseja. Kabla ya hapo, na baada ya hapo hawakuonekana kuwa tishio kwa Stars. Walipoteza mipira ovyo. Walishindwa kutengeneza mashambulizi. Hawakuwa tishio.
Bao lao liliwachanganya wachezaji wa Taifa Stars, benchi la ufundi na mashabiki wa Taifa Stars. Hakuna aliyetegemea. Baadaye wachezaji walionekana kuchanganyikiwa zaidi na kushindwa kujua namna ya kutulia na kufanya walichotakiwa. Kipindi cha pili Msuva na Sure Boy wakabadili kila kitu.
Na sasa tumeanza kupiga hesabu za kilevi katika Kundi J. zinakwenda hizi. Tunisia wanaongoza katika kundi. Stars ni ya pili. Mechi inayofuata ni Stars dhidi ya Libya ugenini. Bahati nzuri kwa Stars mechi yenyewe itachezwa Tunisia. Wenyeji Libya wameamua mechi hii ichezwe katika ardhi ya Tunisia kwa sababu kwao kuna machafuko.
Stars inahitaji pointi zote tatu dhidi ya Libya. Ikishindwa basi ichukue pointi moja tu. inamaanisha itakuwa na pointi nne. Wakati huo huo, Tunisia ana asilimia kubwa ya kumfunga Guinea ya Ikweta ugenini. Hii ina maana Tunisia itakuwa na pointi sita, Stars itakuwa na pointi nne na Libya itakuwa na pointi moja.
Raundi ya tatu Stars itacheza na Tunisia Dar es Salaam. Sioni Stars ikipoteza mechi hii itashinda au itatoka sare. Kwa kuepuka kutia chumvi mambo tunaweza kusema Tunisia itatoka sare Uwanja wa Taifa dhidi ya Stars. Hii itaifanyaTunisia iwe na pointi saba huku Stars ikiwa na pointi tano.
Wakati huo huo naweza kuona Libya ikitoka sare na Guinea ya Ikweta ugenini pale Malibo. Hii itaifanya ifikishe pointi mbili huku Guinea ya Ikweta ikibeba pointi yake ya kwanza. Mechi yetu marudiano dhidi ya Tunisia itakuwa ngumu na tutapoteza ugenini. Tunisia itapata pointi 10 na sisi tutabakiwa na pointi tano.
Wakati huohuo Libya anaweza kumfunga Guinea ya Ikweta pale Tunisia na kutufikia. Pambano baina yao na sisi Dar es Salaam litakuwa fainali na kuna uwezekano mkubwa tukaifunga Libya na kufikisha pointi nane. Hii inamaanisha kwamba tutaiacha na pointi zake tano na sisi tutafuzu. Wakati huo huo Tunisia itafuzu kwa kuichapa Guinea ya Ikweta. Itafikisha pointi 10.  
Hii ina maana kwamba Guinea ya Ikweta itakuwa imetupwa nje ya michuano. Wakati huo huo Stars itasafiri mpaka Guinea ya Ikweta na kwa jinsi nilivyowaona wenyeji wetu hapa Dar es salaam basi hawataweza kuepuka kichapo.
Wakiwa kwao, Guinea ya Ikweta hawatajiangusha. Hawatacheza kwa kujihami. Na hili naliona kama pambano ambalo Stars itashindilia kufuzu kwake wakiwa ugenini. Kama Guinea ya Ikweta wakiambulia sare bado tutakuwa tumeshindilia kufuzu.
Sioni pia Libya akimfunga Tunisia mechi ya mwisho. Mechi hii, kama ilivyo ya awali itachezwa Tunisia. Ingawa mpaka wakati huo Tunisia itakuwa imefuzu lakini Waarabu hawana tabia ya kujidhalilisha kwa kukubali kufungwa nyumbani.
Libya imefanya kosa kubwa kutaka mechi zake zote mbili dhidi ya Tunisia zichezwe Tunisia. Naona ikiiachia Tunisia pointi zote sita. Sisi tuna mechi ngumu dhidi ya Tunisia ugenini, lakini katika Uwanja wa Taifa haitaweza kutoka.
Hizi ni hesabu za kilevi lakini zinawezekana. Stars wana nafasi kubwa ya kurudi Afcon kwa mara ya pili mfululizo.
Kwa jinsi makundi yanavyopangwa nyakati hizi, sioni kama itatuchukua miaka 39 kurudi tena katika michuano hii. Haiwezekani.
Lakini kwanza tuwachape Libya au tutoke nao sare kesho katika pambano la ugenini Tunisia.
 Hakuna kisichowezekana. Kitu cha muhimu katika mwanzo wetu lilikuwa bao la Sure Boy.
Bila ya bao lile hesabu za mlevi zingekuwa ngumu zaidi kukubali. Lakini kwa sasa tunaweza kwenda mwendo mdundo na kufanikiwa tena kufuzu AFCON na kwenda Cameroon.